Makala

GWIJI WA WIKI: Richard Amunga

March 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

TUKILIA kwamba hatuna viatu, tukumbuke kuwa kuna watu wengi wasio na miguu.

Usiwe mwepesi wa kulalamika kila uchao bila ya kuchunguza kiini cha mambo. Shukuru sana katika kila hali na umtumanie Mwenyezi Mungu katika mambo yote.

Upo jinsi ulivyo leo kwa sababu wewe mwenyewe uliamini kwamba utakuwa hivyo tangu jana. Vyovyote vile uwavyo, jinsi utakavyokuwa kesho ni matokeo ya jinsi unavyoamini leo kuhusu hiyo kesho yako.

Katika maisha, usiogope kuamini ukubwa wa imani yako. Mwamini sana Mungu wako kwa kuwa ndiye atakupa mbinu zote mwafaka za kukabiliana na changamoto za kila sampuli.

Bidii, imani, nidhamu, stahamala na ujasiri ni nguzo za mafanikio katika taaluma yoyote. Usiruhusu mawazo yasiyo na sifa hizi akilini mwako. Jifunze kutokata tamaa, kuwa mtu mwenye msimamo na upende kushindana na wakati.

Upendo wa Mungu kwetu sisi binadamu hauwezi kumithilishwi na ule wa kiumbe kingine chochote. Kutokana na upendo huu, masaibu yanayotukia katika sayari hii ya tatu hayafai kutuvunja moyo maadamu ni njia mojawapo ya kujikuza kutoka hatua moja hadi nyingine.

Ni nani asiyejua kuwa katika kufanya jambo na kufeli mara moja au kadhaa ni fursa ya kupata mwanga wa kujua jinsi ya kutenda jambo hilo vyema hata zaidi?

Mshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa neema ya afya aliyokujalia. Mshukuru kila siku kwa uzima na uhai na umwombe akupe nguvu zaidi ya kumtumikia. Mola akikutunukia yote haya, pania mno kutumia kila fursa uipatayo kufanya mambo yatakayomfurahisha na kuridhisha nafsi za binadamu wenzako.

Huu ndio ushauri wa Bw Richard Amunga; mwandishi chipukizi na mwalimu wa Kiswahili katika Shule ya Upili ya St Teresa Mukunga, Kaunti ya Kakamega.

Maisha ya awali

Amunga Ondoli alizaliwa mnamo Mei 17, 1994 katika kijiji cha Isanda, Kaunti ya Vihiga akiwa mtoto wa pili katika familia ya watoto sita.

Mwaka mmoja baada ya kukopolewa kwake, alianza kuishi na nyanyaye katika eneo la Kilingili baada ya ugomvi wa mara kwa mara kuwa kiini cha kutengana kwa wazazi wake.

Babaye (Dickson Amunga) na mamaye (Mary Khang’atsi) walikatiza uhusiano mwaka mmoja baada ya kuzaliwa kwa mwa mwana wao huyu. Amunga hakuonana na babaye mzazi hadi alipohitimu umri wa miaka minane alipopelekwa nyumbani kwao na nyanyaye (mama mzaa mama) kwa minajili ya makumbusho ya marehemu nyanyaye (mama mzaa baba).

Tangu siku hiyo, Amunga ameishi na babaye ambaye alilibadilisha jina lake kuwa Richard Ondoli Amunga. Awali, akiwa kwa nyanyaye, aliitwa Staus Amunga. Kubadilishwa kwa jina lake kulichochewa na tukio la kisadfa kwamba jina lake lilikuwa sawa na la nduguye mkubwa!

Amunga ana ndugu na dada kutoka pande zote mbili za familia yao; upande wa kwanza ukiwa ni ule wa mama mzazi. Baada ya kutengana na Bw Dickson, Bi Khang’atsi alijaliwa kupata watoto wanne zaidi: Gloria, Elizabeth, Msimbi na Nepphy.

Katika upande wa pili (mama mlezi); nduguze Amunga ni Staus, James Musumba, Lydia Anyanzwa, Derick Sande na Carlos Williams Andabwa. Pamoja na hawa, ana binamu wafuatao kutoka upande wa mama mlezi: (Dorcas Opati, Dennis Opati na Maureen Riziki).

Elimu

Amunga alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya Isanda akiwa mwanafunzi wa darasa la kwanza. Wakati huo, alikuwa kitoto cha umri wa miaka tisa pekee. Hakuwahi kuhudhuria madarasa ya chekechea.

