GWIJI WA WIKI: Mtetezi wa Kiswahili ndani ya Seneti
LEONARD ONYANGO na CHRIS ADUNGO
KITI cha Naibu wa Spika wa Seneti kiliposalia wazi baada ya Seneta wa Tharaka Nithi Profesa Kithure Kindiki kubanduliwa Mei 22, mwaka huu, Seneta Maalumu Isaac Mwaura alikuwa miongoni mwa maseneta waliotuma maombi ya kutaka wadhifa huo.
Wengine walioidhinishwa kuwania wadhifa huo ni Seneta wa Kirinyaga Bw Charles Kibiru, Prof Margaret Kamar (Uasin Gishu), Bw Stewart Madzayo (Kilifi) na Bi Judith Pareno (Maalumu).
Lakini siku chache baadaye, Bw Mwaura, Bw Kibiru, Bw Madzayo na Bi Pareno walijiondoa kutoka kwenye kinyang’anyiro baada ya kufanya mashauriano, hivyo kumwezesha Prof Kamar kuchaguliwa bila kupingwa.
Kuchaguliwa kwa Prof Kamar, hata hivyo, ilikuwa baraka kwa Seneta Mwaura.
“Kamar alikuwa katika jopo la wasaidizi wa spika. Alipochaguliwa kuwa naibu wa spika, kulitokea nafasi katika jopo hilo. Mnamo Juni 24, mwaka huu, nilichaguliwa kujaza nafasi hiyo,” anaelezea.
Jopo hilo la watu sita, hujumuisha spika, naibu spika na wasaidizi wanne ambao wanaweza kuongoza vikao vya Seneti.
Wasaidizi hao wanne wanaweza kuendesha vikao spika na naibu wake wasipokuwepo.
Bw Mwaura ambaye ni msaidizi wa spika mwenye umri mdogo zaidi, anasema kuwa wadhifa huo umetimiza ndoto aliyokuwa nayo kabla ya kuingia bungeni 2013 kwamba siku moja angeongoza vikao vya bunge.
“Nilitamani kuwa spika wa Bunge hata kabla ya kuingia bungeni 2013. Ninashukuru sana kwa sababu hiyo ni ndoto ambayo imeafikiwa,” anasema.
Kati ya wasaidizi hao wanne wa spika, Bw Mwaura amekuwa kivutio cha wengi kutokana na hatua yake ya kuendesha vikao vya Seneti kwa kutumia Kiswahili.
“Nilipoanza kutekeleza majukumu yangu kama msaidizi wa spika sikuanza kwa lugha ya Kiswahili. Lakini baadaye nilitafakari kwa kina nikaamua nitumie lugha ya Kiswahili katika vikao vyangu.
“Lakini jambo la kutia moyo ni kwamba Wakenya wamependezwa sana na hatua yangu ya kutumia Kiswahili kuongoza vikao vya Seneti. Nimekuwa nikipokea arafa tele za kunimiminia sifa,” anasema Bw Mwaura.
Seneta Mwaura ndiye alikuwa akiongoza kikao cha Seneti wakati wa kupitisha Mswada wa Ugavi wa Fedha kwa Kaunti (CARB) 2020 mnamo Octoba 6 hivyo kuingia katika daftari la kumbukumbu kwa kuwa spika wa kwanza kutumia Kiswahili kupitisha sheria.
“Hata Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi alinieleza kuwa alipendezwa sana na hatua yangu kupitisha sheria kutumia lugha ya Kiswahili. Hakuna spika ambaye amewahi kutumia Kiswahili nchini Kenya na kuendesha vikao vya Bunge na hatimaye kupitisha sheria.
“Maseneta wanashangaa kwa sababu ninapewa ratiba ya shughuli za Seneti za siku zikiwa zimeandikwa kwa Kiingereza lakini mimi nazitafsiri kwa Kiswahili wakati wa kuzungumza,” anasema.
