Makala

GWIJI WA WIKI: Simiyu Mukuyuni

May 22nd, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

CHIPUKIZI tufanye subira! Usiwanie kisichokuwa chako kwa kuwa maisha ni safari ya kumba. Mafanikio hayashuki kwa mkesha mmoja. Kumbuka unapodhani umerauka, wapo waliokesha.

Andama mambo taratibu ili upate dira kamili ya kukulekeza kwa mema unayoyakusudia kupata. Usipende kushiriki msabaka wa mwenzio. Uliloandikiwa na Mola ndilo lako! Litatimia!

Chako ni chako ilimradi Mungu mtenzi amealifu. Nacho cha wenyewe hakiwezi kuwa chako hata upuruke angani ama utambae chini kama mtambaachi. Wania chako kihalali ili upate fursa ya kupima uwezo wako kinyang’anyironi.

Mara nyingi chipukizi hutamauka kwa sababu misabaka wanayoishiriki, uwezo wao haufikii matakwa ya msabaka wenyewe. Ikiwa unapania kufaulu, baini kuwa kuvua katika maji ya kina kirefu kwataka wavuvi stadi.

Usiige ili uwe kama mwafulani.

Kila ganda lina kiini chake. Uigaji hurovya asili ya mtu. Kiandame kilicho chako hata kama kinakutaabisha.

Kila uchao ni fursa adhimu ya kujifunza. Unapojifunza leo, mafunzo hayo ni nyongeza ya uliyojifunza jana. Mtu hawezi kabisa kusonga mbele kwa kuogopa kujifunza mambo mapya.

Usimtegemee binadamu hata kidogo.

Mtazamie sana Mungu wako ili akuvushe hadi ng’ambo ya pili ya mafanikio. Itakuwa desturi nzuri endapo utaratibu malengo yako ya mara kwa mara na kuandaa nyenzo za kuyafikia.

Chipukizi wanaotenzana nguvu na magwiji, wazee au watangulizi wao, wanastahili kuwa na busara na hekima tele.

Wasiwavue au wasivuane lebasi ya heshima kadamnasi.

Shingoni wafunge talasimu ya stara ili kumsitiri kila mmoja licha ya udhaifu mbalimbali utakaojitokeza katika malumbano.

Majisifu si sifa ya mtu muungwana. Ni nafuu sana kuwa mtu raufu badala ya mtu rafu. Tahadhari na majitapo. Majikwezo ni ngazi ya kumporomosha mtu katika shimo la ‘Ole Wangu! Kinyongo ni fundo la moyoni.

Huozesha nafsi ya mtu. Tuyafurahie mafanikio ya wenzetu. Kila mtu na fungu lake!

Huu ndio ushauri wa Bw Benard Simiyu Mukuyuni.

“Kutokana na changamoto hizi, nilihamia St Mary’s Nai Endebess. Shule hii pia ilikuwa ya mseto na kutwa. Ilikuwa nafuu kusomea hapa kwa sababu nisingesafiri kitalifa. Nilihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 2007. Japo nilipata alama ya wastani ya kujiunga na chuo kikuu, nilikosa ufadhili wa serikali na wavyele wangu hawakuwa na uwezo wa kumudu karo,” asema Mukuyuni.

Aongeza: “Alhamudulillahi! Nilijiunga na Chuo cha Walimu cha Bungoma mnamo 2008, ila maisha bado yalikuwa balaa! Kisa na sababu, karo! Nilikosa kuhudhuria vipindi vingi kwani tulikuwa tukiamrishwa kutopatikana darasani karibu kila juma. Masaibu haya yaliniandama kipindi kizima cha safari yangu ya masomo chuoni. Hata hivyo, nilifanikiwa kuhitimu mnamo Agosti 2008 Agosti.”

Ulianza kujishughulisha na nini baadaye?

Mwezi mmoja baada ya kufuzu, nilitua jijini Nairobi kwa ufadhili wa binamu zangu Kevin Sikolia na Catherine Sikolia waliokuwa wenyeji wangu. Kwa mwezi mmoja, nilitalii mitaa mingi ya Eastlands kusaka ajira. Baadhi ya mitaa hii ni Donholm, Umoja na Eastleigh.

Mnamo Oktoba, nilipata kazi Eastleigh nilikoanzia kutafutia tajriba ya ualimu. Baadaye 2009, nilihamia Shule ya St Juliet, Eastleigh iliyonipa fursa ya kutangamana na walimu bora shuleni humo na shule nyiginezo kama vile Makini na Riara.

Nilifundisha St Juliet kati ya 2011 na 2013. Mnamo 2014, nilifanikiwa kujiunga na Total Care Academy Pangani nilikofundisha kwa miaka miwili. Nilijiunga baadaye na Wamy Academy, Nairobi nilikohudumu kwa kipindi cha miaka miwili kabla ya kuajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC). Kwa sasa ninafundisha katika Shule ya Msingi ya Nauyapong Mixed Boarding, Pokot Magharibi.