Baada ya kuhitimu masomo ya darasa la kwanza mnamo 2004, alipelekwa na babaye hadi eneo la Muhoroni alikojiunga na Shule ya Msingi ya Muhoroni Factory. Alisomea huko katika darasa la pili na la tatu pekee. Anakiri kwamba ari yake ya kukipenda Kiswahili ilianzia huko chini ya ulezi wa marehemu Bi Otieno aliyechangia asilimia kubwa ya alama 98 alizojizolea katika mtihani wake wa kwanza akiwa mwanafunzi wa darasa la pili shuleni Muhoroni Factory.

Amunga anaungama kuwa mamaye mlezi, Bi Tabitha Martha Semo, alikuwa akimhimiza sana katika njia mbalimbali. Alimpa hamasa ya kujitahidi masomoni, kumwelekeza vilivyo na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali. Alimsaidia Amunga kuondoa dhana potovu kwamba “mama kambo si mama”.

Amunga alitolewa katika Shule ya Msingi ya Muhoroni Factory na kupelekwa katika Shule ya Msingi ya Muhoroni Furaha mnamo 2007. Walimu kutoka shule yake ya awali walipandwa na mori maadamu hawakutaka mwanafunzi wao huyu atolewe mikononi mwao.

Akiwa katika darasa la nne, alibahatika kufunzwa na mikota ya lugha wa Kiswahili waliompokeza malezi bora zaidi ya kiakademia katika Shule ya Msingi ya Muhoroni Furaha. Baadhi yao ni Bw Paul Oluoch, Bw James Oware na Bw Douglas Maina ambao pia walitambua na kukipalilia kipaji chake cha utunzi wa kazi za kibunifu.

Zaidi ya kumpa msingi wa kujiboresha na kujikuza kisanaa, walimu hawa walimtia motisha ya kusomea taaluma za Kiswahili kwa undani zaidi katika siku za usoni. Kupitia kwao, aliweza kujua kuwa utamu wa lugha yoyote iwayo ile ni kujifunza msamiati mpya kila siku.

“Tungemsikia Bw Oluoch siku zote akituasa, akituhimiza na kutushauri kutolaza damu. Alitutaka sana tujifunze angalau neno jipya kila siku ili kuboresha viwango vyetu vya umilisi wa lugha.”

Amunga anatambua pia upekee na ukubwa wa mchango wa Bi Beatrice Onudi, Bw Ochieng Rogo, Bw Lang’at, Bw Owinyo, Bw Osundwa, Bw Michael Ochieng, Bi Sande Noel, Bw Ogal Dennish na Bi Hellen Onyancha katika safari yake ya elimu. Hawa walisisitiza yote yaliyokuwa yakisemwa na Bw Oluoch na wakamtia hamasa ya kujitahidi masomoni.

Mshawasha wa Amunga wa kutaka kuzamia sana utafiti wa Kiswahili ulimchochea Bi Onudi kumpagaza jina Profesa ambalo baadaye liliigwa na takriban walimu wote wa shule hiyo. Kubwa zaidi katika maazimio yake ya sasa ni kujituma kwa hali na mali ili kufikia upeo huo wa kitaaluma.

Baada ya kukamilisha mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) katika Shule ya Wavulana ya Kisumu Boys, Amunga alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi kusomea shahada ya ualimu katika masomo ya Kiswahili na Jiografia.

Uandishi

Amunga anaamini kwamba uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani yake akiwa na umri mdogo. Kazi nyingi za kibunifu alizoziandika zilimvunia tuzo za haiba kutoka kwa walimu wake.

Uwezo wa kuchora taswira mbalimbali za kuvutia kimaandishi ndio upekee wake. Anahisi kwamba hili ni jambo ambalo si kila mtunzi anaweza kufanikiwa kwalo. Isitoshe, anajivunia umilisi mkubwa wa msamiati katika Kiswahili. Kutokana na kipaji chake cha utunzi, ametuzwa vyeti mbalimbali katika shule ya msingi hadi chuo kikuu.

Zaidi ya kuwa profesa, mwandishi maarufu na mhadhiri wa Kiswahili, Amunga anaazimia kumiliki kampuni itakayowaajiri wapenzi na wakereketwa mbalimbali wa taaluma za Kiswahili.

Jivunio

Amunga alikuwa Mhariri Mkuu wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi (CHAKIMO) katika mwaka wa kiakademia 2017-18.

Akiwa mhariri, alifanikisha kuchapishwa kwa juzuu mbalimbali za majarida ya CHAKIMO – Dafina na Mshindo.

Amewahi pia kuwa Mwenyekiti wa CHAKIMO katika mwaka wa kiakademia wa 2018-19 na kuchangia uendeshaji wa vipindi vya Lugha, Isimu na Fasihi katika kituo cha MU FM cha Chuo Kikuu cha Moi.

Mbali na riwaya ‘Maisha Pilipili’, Amunga anajivunia kuandika na kuchapishiwa makala mengi ya kibunifu na kitaaluma.