GWIJI WA WIKI: Mufti Mutahi
Na CHRIS ADUNGO
NJIA ya siku nyingi haina alama.
Maisha ni ghali. Ukitaka kuishi kubali gharama.
Binadamu kapewa hekima, busara na Mwenyezi Mungu ili atumie kipawa hicho kubadili dunia anamoishi na kujenga usuhuba wa kudumu kati yake na wanadamu wenzake.
Changamoto za maisha ndizo rutuba aali za mafanikio ya kesho. Binadamu hustaarabika na kustawi zaidi kimawazo iwapo wafuasi wake wanafanikiwa pia.
Utafiti umeniwezesha kutambua kwamba kufanikiwa kwa mwanafunzi kielimu aghalabu hakutokani na mazingira au usuli wake tu, bali pia mbinu zinazotumiwa katika kumpokeza maarifa ya ujuzi autakao. Hili huwezekana tu iwapo tutatembea na majira na kusonga mbele kwa lengo la kushindana na wakati.
Huu ndio ushauri wa Bw Mufti Mutahi – mwandishi mahiri na mshairi shupavu ambaye kwa sasa ni mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya Tenwek, Kaunti ya Bomet.
Maisha ya awali
Mwalimu Mufti Mutahi alizaliwa mnamo Juni 25, 1983, katika kijiji cha Bing’wa, eneo la Siongiroi, Kaunti ya Bomet akiwa mtoto wa tano katika familia ya watoto tisa wa Mzee Champion Sang na Bi Rebecca Sang.
Alisomea katika Shule ya Msingi ya Bing’wa kwa muda mfupi mnamo 1987, kisha akahamia eneo la Sotik na kujiunga na darasa la kwanza katika Shule ya Msingi ya Kisabei mnamo 1988.
Alisomea huko hadi mwishoni mwa 1995 alipoufanya mtihani wa KCPE. Alama nzuri alizozipata zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya Litein, Kaunti ya Kericho mnamo 1996.
Hata hivyo, kutokana na uchechefu wa karo, alilazimika kutupilia mbali masomo baada ya mwaka mmoja tu na kujipata sokoni akichuuza nguo za mitumba kati ya 1997-1998.
Ndoto yake ya kuendelea na elimu ingekatika kabisa isingekuwa kwa juhudi za kakaye, Bw Paul Mutahi aliyemsihi kujiunga na shule ya kutwa ambako karo ilikuwa nafuu kidogo kwa familia yao kumudu. Baada ya muda, alikubali shingo upande wito huo na kusema na liwe liwalo.
Mtihani mkubwa zaidi katika maisha yake ulikuwa ni kufanya uamuzi wa kujiunga na shule changa ya Kapoleseroi iliyokuwa katika mapito mazito wakati huo kutokana na matokeo duni katika mitihani ya kitaifa mbali na kuzongwa na changamoto za ukosefu wa walimu na vifaa muhimu vya kufanikisha masomo mengi. Idadi ya wanafunzi wakati huo katika shule ya Kapoleseroi ilikuwa chini ya 60.
Mufti alipata afueni baada ya aliyekuwa Mwalimu Mkuu Bw Mbivii na naibu wake Bw Simeon Maritim kukubali ombi lake la kuvalia sare zake za shule ya awali na pia kuzikubali mboga za mamaye kuwa sehemu ya karo yake.
Ili kukata gharama na kupunguza zaidi mzigo wa karo, ilimlazimu Mufti kujiunga na Kidato cha Tatu moja kwa moja bila ya kusomea katika Kidato cha Pili kwani mwaka mmoja tayari ulikuwa umepita akiwa mchuuzi wa nguo sokoni.
Baada ya miaka mitatu katika shule ya upili, alifanya mtihani wa KCSE na hata kabla ya matokeo ya mtihani wenyewe kutolewa, akawa tayari amepata kibarua cha kufundisha Kiswahili katika shule ya kibinafsi ya Mara Siongiroi, eneo la Chepalungu, Kaunti ya Bomet.
Matokeo ya KCSE yalipotangazwa, Mufti hakufaulu kujiunga na chuo kikuu moja kwa moja. Ilimjuzu kuendelea kuzumbua riziki kwa kufundisha katika shule mbalimbali angalau apate hela za kumwezesha kujiendeleza kimasomo. Hatimaye, milango ya heri ilijifungua mnamo 2011 na akajiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta kusomea taaluma ya ualimu (Kiswahili na Historia) baada ya miaka 10 ya mahangaiko.
Mufti anawaenzi mno wahadhiri waliofanikisha safari yake ya elimu chuoni, hasa Dkt Jacktone Onyango na Dkt Joseph Kariuki Gakuo ambao waliyanoa makali yake vilivyo na kumrithisha ilhamu na kariha ya kukichangamkia Kiswahili.
Ualimu
Mnamo 2013, akiwa bado mwanafunzi chuoni, Mufti alijiunga na Shule ya Upili ya Kimulot, Kaunti ya Bomet kuwanoa wanafunzi ambao tayari walikuwa wametamauka katika somo la Kiswahili.
