Hamasisha watoto kuhusu dijitali, usiwaadhibu
BAADHI ya wazazi wamekuwa wakiadhibu watoto wao wakome kutumia mitandao ya kijamii.
Kwa kufanya hivi, wanabadilisha maelezo ya kujitambulisha ya akaunti za watoto wao na hata kuzifunga au kuwapokonya vifaa bebe.
Ingawa hatua kama hii inafaa kulingana na jinsi mzazi anavyomfahamu mtoto wake ili kumsaidia kuepuka athari za kudumu anazoweza kujisababishia anapochapisha jumbe na maudhui mtandaoni, wataalamu wanasema zinaweza kuwa na matokeo hasi kwa mtoto.
“Kwa mfano, mtoto aliyeadhibiwa anaweza kuwa mwangalifu zaidi katika kuchapisha jumbe zisizo na heshima mtandaoni, lakini pia anaweza kujifunza kwamba kuwadhalilisha wengine ni jambo zuri kwa kuchukulia kuwa anadharauliwa mtandaoni,” asema mtaalamu wa malezi dijitali Sarah Albert.
Anasema kulingana na utafiti, asilimia 77 ya wazazi wanafuatilia tovuti ambazo watoto wao wametembelea, na kuifanya hii kuwa mbinu ya kawaida ya kinidhamu.
Kinachostaajabisha zaidi ni kwamba uchunguzi huo huo, uligundua kuwa karibu theluthi mbili ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 17 walikuwa na wazazi wao kama marafiki kwenye tovuti za mitandao ya kijamii.
Hivyo basi, asema Albert, wazazi wanaweza kutumia mitandao ya kijamii kama njia ya kuwaruhusu watoto wao kuwafikia wakati wowote.
Hii inawafanya watoto kuchukulia wazazi wanawajali na kutii ushauri wowote ambao watapatiwa. Kwa kufanya hivi, wazazi hawatahitaji kufunga akaunti za mitandao ya kijamii za wanao.
Ingawa katika hali ya kwanza ambapo wazazi wanazima akaunti za mitandao ya kijamii watoto wanaweza kuishia kuhisi kutoheshimiwa na hatua za wazazi, katika hali ya pili, mzazi anaweza kuishia kuhisi kuthaminiwa na kutumia mitandao ya kijamii kujifaidi huku akiepuka athari hasi za majukwaa hayo.
Pande zote mbili zikihisi kusikilizwa, na kuheshimiwa zinajenga uhusiano wa karibu na hivyo kufanikisha matumizi salama ya mitandao ya kijamii, asema Albert.