Tofauti na Bunge la Kitaifa ambalo kanuni zake zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili, kanuni za Seneti hazijatafsiriwa. Lakini kuna jopokazi linaloendelea na shughuli ya kutafsiri kanuni za Seneti kwa lugha ya Kiswahili.
Seneta Mwaura, hata hivyo, anasema kuwa ni wabunge wachache mno wanaotumia Kiswahili wakati wa mijadala licha ya kanuni za Bunge la Kitaifa kutafsiriwa kwa Kiswahili.
HOFU YA KUZUNGUMZA KISWAHILI BUNGENI
Bw Mwaura anasema kuwa maseneta wengi wanasema kuwa hawazungumzi Kiswahili kwa sababu wanaogopa kuboronga lugha.
“Wanahisi kuwa hawataweza kuzungumza kwa ufasaha. Lakini jambo la kushangaza mbona wanatumia Kiswahili kuomba kura kutoka kwa Wakenya wakati wa uchaguzi na hawaoni haya?” anauliza.
Seneta Mwaura ambaye ni mtu wa kwanza mwenye ulemavu kuhudumu katika jopo la maspika, anasema kuwa pongezi ambazo amekuwa akipata zimemtia mshawasha wa kuendelea kutumia Kiswahili kuongoza vikao.
“Tangu nilipoanza kutumia Kiswahili kuongoza vikao Wakenya wamekuwa wakiniambia kuwa sasa wanafuatilia matukio katika Seneti kwa sababu wanaelewa kinachoendelea ndani ya Bunge,” anasema.
ELIMU
Anasema kuwa aliipenda lugha ya Kiswahili alipokuwa kinda katika Shule ya Msingi ya Wasioona ya Thika. Mnamo 1996, Mwaura alitunukiwa tuzo kwa kuwa msemaji bora wa hotuba ya Kiswahili nchini katika mashindano ya wanafunzi wa shule ya msingi.
“Nilifana kuanzia kanda hadi ngazi ya kitaifa na nilitunukiwa cheti katika jumba la KICC na aliyekuwa waziri wa Elimu JJ Kamotho. Wakati huo nilikuwa mwanafunzi wa Darasa la Nane,” anaeleza.
Baada ya kukamilisha elimu ya shule ya msingi, Mwaura alifaa kujiunga na Shule ya Upili ya Starehe lakini akanyimwa nafasi kwa kuwa mlemavu.
Baada ya kukamilisha masomo yake ya shule ya sekondari, Bw Mwaura alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea Elimu ya Watu wenye Mahitaji Maalumu na Kifaransa ambapo alihitimu 2006.
Alipokuwa mwanafunzi aliongoza maandamano dhidi ya shirika lisilokuwa la kiserikali lililokuwa likitumia wanafunzi wasioona kujinufaisha.
Mnamo 2006, aliunda chama cha kutetea masilahi ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Mwaka huo alikutana na mwigizaji mahiri Lupita Nyong’o katika Jumba la Maonyesho ya Sanaa (KNT) alipokuwa akijiandaa kutengeneza filamu yake iliyofahamika kama My Genes.
“Niliomba Bi Nyong’o kunitambulisha kwa baba yake Prof Anyang’ Nyong’o aliyekuwa Katibu Mkuu wa ODM. Baadaye Prof alikuwa mlezi wa Chama cha Watu wenye Ulemavu wa Ngozi (ASK),” anasema.
Mwaura alihudumu kama mshauri wa Waziri Mkuu Raila Odinga kati ya 2010 na 2012. Alimshauri Bw Odinga kuhusu sera zinazohusiana na watu wenye ulemavu.
Mnamo 2013, aliteuliwa kuwa mbunge maalumu aliyewakilisha walemavu.
Bw Mwaura pia alisomea katika Chuo Kikuu cha Leeds cha Uingereza kati ya 2011 na 2012, Chuo Kikuu cha Nelson Mandela Metropolitan (2010 -2012) na Chuo Kikuu cha Presbyterian East Africa (2003-2012).
