Makala

GWIJI WA WIKI: Michael Kipkirui Ng’etich

October 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

KUFAHAMU jinsi ya kusubiri ni miongoni mwa siri kubwa za kufanikiwa.

Haiwezekani kabisa mambo yote yaje kwa wakati mmoja.

Jifunze kuwa na uvumilivu na uwe radhi kuyaruhusu mawazo yako kutawaliwa na nidhamu. Ukweli na ujasiri ni nguzo muhimu maishani. Usiruhusu mawazo yoyote yasiyo na sifa hizi akilini mwako.

Jifunze kutokata tamaa, kuwa mtu mwenye msimamo kisha penda kuenda na wakati.

Kufaulu katika jambo lolote ni zao la jitihada, nidhamu na stahamala.

Thamini kile unachokifanya huku ukijitahidi kuwa mbunifu na kuwauliza wajuao zaidi yako. Jitolee kuongozwa na mapenzi ya dhati katika chochote unachokitenda huku ukipania kujiimarisha kwa kujiwekea malengo mapya ya mara kwa mara.

Huu ndio ushauri wa Bw Michael Kipkirui Ng’etich ambaye ni mwalimu wa Kiswahili.

Kwa sasa ni Naibu Mwalimu Mkuu katika Shule ya Msingi ya ACK Holy Trinity, Kericho.

Maisha ya awali

Ng’etich alizaliwa mnamo 1984 katika kijiji cha Cheptenye, eneo la Kaptoboiti, Belgut, Kaunti ya Kericho akiwa mwanambee katika familia ya watoto saba wa Bi Mary Chelang’at na Bw James Mutai. Alipata elimu ya awali katika Shule ya Msingi ya Cheptenye alikofanyia mtihani wa KCPE mnamo 1998 kisha kujiunga na Shule ya Upili ya Getumbe, Belgut mwanzoni mwa 1999. Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) shuleni humo mwishoni mwa 2002.

Anaungama kuwa aliyemchochea na kumshajiisha zaidi kutia bidii masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni aliyekuwa Mwalimu Mkuu katika Shule ya Cheptenye, Bw Samuel Koskei ambaye kwa sasa amestaafu. Ng’etich anatambua pia ukubwa na upekee wa mchango wa Bw Koskei katika kumwelekeza vilivyo na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Ni wakati akiwa mwanafunzi wa Darasa la Sita ambapo Ng’etich aligundua utajiri wa kipaji chake katika utangazaji wa kabumbu, mchezo uliomvutia tangu utotoni kiasi kwamba alijipata akiziiga sauti za Jack Oyoo Sylvester, Peter Kimeu na Ali Salim Mmanga kila walipokuwa wakitangaza mpira redioni.

Alivutiwa pia na weledi wa Billy Omala, mwanahabari ambaye katika uhai wake, alimfundisha mambo mengi kupitia kipindi Maswali kwa Wanafunzi alichokuwa akikiendesha katika Idhaa ya KBC. Mbali na Leonard Mambo Mbotela, mwingine aliyemtandikia Ng’etich zulia zuri katika jitihada za kukichapukia Kiswahili ni aliyekuwa mwalimu wake katika shule ya upili, Bw Martine Wangila.

Mtihani mgumu zaidi aliokabiliana nao baada ya kukamilisha KCSE ni vita vya ndani ya nafsi vilivyompa msukumo wa kutaka kujitosa kikamilifu katika ulingo wa Kiswahili na kuwa ama mwanahabari maarufu kufu ya Charles Hillary Martin wa Tanzania au mwalimu na mwandishi mashuhuri mfano wa Doyen wa Kiswahili Afrika Mashariki, Guru Ustadh Wallah Bin Wallah.

Uanahabari na ualimu ni taaluma ambazo Ng’etich alivutiwa nazo tangu akiwa mwanafunzi wa Darasa la Tano shuleni Cheptenye.

Ilikuwa hadi Agosti 2011 ambapo Ng’etich alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi kusomea ualimu (Kiswahili na Jiografia). Msukumo wa kutaka kujiendeleza kitaaluma ulichangia pakubwa uamuzi wake huo.

