Makala

Hii ni yako: Wakenya wamchemkia Cherargei anayelenga kuongeza muhula wa Ruto

Na VICTOR RABALLA October 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKENYA wamewasilisha maoni kwa wingi kuhusu pendekezo la kuongeza muhula wa kuhudumu kwa rais na viongozi waliochaguliwa huku uchambuzi wa awali ukiashiria upinzani mkali kwa mswada huo.

Saa chache kabla ya mwisho wa zoezi la kutoa maoni Ijumaa, Oktoba 25, 2024, idadi ya juu zaidi ya barua pepe zilikuwa zimetumwa huku seneti ikisema ilikuwa imepokea zaidi ya 200,000.

Bunge la Seneti liliomba radhi kwa usumbufu uliotokea kwa kuwa halingeweza kupokea jumbe zaidi kupitia barua pepe rasmi na kutoa wito kwa Wakenya kuendelea kutuma maoni yao kupitia barua pepe mbadala, [email protected].

‘Asante kwa majibu mengi kuhusu Mswada wa Katiba ya Kenya (Marekebisho) (Nambari 2), 2024. Kutokana na wingi wa mawasilisho, mfumo wetu wa barua pepe umekumbwa na matatizo kwa muda,’ seneti ilichapisha kwenye akaunti yake rasmi ya X.

Seneti ilichukua hatua hiyo muda mfupi baada ya kuanza kusikiliza maoni ya umma kuhusu Mswada wa Marekebisho ya Katiba ya Kenya (Marekebisho) ya 2024, mbele ya Kamati ya Seneti ya Haki na Masuala ya Kisheria katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta.

Mswada huo unaofadhiliwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei unalenga kurekebisha vifungu vya 101, 177, na 180 vya Katiba ili kuongeza muhula wa kuhudumu wa Wabunge, Maseneta na Magavana kutoka miaka mitano ya sasa hadi saba.

Huku Seneta Cherargei akisema kuwa miaka mitano haitoshi kwa viongozi kutekeleza majukumu yao ya kikatiba kikamilifu, mapendekezo hayo yamepokewa kwa hasira na Wakenya.

Wakenya kadhaa wamedai kuwa Bw Charargei ambaye ni mshirika wa karibu wa Rais William Ruto anatumiwa na serikali kupima hali.
Katibu mkuu wa United Democratic Alliance (UDA) Hassan Omar pia amewataka wanachama kujitenga na Mswada huo wenye utata.

‘Hii ni dharau kwa maadili yetu ya kikatiba na lazima ikomeshwe,’ Bw Omar alisema.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wa aliutaja Mswada huo kama’ usioweza kufaulu’ na kueleza imani kuwa utazimwa utakapotua katika Bunge la Kitaifa.

‘Hilo pendekezo la kisheria la Cherargei kuhusu muhula wa kuhudumu wa rais umekufa hata kabla ya kufika kwetu. Anapaswa kuokoa wakati wake mwenyewe, wa maseneta wengine na pesa za walipa ushuru,” Bw Ichung’wah alisema hivi majuzi kwenye akaunti yake ya X.

Mswada wa Seneta Cherargei unalenga zaidi kuimarisha mamlaka ya Seneti kwa kuipa mamlaka ya kipekee ya kuwachunguza na kuwaidhinisha maafisa wa Serikali, wakiwemo Mawaziri, Mwanasheria Mkuu, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Jaji Mkuu na majaji, miongoni mwa wengine.

Pia unapendekeza Seneti kuchukua mamlaka ya kuwasilisha maombi ya kuondolewa ofisini kwa wanachama wa tume ya kikatiba au afisi huru jukumu linalotekelezwa na Bunge la Kitaifa kwa sasa.

Kwa upande mwingine, unaeleza kuwa Mabunge yote mawili yanafaa kudhinisha kutumwa kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya katika sehemu yoyote ya nchi, jukumu ambalo kwa sasa ni la Bunge la Kitaifa pekee.

Mswada huo ambao ulisomwa kwa mara ya kwanza katika Seneti mnamo Septemba 26 kabla ya kuwasilishwa kwa Kamati ya Haki na Masuala ya Kisheria kuzingatiwa, umekuwa ukishirikishwa kwa umma tangu Oktoba 2.

Imetafsiriwa na Benson Matheka