MATAZAMIO
Bw Mwaura anahimiza Wakenya, haswa viongozi kukumbatia Kiswahili kwa sababu mawanda yake yanazidi kuenea kote barani Afrika.
“Kiswahili kinazidi kukua barani Afrika. Kiswahili sasa kinafundishwa mataifa mbalimbali barani Afrika kama vile; Afrika Kusini, Rwanda, Burundi, Namibia na Dr Congo,” anasema.
Anasema kuwa Kiswahili kinafaa kuzungumzwa na wabunge wote bila kujali maeneo wanayotoka.
“Kwa mfano, katika Seneta wa Laikipia John Nderitu Kinyua hutumia lugha ya Kiswahili kwa ufasaha sana pale katika Seneti. Lugha ya Kiswahili hakifai kuwa tu ya wabunge na maseneta kutoka Pwani. Kiswahili kinastahili kuenziwa na kila seneta au mbunge,” anasema.
“ Ninashangazwa kwamba hakujawahi kutokea spika ambaye amewahi kukumbatia Kiswahili bungeni. Hata Spika wa kwanza wa Seneti Timothy Chitasi Chokwe aliyehudumu kati ya 1963 na 1966, hakuwa akitumia Kiswahili kuendesha shughuli za Bunge licha ya kuwa mzaliwa wa maeneo ya Pwani,” anaongezea.
Anasema kuzungumza Kiswahili Bungeni ni ishara ya kuonyesha kuwa wabunge wanamjali mwananchi wa kawaida.
“Mara nyingi tunapozungumza Kiswahili watu huelewa zaidi. Hii ni kwa sababu idadi kubwa ya Wakenya wanaelewa Kiswahili ikilinganishwa na lugha ya Kiingereza.
Haja kubwa hapa si lafudhi au ufasaha bali na kujieleza. Hatufai kuendeleza kasumba ya wakoloni ambao walikichukulia Kiswahili kuwa lugha ya watu ambao hawajasoma na watumwa. Kiswahili ni lugha ya kila mtu; kuanzia wale hawakupata fursa ya kwenda shuleni hadi wale wamesoma hadi kiwango cha uzamifu (PhD),” anasema.
Anasema kuwa tangu alipoanza kuongoza vikao vye Seneti kwa lugha ya Kiswahili baadhi ya maseneta wamepata ujasiri wa kuwasilisha hoja kwa kutumia lugha hiyo ambayo inatumika humu nchini kama lugha rasmi na lugha ya kitaifa.
Anasema kuwa kanuni za sasa zinazotumika katika Seneti na Bunge la Kitaifa pia zinachangia katika kufanya wabunge kutozungumza Kiswahili.
“Tunafaa kubadilisha kanuni za Bunge ili kuruhusu maseneta kuchanganya Kiswahili na Kingereza wakati wa kutoa hoja bungeni. Kwa sasa kanuni za Bunge zinasema kuwa unapoanza kuzungumza kwa Kiingereza ni sharti umalize hotuba kwa Kiingereza. Ukianza kwa Kiswahili unamalizia kwa Kiswahili – wengi hupendelea kuanza kwa Kiingereza,” anasema.
Bw Mwaura anasema kuwa ili kuwatia mshawasha wa kuzungumza Kiswahili maseneta wenzake: “Ninapokuwa kwenye kiti cha Spika maseneta wanapozungumza kwa Kiingereza mimi nawajibu kwa Kiswahili.”
Anasema kuwa viongozi wakuu serikalini wanafaa kukumbatia Kiswahili.
“Rais Uhuru Kenyatta, kwa mfano, anasoma hotuba yake ya Kiingereza na kisha mwishoni anafafanua mambo aliyoyasoma kwa Kiswahili. Huko ni kudunisha Kiswahili.
“ Natamani siku ambayo Rais Kenyatta atasoma hotuba yake rasmi kwa Kiswahili bila kuchanganya na Kiingereza. Huo si uzalendo tu bali itawafikia Wakenya wengi,” anasema.