GWIJI WA WIKI: Yohana ‘Mwana-Kitivo’ Kamwaria
Na CHRIS ADUNGO
KUMHINI mtu lugha yake ni kumuumbua! Kiswahili ni sawa na masomo mengine kama vile Kemia, Fizikia na Hisabati.
Mtaalamu wa Kiswahili ana uwezo wa kununua gari, nyumba, ploti na chochote kile kinachoweza kununuliwa kihalali na mhandisi, wakili, daktari au rubani kwa kukitumia na kukitumikisha Kiswahili tu.
Muhimu zaidi ni kufuata msukumo wa ndani ya nafsi yako na kutambua kuwa mafanikio ni zao la imani, bidii na stahamala. Kwa hivyo, lenga kuwa bora katika kila uteuacho kufanya na chochote uamuacho kutenda.
Huu ndio ushauri wa Bw Yohana ‘Mwana-Kitivo’ Kamwaria – mshairi shupavu, mwandishi chipukizi, mlezi wa vipaji na mwanamuziki stadi ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Upili ya Tartar Girls, Kaunti ya Pokot Magharibi.
MAISHA YA AWALI
Yohana Kamwaria alizaliwa katika kijiji cha Ngurukiri, kata ndogo ya Kigumo, eneo la Runyenjes, Kaunti ya Embu. Yeye ni mzaliwa wa nane kati ya watoto tisa wa marehemu Bw Alfonzo Nyaga Kamwaria na marehemu Mama Venanzia Kamwaria.
Alianza safari yake ya elimu katika Shule ya Msingi ya ACK Ciamanda kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Mtakatifu Paulo Kevote, Embu mnamo 1987. Huko ndiko alikofanyia Mtihani wa Kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mnamo 1990.
Kamwaria alijiunga na Chuo Kikuu cha Kenyatta mnamo 1992 kusomea shahada ya kwanza katika taaluma ya ualimu (Kiswahili na Jiografia). Akiwa huko, aliwahi kuteuliwa Mhazili Mkuu wa Chama cha Wanafunzi Wakatoliki. Aliasisi pia kwaya ya wanafunzi iliyokuwa ikishiriki uendeshaji wa Ibada za Misa na akawa mwakilishi wa wanafunzi Wakatoliki wa vyuo vya Kenya kati ya 1995 na 1996.
Alikuwa akiyaendesha majukumu yake katika Masjala ya Katoliki ya Vijana na Walei chini ya ulezi wa Padre Paulino Mondo wa Shirika la Wamisheni wa Comboni katika makao makuu ya Mji wa Furaha, Nairobi.
Wadhifa huo ulimpa fursa ya kuhudhuria makongamano mengi ya kitaifa na kimataifa hususan nchini Uganda, Tanzania na Italia (Vatican). Isitoshe, alipata majukwaa maridhawa ya kutoa mihadhara ya mafunzo ya maadili na imani.
Kamwaria anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhamasishwa mno na waliokuwa walimu wake katika shule ya msingi, hasa Bi Njiru, Bi Mwaniki na Bw Simon Kapingazi waliomfundisha Kiingereza kati ya 1984 na 1986.
Mbali na Bi Mugambi aliyependa sana kumpongeza na kumtuza kila alipofaulu vyema katika mitihani ya Kiswahili shuleni St Paul’s Kevote, mwingine aliyemtia Kamwaria motisha na kumwamshia utashi na hamasa ya kukichangamkia Kiswahili; ni Dkt Richard Makhanu Wafula wa Chuo Kikuu cha Kenyatta.
UALIMU
Baada ya kuhitimu ualimu mnamo Agosti 1996, Kamwaria alijiunga na Chuo Kikuu cha Urbaniana, Roma kwa masomo ya Falsafa na Dini chini ya udhamini wa Taasisi ya Falsafa na Dini ya Consolata, Nairobi. Alihitimu mwishoni mwa 1998.
Wakati akiwafunza vijana maadili na kuwapa ushauri-nasaha katika Makao ya Kitaifa ya Vijana ya Mji wa Furaha, Nairobi kati ya 1997 na 1999, Kamwaria alikuwa pia mwalimu katika Shule za Sekondari za Makongeni mjini Thika na Seminari ya Kiserian, Kaunti ya Kajiado (2000).
Alihamia mjini Kitale, Kaunti ya Trans-Nzoia mnamo 2001 na kujiunga na Taasisi ya Masomo ya Sekondari na Ualimu ya Bakhita chini ya Kanisa Katoliki la Rumbek, Sudan Kusini.
Ilikuwa hadi mwaka wa 2005 ambapo aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) na akatumwa kufundisha katika Shule ya Kitaifa ya Tartar Girls. Kwa sasa, anasomea shahada ya uzamili katika masuala ya Mawasiliano, Teknolojia na Elimu katika Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret.
Akiwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili shuleni Tartar Girls, Kamwaria aliwahi kuwaongoza watahiniwa wake 416 kusajili alama wastani ya 7.5 (B-) katika KCSE Kiswahili 2019. Anasema matokeo hayo ni zao la ushirikiano mkubwa miongoni mwa walimu na kuwepo kwa Chama cha Wakereketwa wa Kiswahili Tartar (CHAWAKITA) alichokiasisi mnamo 2010 kwa msaada wa mwanahabari wa Taifa Leo, Bw Osborn Manyengo.
CHAWAKITA kilizinduliwa rasmi mnamo 2012 chini ya uvuli wa Chama cha Kitaifa cha Wasomaji wa Taifa Leo (WAKITA) na Kampuni ya Nation Media Group (NMG). Kamwaria amekuwa akiwaelekeza wanachama wa CHAWAKITA kuandaa kazi mbalimbali za kibunifu, kutuma barua kwa mhariri na kushiriki kikamilifu Shindano la Uandishi wa Insha katika gazeti hili la Taifa Leo.
Bw Ogoti Ongarora ambaye hushirikiana pakubwa na Kamwaria katika Idara ya Kiswahili shuleni Tartar Girls, aliwahi kutawazwa Mwalimu Bora wa Mwaka (TOYA) 2018.
UANDISHI
Uandishi ni sanaa iliyoanza kujikuza ndani ya Kamwaria tangu akiwa mtoto mdogo. Mbali na kutunga na kukariri mashairi, alikuwa mwandishi hodari wa Insha.
Kwa sasa anatarajia Oxford University Press (OUP) imchapishie riwaya ‘Safari ya Usuli’ na shirika la East African Educational Publishers (EAEP) limfyatulie ‘Diwani Aali ya Ushairi: Maandalizi ya KCSE’.
Mengi ya mashairi yake yamekuwa yakichapishwa katika gazeti hili tangu 2012-15. Kwa sasa anashughulikia miswada ya novela ‘Msala wa Umma’ na riwaya ‘Nilipotua Mapito’ kwa matarajio ya kuchapishwa hivi karibuni.
Kati ya wanafasihi waliompigia mhuri wa kuwa mwandishi mzuri wa Kiswahili na kumpa msukumo wa kupiga mbizi katika bahari ya utunzi wa vitabu vya Kiswahili mnamo 2016, ni marehemu Profesa Ken Walibora na marehemu Omar Babu almaarufu Abu Marjan.
MUZIKI
Kamwaria ni mwalimu wa kwaya katika Kanisa Katoliki la St Patrick’s Kibomet, Kitale. Ndiye mwasisi na kiongozi wa kikundi cha Kwaya ya Moyo Mtakatifu wa Yesu Kristu. Mbali na kipaji cha uimbaji, pia ana uwezo wa kucheza vyombo na ala mbalimbali za muziki.
Alishirikiana na Mwalimu Gabriel Mkude Sekulu wa Kwaya Kuu ya Mtakatifu Cesilia, Arusha, Tanzania kuzindua kanda ya sita ya DVD ya Wanamoyo Mtakatifu wa Yesu mnamo 2019.
Nyimbo za Kamwaria zimeimbwa na kurekodiwa kwingi katika janibu za Kitale, Bungoma, Pokot Magharibi, Kabarnet, Nairobi, Meru, Uganda na Tanzania.
Baadhi ya vibao hivyo vinapatikana kwenye mtandao wa YouTube kwa anwani ‘Moyo Mtakatifu wa Yesu Kibomet Kitale Kenya’.
JIVUNIO
Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake, Kamwaria anaazimia kuweka hai ndoto za kuwa mwandishi stadi wa Kiswahili. Anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu na wasomi ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Mnamo 2019, alipata fursa ya kuwa mwelekezi mkuu wa jopo lililomwandaa Bi Grace Ataro Onyango wa Shule ya Upili ya St Monica Girls, Kitale aliyekuwa akiwania taji la Mwalimu Mkuu Bora wa Mwaka (POYA) katika Kaunti ya Trans-Nzoia.
Kamwaria anajivunia kuwa kiini cha motisha ambayo kwa sasa inatawala wengi wa wanafunzi na walimu ambao wametangamana naye katika warsha za masuala ya dini, vikao vya wanamuziki, makongamano ya Kiswahili na tamasha za kitaifa za muziki na drama.
Baada ya kuwa Mtahini Mkuu wa Kiswahili kwa kipindi kirefu, yeye kwa sasa ni kinara wa ‘Dira Yetu’. Hiki ni Chama cha Walimu wa Somo la Kiswahili katika Kaunti Pokot Magharibi ambacho kiliasisiwa mnamo Februari 2020.
Kwa pamoja na mkewe Bi Bancy Njoki, wamejaliwa watoto watano: Elsa, Daniella, Antoinnete, June Wendo, na Afra Imani.