Makala

GWIJI WA WIKI: Yvonne Wavinya

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 4

Na CHRIS ADUNGO

UKIONA mtu amekata tamaa, chanzo huwa ni mawazo yake!

Kushindwa au kufaulu katika jambo lolote hutegemea jinsi unavyowaza.

Pania sana kuelewa wewe ni nani kwa kufahamu ukubwa wa uwezo wako. Ili ufanikiwe, ni vyema uwe na nidhamu katika hisia zako kwa kuwa ndiyo njia ya pekee ya kujifunza mambo mengi.

Haitawezekana kabisa kwa mengi ya matarajio yako kutimia iwapo hutakuwa na malengo mapya ya mara kwa mara. Badili mtazamo wako kuanzia sasa na amini kwamba jitihada zako zitazaa matunda.

Utakapopania kutia bidii katika kazi yako, Mungu atafanikisha chochote utakachokitia mikononi. Mwamini sana Mungu Muumba wako kwa kuwa ndiye wa pekee mwenye uwezo wa kukufungulia milango ya heri maishani.

Huu ndio ushauri wa Bi Yvonne Wavinya James Nee-Matheka ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Machakos Baptist.

Maisha ya awali

Yvonne alizaliwa mnamo Septemba 1, 1969 katika kijiji cha Misouni, eneo la Kalama, Kaunti ya Machakos akiwa mtoto wa nne katika familia ya watoto saba wa marehemu Bi Rose Mukini na marehemu mwalimu mstaafu Bw Jones Mutua Matheka aliyewahi kufundisha Kiswahili na somo la Hisabati katika Shule ya Msingi ya Kikumbo, Kalama.

Yvonne alipata elimu ya msingi katika Shule ya Kikumbo kati ya 1974 na 1982 kabla ya kujiunga na Shule ya Upili ya Machakos Girls na kuhitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCE) mwishoni mwa 1986.

Alisomea ualimu katika Chuo cha Walimu cha Mosoriot, Kaunti ya Nandi kati ya 1992 na 1994.

Msukumo wa kujiendeleza kitaaluma ulimchochea kujiunga na Chuo Kikuu cha Nairobi kusomea Shahada ya Kwanza katika Ualimu (Kiswahili na Dini) mnamo 2006.

Tangu ahitimu mwishoni mwa 2011, amekuwa mkufunzi wa Kiswahili na somo la Dini katika vyuo mbalimbali katika Kaunti ya Machakos.

Yvonne anatambua ukubwa wa mchango wa marehemu baba yake katika kumwelekeza, kumshauri na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Aliyemshajiisha kujitahidi masomoni akiwa mwanafunzi na pia kujituma zaidi kitaaluma akiwa mwalimu; ni marehemu kaka yake Bw Josephat Kyalo aliyepanda na kuotesha ndani yake mbegu za kusoma kazi nyingi za Kiswahili na hadithi za kila sampuli.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa na Yvonne kwa sasa katika ulingo wa Kiswahili ulichangiwa pakubwa na tukio la yeye kufundishwa na watu ambao zaidi ya kubobea ajabu katika taaluma, pia wa iipenda na kutawaliwa na ghera ya kuipigia chapuo lugha hii.

Anakiri kwamba mtagusano wa karibu aliokuwa nao na wahadhiri wake katika Chuo Kikuu cha Nairobi; hasa Dkt Evans Mbuthia, Dkt Zaja Omboga, Profesa Raya Timamy na Profesa Iribe Mwangi ulimpa ilhamu ya kukithamini Kiswahili. Kariha na motisha zaidi ilitoka kwa wanafunzi wenzake waliokuwa wakimpongeza mara kwa mara kwa matamshi yake fasaha ya Kiswahili na upekee wa kiwango chake cha ubunifu katika utunzi wa nyimbo na mashairi.

Wengine waliomtandikia Yvonne zulia zuri la Kiswahili kwa imani kuwa ni lugha iliyo na upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote ni Profesa Kyallo Wadi Wamitila na aliyekuwa mwalimu wake shuleni Machakos Girls, Bw Kilae.

Ingawa kwa wakati fulani changamoto za kila sampuli zilitishia kuuzima kabisa mshumaa wa tumaini lake la kukamilisha masomo ya Chuo Kikuu, Yvonne anatambua ukubwa wa mafao aliyoyapokea kutoka kwa mavyaa wake marehemu Mary Nzilani, dada yake Jane Mutindi (mwanabenki) na mashemeji zake Davis Maeke (mwalimu mstaafu) na John Alphonse (askari polisi mstaafu).

Ualimu

Baada ya kuhitimu masomo ya sekondari mnamo 1986, Yvonne alipata kibarua cha kufundisha katika Shule ya Msingi ya Kinoi, Kalama. Alihudumu huko kwa kipindi cha miaka sita kabla ya kujiunga na Chuo cha Walimu cha Mosoriot.

Ni wakati akiwa Mosoriot ambapo alitambua utajiri wa kipaji chake katika uigizaji, ulumbi, utunzi wa mashairi na uimbaji.

Mnamo 1994, Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) ilimtuma katika Shule ya Msingi ya Kinoi na akateuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili. Alifundisha huko kwa kipindi kifupi kabla ya kuajiriwa kuwa mhazili katika Afisi za Elimu, Tarafa ya Kalama, Machakos.

Pamoja na kufanya uhazili, Yvonne aliendelea kufundisha Kiswahili katika Shule ya Msingi ya Kinoi na baadaye katika shule za msingi za Kimutwa na Kwa-Kavoo, Machakos.

Ilikuwa hadi Desemba 1995 ambapo Yvonne alifunga pingu za maisha na mumewe mpendwa, Bw Benjamin James Kithuka.

Baada ya kufuzu katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alihamia katika Shule ya Msingi ya Machakos Baptist anakozidi kuamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake.

Mbali na kuwa Mkuu wa Idara ya Kiswahili shuleni humo, Yvonne pia ni mwanajopo wa kutunga mitihani ya viwango mbalimbali katika Kaunti ya Machakos. Isitoshe, yeye ni mwamuzi wa kupigiwa mfano katika tamasha za kitaifa za muziki na drama na pia amewahi kuwa Mtahini wa Baraza la Mitihani la Kenya (Knec) kati ya 2007 na 2015.

Yvonne kwa sasa analenga kuwachochea wanafunzi wake kusajili alama za juu zaidi katika KCPE Kiswahili mwaka 2019.

Kwa pamoja na Bi Jane Muthoni Njeru ambaye ni Mwalimu Mkuu shuleni Machakos Baptist, anaungama kwamba kufaulu kwa mwanafunzi katika somo lolote ni zao la imani, bidii, nidhamu na mtazamo wake kuhusu somo lenyewe na mwalimu anayetangamana naye darasani.

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Kiswahili shuleni Machakos Baptist (Bi Joyce Mwaniki, Bw Amos Mutua, Bi Alice Kisinga, Bi Florence Mulwa na Bi Ann Kilonzo), ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaoujivunia kila mwaka matokeo ya KCPE yanapotolewa.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake, Yvonne ambaye pia ni mmiliki wa kikundi cha Wajopa Creative Designers, anajivunia kuwa kiini cha motisha na hamasa ambayo kwa sasa inawatawala walimu wengi anaoshirikiana nao katika jitihada za kukitetea Kiswahili.

Wajopa ni kikundi kinachojishughulisha na ufinyanzi wa bidhaa mbalimbali zinazowaniwa pakubwa katika masoko mengi ya Kaunti za Machakos, Kitui, Garissa, Kajiado, Makueni na Nairobi.