Hatari ya nyumba nafuu za serikali
SERIKALI imetoa kandarasi za ujenzi wa nyumba za bei nafuu za jumla ya Sh49.5 bilioni katika ardhi ambayo haina hati miliki, na hivyo kuongeza hatari na mkanganyiko ambao umezingira mpango huo huku umma ukikosa imani nao.
Hili linazua maswali kuhusu jinsi Wakenya wanaonunua nyumba kutoka kwa miradi hiyo watapata hati za kuzimiliki bila kuwa na hatimiliki asili, wakati ambapo mpango wa nyumba za bei nafuu (AHP).
“Idara ya Serikali inayosimamia nyumba ina mikataba na wanakandarasi mbalimbali kwa ujenzi wa nyumba za bei nafuu kote nchini kwa jumla ya Sh49,456,549,086. Hata hivyo, hati za umiliki wa ardhi za maeneo ambayo miradi inatekelezwa hazikutolewa kwa ukaguzi,” Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Nancy Gathungu anasema katika ripoti ya ukaguzi ya hadi Juni 2024.
Ripoti hiyo inafichua kuwa suala hilo linaweza kuzuia uuzaji wa nyumba kwa umma, kwa kuwa hati miliki za nyumba haziwezi kutolewa bila hati miliki asili ya ardhi zilikojengwa.
Hatua ya idara ya serikali, hata hivyo, inaongeza tu utata ambao umekumba AHP, na mawasiliano yasiyoeleweka kuhusu malengo, mafanikio na hata maendeleo ya mradi huo, huku Wakenya wakikosa kuchangamkia nyumba za mradi huo mkubwa wa Rais William Ruto.
Idara ya serikali ilitia saini kandarasi ili nyumba hizo zijengwe katika ardhi isiyo na hatimiliki licha ya ufichuzi wa hivi majuzi wa jinsi umiliki wa ardhi ya Serikali ya Kaunti ya Nairobi ulivyohamishwa kwa mwekezaji wa kibinafsi ambaye kisha aliitumia kuchukua mkopo wa benki wa Sh1.9 bilioni.
Serikali imekuwa ikitetea AHP huku maafisa wakuu wa serikali wakipigia debe mafanikio yake.Hii ni licha ya kubainika kuwa ni mmoja pekee kati ya watu wazima 559 wanaoweka akiba katika jukwaa la Boma Yangu ili kumiliki nyumba za AHP huku Wakenya wengi wakipanga kujenga badala ya kununua nyumba.Hapo awali, lengo lilikuwa kujenga nyumba 250,000 kwa mwaka kabla ya kupunguzwa hadi 200,000.
Tangu Rais Ruto aingie mamlakani zaidi ya miaka miwili iliyopita, ahadi hiyo haijatekelezwa.Serikali inasema kwamba sasa iko katika mipango ya mwisho ya kuzindua nyumba 4,888 za kwanza mwezi huu, na kwamba nyumba 140,000 ziko katika hatua tofauti za ujenzi.
”Nitatoa nyumba 4,888 kwa umma mwishoni mwa Machi na kila robo mwaka nitakuwa nikitoa nyumba kati ya 4,000 na 5,000. Katika mwaka mmoja ujao, ninapaswa kuwa na karibu nyumba 140,000,” Waziri wa Ardhi na Makazi Alice Wahome alisema mwezi uliopita.
Serikali pia haijakuwa wazi kuhusu idadi ya nafasi za kazi zilizoundwa kupitia miradi ya AHP, huku maafisa wa umma wakipinga takwimu katika nyaraka rasmi za serikali.

Bi Wahome wakati wa mahojiano mnamo Februari 19 alisema kuwa nafasi za kazi milioni 1.12 zimeundwa kupitia nyumba 140,000 zinazoendelea kujengwa, huku takriban Wakenya wanane wakiripotiwa kufanya kazi katika kila nyumba. Hata hivyo, katika Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS) Hazina ya Kitaifa yasema kwamba ‘AHP imeunda zaidi ya ajira 164,000 kupitia mfumo wa thamani ya nyumba.