Anakiri kwamba kariha na ilhamu ya kuzamia utetezi wa Kiswahili akiwa chuoni ni zao la kutangamana kwa karibu sana na wahadhiri wake, hasa Bi Sawe aliyemtanguliza vyema zaidi katika taaluma ya Lugha na Isimu.

Mbali na kupanda kisha kuotesha mbegu za mapenzi ya dhati kwa Kiswahili ndani ya Ng’etich, Bi Sawe alimpokeza mwanafunzi wake huyo malezi bora ya kiakademia.

Mwingine aliyemchochea Ng’etich pakubwa kwa imani kwamba Kiswahili kina uwezo wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hiyo ni kiwanda kikubwa cha maarifa, ajira na uvumbuzi ni somo wake, Bw Ng’etich, aliyemfundisha katika Chuo Kikuu cha Moi, Bewa la Kericho. Ng’etich alihitimu na kufuzu chuoni mnamo Septemba 2016.

Ualimu

Ng’etich alijitosa katika ulingo wa ualimu pindi alipohitimisha masomo yake ya sekondari. Alifundisha katika Shule ya Msingi ya Cheptenye kwa kipindi kifupi katika mwaka wa 2003 kabla ya kujiunga na Chuo cha Walimu cha Bondo, Kaunti ya Siaya mnamo 2004.

Alifuzu mwishoni mwa Julai 2006 na kupata ajira katika Shule ya Msingi ya AGC Sosiot, Belgut miezi miwili baadaye. Alihudumu huko kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kujiunga na Shule ya Msingi ya ACK Holy Trinity Academy, Kericho mnamo Septemba 19, 2007.

Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili shuleni na kuamsha ari ya kuthaminiwa pakubwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake. Miaka miwili baadaye, Ng’etich alihamia katika Shule ya Msingi ya Chumo Educational Centre, Belgut.

Alifundisha huko kuanzia Septemba 2009 hadi mwishoni mwa Aprili 2010. Ilikuwa hadi Mei 1, 2010 ambapo vinara wa ACK Holy Trinity Academy waliyahemea upya maarifa yake. Alijiunga nao na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili kisha kupandishwa cheo kuwa Naibu Mwalimu Mkuu wa shule hiyo mnamo Januari 2018.

Ng’etich anakiri kwamba kufaulu kwa mwanafunzi yeyote hutegemea mtazamo wake kwa somo hilo na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani. Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni ACK Holy Trinity ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaojivunia kila mwaka matokeo ya KCPE yanapotolewa.

Uandishi

Ng’etich anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza rasmi tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Mbali na utunzi wake kumpandisha katika majukwaa mbalimbali ya makuzi ya Kiswahili, nyingi za insha bora alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kubwa na za kutamanisha mno.

Msukumo wa kutaka ujuzi alionao katika uandishi na ufundishaji wa Kiswahili uwafaidi pia wanafunzi na walimu wengine ni kiini cha Ng’etich kushiriki kikamilifu uendeshaji wa kipindi Lugha Yetu katika Idhaa ya Radio Injili, Kericho.

Yeye hufundisha Kiswahili redioni kila Jumapili kuanzia saa saba na nusu hadi saa nane mchana.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai ndoto za kuwa profesa na mhadhiri wa Kiswahili katika chuo kikuu, Ng’etich anajivunia kuandaa na kuhudhuria makongamano mengi katika sehemu mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili.

Tangu 2014, Ng’etich amekuwa mtahini wa kitaifa na uzoefu alionao umemwezesha kuzuru shule mbalimbali ili kuwashauri na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu ibuka na mwafaka zaidi katika kujiandaa kwa mitihani ya KCPE.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, Ng’etich amelivalia njuga suala la ufugaji na ukuzaji wa majani-chai katika Kaunti ya Kericho.

Anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalim- bali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Miongoni mwao ni kakaye Japhet wa Shirika la Maziwa la Kenya (KCC), Noah Randiek anayesomea uanasheria na Lilian Chepkirui ambaye ni mwuguzi katika zahanati ya Cheptenye. Kwa pamoja na mkewe Bi Sally Chepkirui ambaye pia ni mwalimu, wamejaliwa mtoto mmoja; Blessing Chepkoech.