• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 7:47 PM
GWIJI WA WIKI: Meja Bukachi

GWIJI WA WIKI: Meja Bukachi

Na CHRIS ADUNGO

MWANADAMU lazima awe na malengo maishani. Pania kuyatimiza hayo maazimio yako kabla ya kufa. Usiondoke duniai bila kuacha lolote lenye mashiko.

Kabla ya maisha kuisha, hakikisha kwamba lipo jambo – japo moja – ambalo waliosalia duniani watakukumbukia nalo.

Ukiwa mwimbaji, imba angalau ubeti mmoja tu utakaosikilizwa wakati wa kupumzika kwako ukiwadia. Ukiwa kiongozi, jenga daraja bora la mapatano na ulizindue; na iwapo umejaliwa mkono wa kuandika, basi andika na uandike bila hofu!

Kumbusha watu kuhusu umuhimu wa maisha na waeleze ubora wa kutenda mema kabla hawajaisha!

Huu ndio ushauri wa Bw Meja S. Bukachi – mwalimu wa Kiswahili, mwandishi wa vitabu, mwanahabari na mjasiriamali ambaye kwa sasa ni mhariri wa miswada katika kampuni ya Bestar Publishers na mhariri wa Chama cha Kiswahili cha Nakuru (CHAKINA).

MAISHA YA AWALI

Meja amelelewa katika familia ya walimu. Mbali na nduguye Elphaz Shigugu Bukachi wa Shule ya Msingi ya Ingotse, Kakamega; nduguze wengine wawili kati ya saba pia ni walimu.

Hawa ni Philip Masaga Bukachi na Duncan Bukachi wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Ebutenje katika Kaunti ya Kakamega. Nduguze wengine ni Violet Bukachi, Hoglah Bukachi, Daniel Bukachi na Byrum Sunguti ambaye ni Luteni wa Kanisa la Jeshi la Wokovu katika Jimbo la Vihiga.

Meja alizaliwa kijijini Eshilakwe, eneo la Lurambi, Kaunti ya Kakamega. Ni mwana wa saba katika familia ya watoto wanane wa Bw John Bukachi Sunguti almaarufu ‘Mzee wa Job’ na Bi Gladys Mmbone Bukachi.

Alianza safari ya elimu katika Shule ya Msingi ya Eshilakwe alikolainishwa na Mwalimu Mary Namayi ambaye alimpokeza malezi bora ya kiakademia. Meja alifanyia mtihani wa kitaifa wa darasa la nane (KCPE) shuleni Eshilakwe mwishoni mwa 2004.

Licha ya kufaulu vyema katika KCPE na kupata nafasi katika Shule ya Wavulana ya Kakamega na Shule ya Wavulana ya Lubinu, Kakamega; uchechefu wa karo ulimlazimu kujiunga na Shule ya Upili ya Sirigoi katika eneo la Navakholo, Kakamega akiwa mwanafunzi wa kutwa. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2009.

Meja anatambua jitihada za wazazi wake katika kumlea kwa kumcha Mungu, kupenda amani na kuwaheshimu watu wote – wakubwa kwa wadogo.

Anakiri kuwa asingekuwa ‘Meja’ mwenye mapenzi kwa taaluma yake isingekuwa kwa ushajiishaji na uelekezi wa Bw Geoffrey Furechi, Peter Cetera Okova, Bw Khakali, Bw Josephat Matikho na Bw Shadrack Nashilobe waliomfundisha shuleni Sirigoi na Bi Violet Chimika na Bw Njuguna waliomtandikia zulia zuri la elimu shuleni Eshilakwe.

Wengine waliomchochea zaidi kitaaluma ni Bw Mugo Maina almaarufu ‘Balozi Ustadh’, Bw Mugendi Mutegi almaarufu ‘Msafiri Makini’, Bi Shelmith Weru wa Moi Forces Academy – Lanet, Bw Brian Kimutai Rop, Bi Terry Ambundo na Bw Nahashon Akunga Nyangeri ambaye alikipalilia kipaji chake katika sanaa ya uandishi.

UALIMU

Meja alihitimu stashahada katika ualimu (Kiswahili na Historia) kutoka Chuo cha Mafunzo ya Ualimu cha Lanet, Nakuru mnamo 2014 na kuanza kufundisha katika Shule ya Upili ya Anestar, Nakuru.

Haja ya kujiendeleza kitaaluma ilimfanya kujiunga na Chuo Kikuu cha Mount Kenya (MKU) mwaka uo huo wa 2014 na akahitimu Shahada ya Ualimu mnamo 2016.

Meja pia amewahi kufundisha Kiswahili katika Shule ya Upili ya Ematiha, Kakamega kwa kandarasi ya bodi pindi tu alipokamilisha KCSE. Yeye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili na Historia katika Shule ya Upili ya Anestar Premier, Nakuru.

UANAHABARI

Moto wa Meja katika fani ya uanahabari uliwashwa na aliyekuwa mwanahabari mahiri wa kipekuzi, Mohamed Ali ‘Jicho Pevu’ ambaye sasa ni Mbunge wa Nyali, Kaunti ya Mombasa. Kutoka utotoni, Meja alipenda masuala ya kijasusi na ndoto yake ilikuwa kuwa kachero.