“Mnamo Septemba mwaka jana, idara ya serikali ya makazi ilisema kuwa nafasi za kazi 160,000 zimeundwa katika nyumba 100,000. Takwimu zinazotofautiana zimeongeza mkanganyiko huo, huku Wakenya wengi wakitatizika kuelewa jinsi Ushuru wa Makazi wa asilimia 1.5 wanaokatwa kutoka kwa mishahara tangu Julai 2023 unavyotumiwa.
Kufikia Desemba 2024, serikali ilikuwa imekusanya Sh88.7 bilioni kutoka kwa Ushuru wa Nyumba unaokatwa wafanyikazi na waajiri, ambapo Sh46 bilioni ziliwekezwa katika Hazina ya Kitaifa.
Uchunguzi wa Shirika la Kitaifa la Takwimu Kenya (KNBS) wa 2023/24 unaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya Wakenya (asilimia 55.5) wanapendelea kujenga nyumba zao, huku asilimia 12.5 wakipendelea kununua.
Hatari nyingine inayoikabili serikali katika mpango wake wa AHP imetajwa kuwa shaka kuhusu uendelevu wa mapato ya wanaolengwa ambao watatakiwa kutoa malipo ya kila mwezi hadi miaka 30 hivyo kukabiliwa na hatari ya kufukuzwa pale wanaposhindwa kulipa.
Hatua hii inazua hatari ya uendelevu wa mpango huu, huku walengwa wengi wakiwa ni Wakenya katika sekta isiyo rasmi ambayo huathiriwa na matukio ya kupoteza kazi au kukosa mapato.
Uchunguzi wa Benki Kuu ulibainisha kuwa karibu nusu (asilimia 42) ya kampuni nchini ziliwafuta kazi wafanyakazi wa kawaida kutokana na hali ngumu ya uchumi, wengi wa wafanyakazi hao wakiwa wanaolengwa katika mpango huo.
Wizara inasema mtu yeyote ambaye atashindwa kutoa malipo ya kila mwezi ya nyumba hizi atafurushwa, jambo ambalo tafiti za awali za kiuchumi na wachumi zimebainisha kuwa hatari kubwa.Hii ni kwa sababu wengi wa wanaolengwa ni maskini zaidi katika jamii na mapato yao si ya kutegemewa.
Hatari ya matajiri wenye ushawishi mkubwa kutumia vibaya mpango huo kwa kujitwalia nyumba ili wauze kwa bei kubwa imekuwepo, hasa baada ya Hazina ya Kitaifa kuruhusu mtu mmoja kumiliki zaidi ya nyumba moja.

Wizara inasema kwamba bodi ya nyumba za bei nafuu, ambayo inasimamia mpango huo, itakuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu ni nani atapata nyumba gani.
Waziri Wahome alisema kuwa pindi mtu anaponunua nyumba kupitia AHP, atapewa hati miliki ambayo itadumu hadi miaka 99, ambapo mtu aliye na hati miliki ya awali ya ardhi anaweza kubadilisha masharti ya makubaliano ya umiliki na kuwalazimu wenye nyumba kulipa pesa zaidi.
Hili linaibua maswali kuhusu iwapo hati miliki za ardhi kunakojengwa miradi ya AHP zinafaa kuwa katika majina ya mashirika ya kibinafsi na watu binafsi, kinyume na serikali inavyotaka sheria.
Hii ni kufuatia maelezo kwamba kampuni inayohusishwa na raia wa Uturuki mwenye utata na mshirika wa Rais Ruto, Harun Aydin, iliorodheshwa kujenga nyumba 100,000.
Bw Aydin alifurushwa kutoka Kenya katika mazingira ya kutatanisha mwaka wa 2021.