Nani waliokuchochea zaidi kukipenda Kiswahili?

Hakika nguo haijui iwapo imetakata, ila mtakasaji! Katika shule ya msingi, walimu Bi Alice Busuru na Bi Truphena Mandela walipanda na kuotesha ndani yangu mbegu za kukichapukia Kiswahili.

Bw Noah Asachita aliyekirimiwa kipawa cha uigizaji, utunzi wa nyimbo na uchoraji alinihimiza pakubwa. Kariha, ilhamu na hamasa zaidi ilichangiwa na Eric Mukuyuni. Yeye ni mwalimu na binamu yangu mkubwa.

Katika shule ya upili, natambua upekee wa mchango wa Bi Sarah Munialo na Bi Rhoda kwa kunielekeza katika mkondo wa nidhamu kali na kunihimiza kujitahidi zaidi masomoni. Nikiwa chuoni, nilitagusana kwa karibu sana na marehemu Omar Babu Marjan, Job Mokaya, Tom Nyambeka, Mathias Momanyi, Geoffrey Mung’ou, Rachel Maina na Profesa Ken Walibora.

Upi mchango wako katika makuzi ya Kiswahili kitaaluma?

Nimewafundisha wanafunzi wengi wa ughaibuni kukipenda Kiswahili.

Nimehakikisha kuwa tunayaweka mambo sawa pindi waborongaji wanapovuruga lugha mitandaoni na katika majukwaa mengine.

Nimehakiki vitabu vya Kiswahili, kikiwamo ‘Manati ya Kiswahili’.

Nimekuwa miongoni mwa wanaleksikografia waliochangia maandalizi ya Kamusi Teule ya Kiswahili Toleo la 3. Nimeandika hadithi za Kiswahili kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Vitabu hivi ni ‘Busara na Hekima’, ‘Tesi na Ndege’ na ‘Tusome Msamiati’. Vyote vimeidhinishwa na Taasisi ya Ukuzaji Mitaala (KICD) na kuchapishwa na kampuni ya East African Educational Publishers (EAEP).
Zipo kazi nyinginezo zinazoshughulikiwa kwa sasa katika KICD, na zitafyatuliwa hivi karibuni Inshallah. Nimeshiriki midahalo mingi katika kuchangia uendeshaji wa vipindi vya Kiswahili katika vyombo vya habari kama vile Radio Citizen, KBC Idhaa ya Taifa, Radio Maisha na Ebru TV.

Mnamo 2005, nilishiriki kongomano la Kiswahili mjini Arusha, Tanzania.

Lilipania kuwahamasisha Wanaafrika Mashariki kuhusu umuhimu wa umoja na mshikamano wa jumuiya yetu kupitia Kiswahili. Chini ya ufadhili wa Shirika la Elimu Barani Afrika (ADEA) lenye makao makuu jijini Abidjan, Ivory Coast, nilishiriki kongamano jingine jijini Kampala, Uganda mnamo Novemba 2018.

Semina hiyo ilihusu utambuzi, utumikaji na uandishi katika lugha zetu za Afrika.

Hapa Kenya, nimeshiriki makongamano mengi ambayo yameandaliwa na KICD na mashirika mbalimbali ya uchapishaji.

Una maazimio gani ya baadaye maishani na kitaaluma?

Lengo kuu ni kupata shahada ya kwanza katika ualimu. Kwa sasa mimi ni mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Kenyatta. Ninaazimia pia kuandika vitabu vingi ambavyo vitakuwa na msisimko wa kipekee miongoni mwa wasomaji.

Ni kipi cha pekee unachokifanya tofauti na wenzako kitaaluma?

Ninatofautiana na wengi kimsimamo. Kuna baadhi ya magwiji ambao nimetofautiana nao mara nyingi kuhusiana na masuala ya Kiswahili. Mimi daima huunga au kupinga hoja bila ya kuangalia mtoaji wa hoja ni nani. Nikoseapo, mimi huungama hakuna “bingwa mazoea.” Nyenzo za utafiti ndizo zinazonikuza kila uchao. Baadhi ya nyenzo hazipo katika maktaba zetu za humu nchini. Mimi hukitegemea sana kile nijifunzacho kutokana na utafiti wangu.

Umewahi kutambuliwa na kutuzwa kutokana na mapenzi au mchango wako kwa Kiswahili?

Naam! Nimetuzwa vyeti mwishoni mwa makongamano yote mawili ambayo nilishiriki nchini Tanzania na Uganda.

Unajivunia nini kikubwa maishani na katika taaluma yako? Ninajivunia wanafunzi ambao nimewahi kufundisha na wakafanikiwa maishani.

Ninamstahi sana mke wangu Carolyne Chepchirchir na binti yangu Shirleen Betty.

Mungu awahifadhi katika wingi wa afya na baraka.