• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Haja ipo maski zivaliwe vizuri ili kuepeuka kuambukizwa corona

Haja ipo maski zivaliwe vizuri ili kuepeuka kuambukizwa corona

Na SAMMY WAWERU

AGIZO la Rais Uhuru Kenyatta la Jumatano “hakuna kupata huduma ikiwa hujavalia maski” limezua hisia tofauti miongoni mwa wananchi.

Rais Kenyatta alitoa amri hiyo kufuatia kuendelea kuongezeka kwa maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 nchini. Isitoshe, idadi ya maafa yanayoandikishwa kutokana na virusi hivyo inaongezeka.

Chini ya muda wa majuma mawili yaliyopita, idadi ya wagonjwa walioandikishwa kuambukizwa Homa ya Corona imeonekana kuongezeka mara dufu na kwa kasi.

Hali hiyo imechangiwa na utepetevu wa wananchi, viongozi wakiwa katika mstari wa mbele kuvunja na kukiuka sheria na mikakati iliyotolewa na Wizara ya Afya kusaidia kuzuia kuenea kwa corona.

Kati ya mikakati hiyo, ni pamoja na kuvalia maski kila wakati hasa katika maeneo ya umma, kutakasa mikono kwa jeli yenye kemikali kuua virusi vya corona au kunawa mikono kwa sabuni, kuzingatia umbali kati ya mtu na mwenzake, miongoni mwa mingine.

Rais Kenyatta aliweka paruwanja kuwa ni hatia kutembea bila maski, barakoa. “Iwapo huna maski hutapata huduma,” akaagiza kiongozi huyo wa nchi, akisisitiza amri hiyo itekelezwe katika maeneo yote yanayotoa huduma za umma, akitaja masoko kuwa miongoni.

Amri hiyo ya Rais imepokelewa kwa hisia tofauti, Wakenya wengi wakielekeza maoni yao katika mitandao ya kijamii. “Umma imelegea kuheshimu sheria na mikakati kudhbiti Covid-19, tuvalie maski ili tuondoe janga hili nchini,” akaelezea Councillor Njohi kwenye Facebook.

Kisa cha kwanza cha corona kiliripotiwa nchini Machi 2020, na siku za kwanza wananchi walitii mikakati iliyotolewa na Wizara ya Afya, ambayo pia imeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

“Itakuwaje ikiwa ni mtumishi wa umma ambaye hajavalia maski wakati anahudumia wananchi?” akataka kujua Victor Bwire.

“Ubora wa maski unapaswa kupigwa msasa kwa sababu baadhi wanavalia vitambaa vya kuchemua na kupiga chavya,” Khaemba Sifwabi Lusweti amependekeza.

Suala la uvaliaji maski vizuri limekuwa likizua gumzo, ambapo Julai 2020 Gavana wa Nyeri, Mutahi Kahiga alieleza kushangazwa kwake na watu wanaoininginiza kidevuni badala ya kuivalia ipasavyo.

Wataalamu wa afya wanasema barakoa inapaswa kufunika mdomo na pua ili kuepuka kutagusana na matone ya mate au maji yoyote yale yanayotoka kwa mtu.

“Katika Kaunti ya Nyeri, idadi kubwa ya wakazi wana maski ila wanaining’iniza kidevuni hata wakiwa maeneo ya umma. Ni taswira ya maeneo mengine nchini,” Bw Kahiga alisema, akipendekeza maafisa wa usalama kukamata wasiovalia barakoa vizuri na kuwachukulia hatua kali kisheria kwa kile alitaja kama “mtandao unochangia kuenea kwa corona”.

Wakati akitangaza kukaza kamba baadhi ya sheria alizokuwa amelegeza, Rais Kenyatta alikiri viongozi wamekuwa katika mstari wa mbele kukiuka mikakati kudhibiti kuenea kwa Covid-19, ugonjwa ambao sasa ni janga la kimataifa.

“Kama viongozi, mimi nikiwa mmoja wao, tumeanguka mtihani kwa sababu ya vile tumekuwa tukijiendesha ni kama hakuna ugonjwa. Kuandaa mikutano ya umma bila barakoa, kuleta watu pamoja…mambo haya ndiyo yametuumiza…” akaelezea Rais, akionya “serikali itachukulia hatua anayevunja sheria awe ni nani ama ni nani”.

Ripoti ya Maridhiano, BBI ilipozinduliwa majuma machahe yaliyopita, Rais Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga wamekuwa wakiendeleza kampeni katika mikutano ya umma kuhamasisha upitishaji wa ripoti hiyo, ili kuifanyia Katiba marekebisho.

Naibu wa Rais, William Ruto, kwa upande wake amekuwa akizuru maeneo tofauti nchini, naye akionekana kushinikiza ripoti hiyo kufanyiwa marekebisho ili kuwafaa wananchi.

Dkt Ruto hata hivyo mnamo Jumanne alitangaza kusimamisha hafla zake kwa muda, akitaja hatua hiyo kama njia mojawapo kusaidia kudhibiti maenezi ya corona.

Yote tisa, kumi, Rais alisimamisha mikutano ya umma kwa muda wa siku 60 zijazo, na kwa wanaotaka kuiandaa wakitakiwa kuifanya katika ukumbi na kuzingatia sheria na mikakati. Alisema wanaohudhuria wasizidi thuluthi moja ya idadi jumla ya ukumbi.

Huku umma ukitakiwa kuvalia maski ili kupata huduma, ni muhimu mkazo utiliwe kuivalia ipasavyo ili tulishinde janga hili la Covid-19.

You can share this post!

Blue Nile Rolling Mills yazidi kupiga hatua licha ya janga...

Wahudumu wa afya watishia kuendelea na mgomo Mombasa