Makala

Handisheki inaweka vizuizi Ruto kupata funguo za Ikulu?

August 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

UAMUZI wa Raila Odinga kufanya kazi kwa ushirikiano na Rais Uhuru Kenyatta unadadisiwa kuzidisha ugumu wa Naibu Rais, William Ruto kurithi funguo za Ikulu 2022.

Odinga tangu 2013 hajaficha taswira ya pingamizi alizo nazo kwa uwezekano wa Ruto kuwa Rais na ni hivi majuzi tu alionya kuwa Ruto ili afanikiwe kuwa Rais, ni lazima asake uungwaji mkono kutoka kwake.

Wadadisi wanaonekana kuungama kuwa onyo hilo lilikuwa dhaifu Odinga akiendeleza siasa za ukaidi dhidi ya UhuRuto, lakini sasa ni onyo hatari akiwa amekumbatia siasa za handisheki.

Odinga anaorodheswa kuwa hatari nyingine kwa azima ya Ruto kuwa Rais ikizingatiwa kuwa ndani ya UhuRuto kuna mirengo inayoandaa njama ya kuzima ndoto yake ya urais.

Kwa mujibu wa mrengo unaoibuka katika ngome muhimu ya kufanikiwa kwa urithi huo ya Mlima Kenya, Rais Kenyatta anafaa abadilishe mbinu ya ni kwa nini hasa anampendekeza Ruto.

Ukaidi huo dhidi ya Ruto umeanza kushika kasi katika eneo la Mlima Kenya huku mbunge wa Nyeri Mjini, Bw Wambugu Ngunjiri hata akisusia ziara ya Ruto ya Kaunti ya Nyeri.

Bw Ngunjiri tayari amemuonya Ruto kuwa hakuna sheria ambayo inampa urithi bila ya kuushindania na ajiandae kukabiliana na upinzani mkuu eneo la Kati.

Wimbo huo wa Bw Ngunjiri sio mgeni kwa kuwa aliyekuwa Gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo alitoa pingamizi zake 2017 akifuatiwa na kinara wa Narc-Kenya, Bi Martha Karua na pia aliyekuwa Seneta maalumu, Ben Njoroge kutoka Nakuru.

Sasa, Mwakilishi wa Wanawake wa Kaunti ya Murang’a katika Bunge la Kitaifa, Bi Sabina Chege amesema Rais Kenyatta anafaa kumjenga mrithi kutoka Mlima Kenya ambaye atahakikisha masilahi pana ya eneo hilo yamesimamiwa kwa njia thabiti katika uchaguzi mkuu wa 2022.

“Rais Kenyatta anafaa kuanza kuandamana na atakayetwaa usemaji wa kijamii katika siasa zake. Hatutaki kujipata katika sintofahamu ya 2022. Bw Ruto yuko nyanjani akijiimarisha na ambapo amekuwa akiwajenga wanasiasa chipukizi kama Ababu Namwamba kutoka Magharibi, Kipchumba Murkomen wa Elgeyo Marakwet na wengine kadhaa,” akasema akiwa katika mahojiano ya kituo cha Kameme FM.

Wanaompinga Ruto kwa sasa eneo hilo wanasema kuwa hawafanyi hivyo kwa njama yoyote ile, bali kile wanapambania ni haki za kisiasa, kiuchumi na kijamii kwa wenyeji zitambuliwe na zidumishwe.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua, Elias Mbau na ambaye ni mwandani wa aliyekuwa mbunge wa Gatanga, Bw Peter Kenneth anasema kuwa “kutuambia tumchague Ruto bila ya kwanza kuandaa mkataba wa kimaelewano ni wazo butu sana la kisiasa.”

 

“Rais na Ruto wanafaa wabadilishe mbinu na wauze mradi huo wa kisiasa katika msingi wa utendakazi na kubadilisha maisha ya Wakenya,” anasema Peter Kenneth.

Anasema kuwa hizo ndizo siasa ambazo kambi ya Bw Ruto imekuwa ikisukumia Mlima Kenya “ambapo vipaza sauti wake kama gavana wa Uasin Gishu, Jackson Mandago amekuwa mwingi wa semi za vitisho, mafumbo ya kusambaza taharuki kwa wapiga kura wa Mlima Kenya kuhusu ahadi kuwa deni.”

Mbunge wa Rongai, Raymond Moi akiwakilisha sauti ya Seneta wa Baringo na aliye nduguye, Gideon Moi anasema kuwa hakuna deni kati ya Kalenjin na Agikuyu.

“Hayati Mzee Jomo Kenyatta alimtuza babangu, Daniel Moi na urithi wa urais. Naye Moi akajibu wema huo kwa kumwandaa Uhuru Kenyatta kuwa Rais. Deni likaisha. Sasa hakuna deni iko kati yetu na katika uchaguzi wa 2022, sisi tutapinga Ruto kuhadaa Wakenya kuwa kuna deni la kisiasa ambalo anafaa kulipwa na Agikuyu,” akasema Raymond.

Ukaidi huo unaonekana kusambaa hadi kwa vyama washirika kwa Jubilee ambapo kinara wa Maendeleo Chap Chap, Dkt Alfred Mutua anasema kuwa wazo hilo la Rais halina msingi wa kisheria.

“Sijaona kipengele chochote katika katiba kinachosema kuwa ni lazima wadhifa wa urais uwachie mtu. Atawachiwa kwani ni miliki ya yeyote? Nyadhifa za kugombewa huwa ni za raia na wao ndio wanafaa kuamua,” anasema Dkt Mutua.

Anasema kuwa atawania urais 2022 na hatarajii kuambiwa akome kwa msingi kuwa ni wadhifa ambao umeahidiwa mtu.

Dkt Mutua anasema kuwa hadi sasa kuna taswira inayojiunda ya hatari kuu “taifa kukabidhiwa wanyakuzi wa mashamba na wapujaji wa pesa za kimaendeleo.”

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria anasema kuwa kuna njama inayojiunda ya kumzima Ruto.

 

Bw Kuria anasema kuwa hata wengi kutoka Mlima Kenya waliokuwa wakimpigia debe Ruto kabla ya Rais Kenyatta kujishindia awamu ya pili Ikulu wamenyamaza tuli siku hizi, kuashiria kuwa kuna mengi yanaendelea kichinichini na ambayo yataishia “kuangazia jamii yetu kama isiyoaminika katika kutoa ahadi za kisiasa.”

“Hata mimi nimehama mrengo huo wa Ruto na sasa nimejiunga na wale ambao wanangoja tu kuona itakuwa namna gani, mimi nikiwa tayari nimetangaza kuwa katika uchaguzi huo nikiwa mwaniaji wa urais,” akasema Kuria.