Ilhamu yake katika uanahabari ilichangiwa pia na vipindi vya Kiswahili kama vile Ramani ya Kiswahili (KBC) iliyokuwa Bahari ya Lugha (Radio Citizen) na Nuru ya Lugha kinachoendeshwa na Ali Hassan Kauleni wa Radio Maisha.

Kariha zaidi ilikuwa zao la kuhimizwa na mwanahabari Mugendi Mutegi alipokuwa Radio Fahari (Nakuru) akiendesha kipindi cha ‘Upeo wa Lugha’. Meja alianza kushirikishwa kama mchambuzi na mchanganuzi wa masuala ya Kiswahili kabla ya kupewa fursa ya kuwa mwelekezi mwenza wa kipindi akiwa msaidizi wa Mugendi.

Nafasi hii ilimtia ari ya kujiunga na Chuo cha East Africa Institute of Certified Studies (ICS) alikofuzu na stashahada ya uanahabari mnamo 2018.

Haja ya kujiendeleza zaidi katika taaluma hii ilimfanya kujiunga na Chuo Kikuu cha Multimedia anakosomea shahada ya uanahabari kwa sasa.

Meja pia ameanzisha kampuni ya masuala ya Habari na Mawasiliano ya Simba Media Services ambayo analenga kuisajili rasmi mwakani.

Akishirikiana na Mugendi Mutegi, wamezindua huduma za matangazo ya biashara na habari, uuzaji na ununuzi wa vitabu na huduma nyinginezo kupitia mtandao. Huduma ya Koupon City (KC) inawawezesha waandishi na watoaji huduma kama vile wanahabari na walimu kuuza na wanunuzi kununua bidhaa kwa bei nafuu na tena kwa starehe zao.

UANDISHI

Meja anashikilia kuwa uandishi ni talanta iliyoanza kujikuza ndani yake akiwa mwanafunzi wa darasa la sita. Huo ndio wakati alipoandika ‘mfano’ wa mswada wa riwaya aliouita ‘Raha Karaha’ japo hakuukamilisha hadi sasa. Insha nzuri alizoziandika na kumzolea tuzo za haiba wakati huo ni ushahidi wa utajiri wa kipaji chake katika uandishi.

Hamu ya kuandika ilimkaba koo zaidi kutokana na mapenzi yake ya kusoma kazi bunilizi za waandishi Prof Said A. Mohamed, Dkt Robert Oduori, Prof K.W. Wamitila, marehemu Prof Ken Walibora, marehemu Prof Euphrase Kezilahabi na marehemu Prof Katama G.C. Mkangi.

Waandishi wengine waliomtia Bukachi hamu ya kutunga ni Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Geoffrey Mung’ou na Dkt Hamisi Babusa.

Kampuni ya Uchapishaji wa Vitabu ya Maxwel Publishers Limited ilimchapishia Meja ‘Uketo wa Fasihi’ toleo la kwanza mnamo 2017, mwaka mmoja kabla ya Smart Publishers kumfyatulia ‘Mwongozo wa Kigogo’ na ‘Mwongozo wa Tumbo Lisiloshiba’ mnamo 2018.

Mnamo 2019, Maxwel Publishers Limited ilimtolea Bukachi ‘Mwongozo wa Chozi la Heri’ kabla ya Bestar Publishers kuzamia uchapishaji wa msuru wa ‘Uketo wa Sarufi’, ‘Uketo wa Fasihi’, ‘Uketo wa Ushairi’, ‘Uketo wa Fasihi Simulizi’, ‘Uketo wa Insha, Ufahamu, Ufupisho na Isimujamii’.

Meja pia ameandika kazi za kibunifu zikiwemo riwaya ya ‘Hawakuziki Mama’ (2019) na ‘Mola Mkuu’ (2020) ambazo zimechapishwa na Bestar Publishers. Miswada miwili ‘Ameavya Tena’ (riwaya) na ‘Pepo Tusitusi’ (tamthilia) inashughulikiwa na Gateway Publishers Limited na African Ink Publishers mtawalia.

Meja ameshirikiana na John Wanyonyi Wanyama kuhariri antholojia ya hadithi fupi ya ‘Wingu Limetanda na Hadithi Nyingine’ iliyochangiwa na wanachama wa CHAKINA na kuchapishwa na Bestar Publishers mnamo Machi 2020.

Ameshirikiana pia na Mugendi Mutegi kuandika diwani mbili za ushairi – ‘Diwani ya Kupe’ na ‘Uketo wa Ushairi’.

JIVUNIO

Anapojitahidi kufikia upeo wa malengo yake, Meja anaazimia kutumia kampuni ya Simba Media Services na mtandao wa Koupon City kupigia chapuo Kiswahili na kuwasaidia vijana.

Anajivunia kufundisha vijana wengi ambao wamezamia uanahabari na taaluma nyinginezo katika sekta mbalimbali za maendeleo ya jamii. Meja anajivunia kuwa kielelezo kwa vijana wanaotambua kuwa kutenda jambo hakutegemei umri.

You can share this post!

Ibrahimovic afunga mawili na kusaidia AC Milan kuzamisha...

KINA CHA FIKIRA: Ni busara kufikiri kabla ya kusema, maneno...