Baada ya mwaka mmoja, somo la Kiswahili liliwashangaza wengi kwa kuwa ambalo lilitoa mleli na kutia fora zaidi baada ya wanafunzi 48 wa Kimulot kupata gredi ya A matokeo ya KCSE yalipotolewa. Somo la Kiswahili likawa ndilo lililofanywa vyema zaidi kiasi cha kumwezesha Mufti kutawazwa Mwalimu Bora wa Mwaka katika Kaunti ya Bomet akishirikiana na Bw Masinde Conrad (St Peter’s Mumias).
Awali, alikuwa amefundisha katika shule za Kaboson Girls, Mara, Chumo (Kericho), Milimani miongoni mwa nyinginezo nyingi. Akiwa Kimulot, alifanikiwa kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili na akawachochea wengi wa wanafunzi wake kuanza kupenda masomo ya Lugha.
Aidha, aliandaa makongamano mengi na kushiriki mashindano mbalimbali ya tamasha za muziki hadi kiwango cha kitaifa. Aliteuliwa kuwa Mlezi wa Chama cha Kiswahili na mkuu wa kutathmini ubora wa masomo shuleni (DQASO) kushikilia nafasi ya mwalimu Gilbert Bor aliyeteuliwa kuwa Naibu Mwalimu Mkuu wa Kimulot.
Tangu 2015, Mufti amekuwa mtahini wa kitaifa na mhakiki wa karatasi za mitihani.
Uzoefu huu umemwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kuinua kiwango cha Kiswahili kwa kuwashauri na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu ibuka na mwafaka zaidi katika kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.
Kwa ushirikiano na walimu watajika na wapenzi wa Kiswahili, Mufti amezindua majopo mawili ya Kiswahili mtandaoni. Kumbi hizi huwaleta pamoja maelfu ya walimu wa Kiswahili kutoka zaidi ya shule 500 nchini Kenya.
Uandishi
Uandishi ni sanaa ambayo Mufti alianza kuizamia akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi. Mwalimu wake wa Kiswahili, mwendazake Samwel Gwaro, ndiye aliyemtilia pondo kwa kusoma Insha zake kila wakati mbele ya wanafunzi wengine darasani. Anamvulia nduguye Paul kofia kwa kumhimiza kila wakati kusoma riwaya mbalimbali za Sheikh Shabaan Bin Robert na pia kumnunulia magazeti ya Taifa Leo mara kwa mara. Akiwa mwanafunzi wa shule ya upili, Mufti alijikakamua kutunga mashairi aali baada ya kipawa chake kutambuliwa na Bw Robinson Langat (Mwalimu Mkuu Kamungei).
Kufikia 2006, tayari alikuwa ameandika mswada wake wa kwanza wa kitabu ‘Matumizi ya Lugha na Istilahi za Kifasihi’. Lakini kwa sababu wakati mwingine kanga wa mkata hatagi na akitaga haangui, mswada huo uliangukia mikononi mwa matapeli na ukatoka kwa jina la mtu mwingine. Juhudi zake za kufuatilia na kutafuta haki ziligonga mwamba kutokana na unyonge aliolazimishiwa na uhaba wa mali. Alilazimika kumeza shubiri na kumshtakia Mola kwani fimbo ya mnyonge mlifi ni Mungu!
Baada ya kushauriana pakubwa na Bw Simon Mutali Chesebe (Mwalimu Mkuu, Tenwek High) na Guru Ustadh Wallah Bin Wallah, Mwalimu Mufti alianzisha
kampuni yake ya Muficom Educational Movers & Publishers mnamo 2017.
Kampuni hii imemfaa pakubwa katika kuratibu maandalizi ya makongamano na uandishi wa vitabu na makala mbalimbali ya kitaaluma. Mufti alishirikiana na Mwalimu Brian (Shule ya Upili Chikamba, Nakuru) kuandaa kitabu ‘Nyota ya Sarufi’ kabla ya kuzindua kitabu kingine, ‘Utamu wa A’ mnamo 2018. Kwa sasa anakamilisha maandalizi ya miswada ya vitabu ‘Nyota ya Fasihi Simulizi’, ‘Msingi wa Isimujamii’ na ‘Insha Kufu’. Anashirikiana pia na malenga Mstahiki Dennis Osano almaarufu Nyani wa Jangwani kuandaa diwani ‘Mashairi Teule’ itakayofyatuliwa wakati wowote mwaka huu.
Jivunio
Mufti anatambua ukubwa na upekee wa mchango wa malkia mchumba wake Bi Edinah Mutahi ambaye daima humpa moyo na ari ya kuzidi kukwea ngazi za kitaaluma na kufikia upeo au kilele cha ufanisi.
Anajivunia kufunza idadi kubwa ya wataalamu wa Kiswahili na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali humu nchini.
Baadhi yao ni Victor Mutai na Nathan Rotich waliosomea taaluma ya uhandisi katika Vyuo Vikuu vya Havard na Yale nchini Amerika. Kwa pamoja na mkewe, Mwalimu Mufti amejaliwa watoto watatu: Brian Junior, Gideon na Caleb.