Hofu sindano za kukata uzito zikiuzwa kiholela
MAPEMA wiki hii, nilizunguka kwenye maduka kadhaa ya dawa nikitafuta sindano ambazo baadhi wameripotiwa kuzitumia katika harakati zao za kupunguza uzito.
Sindano hizo almaarufu semaglutide injections ambazo pia zimeenea kwa taarifa kwamba husaidia watu wanaougua ugonjwa wa kisukari na magonjwa ya moyo, hazipaswi kupatiwa wagonjwa bila maagizo ya daktari.
Katika uchunguzi wake jijini Nairobi, mwandishi huyu, alibaini kuwa ni rahisi kuuziwa dawa hizo bila maagizo ya daktari na ziliuzwa kwa bei tofauti.
Muuzaji wa kwanza alipiga simu kwa wauzaji wawili waliomweleza kuwa nikiwa na Sh68,000 au Sh105,000 nitauziwa dawa hiyo aina ya Ozempic.
“Lakini kuna nyingine yenye bei nafuu inayojiita Sema Q ambayo ni Sh25,400,” akaniambia baada ya kuona mshangao kwa uso wangu.
Mita chache kutoka duka hilo la dawa, nilipata muuzaji mwingine aliyenishauri kuwa ataniuzia sindano hiyo kwa Sh5,800 – dozi ya Sema Q ya wiki moja.
Kwa mujibu wa Dkt Sairabanu Sokwalla, mtaalamu wa ugonjwa wa kisukari katika hospitali ya Aga Khan, sindano hizo husaidia kupunguza sukari kwa damu kwa kufanya kazi sawa na homoni ya incretin mwilini.
“Homoni hiyo huwa na kazi nyingi mwilini. Husaidia mfumo wa umeng’enyaji wa chakula kwa kukufanya ushibe kwa muda mrefu, kongosho kwa kutengeneza insulini wakati sukari ipo kwenye damu na hata ubongo ili kukupunguzia hamu ya chakula na kuhisi umeshiba kwa wakati mrefu,” anasema.
Hata hivyo, japo sindano hizi ni nzuri na zina manufaa tele kwa watu tofauti, Dkt Sokwalla anasema hazipaswi kuuzwa bila maagizo ya daktari.
“Sababu kuu ni kuwa sindano hizi huwa na dozi tofauti. Kwa watu wanaonuia kupunguza uzito wao, dozi yao almaarufu Wegovy huenda mpaka miligramu 2.4. Lakini mgonjwa anapaswa kuelekezwa jinsi atakavyojidunga,” anaeleza.
Isitoshe, Dkt Sokwalla anasema kuwa kuna athari za dawa hizi zinazotokea baada ya kuzitumia.
“Kwanza ni maumivu ya tumbo au mfumo wa usagaji chakula ambayo humfanya mgonjwa kuhisi kama tumbo limefura, kichefuchefu, kutapika, kuendesha, kukaukiwa na haja kubwa na hata kupoteza maji mengi na kuharibu figo,” anaelezea.
Pia, Dkt Sokwalla anasema mgonjwa anaweza kuathiriwa ngozi- akafura au akajikuna au hata kongosho au kibofu cha nyongo kufura.
Sindano hizi pia huwaathiri wagonjwa walio na uzito uliopita kawaida kwa kuongezea hatari ya kibofu chao cha nyongo kufura.
Matumizi ya sindano hizi kwa muda mrefu pia huchangia magonjwa kadha wa kadha kwa mujibu wa Dkt Sokwalla.
“Inaweza sababisha ‘mawe’ kwenye kibofu cha nyongo na kufura kwa kiungo hicho na hata kusababisha aina ya kansa ya tezi (medullary thyroid cancer).”
Pia, sindano hizo huongeza hatari ya kudorora kwa sehemu nyeusi ya macho (retina) haswa iwapo mgonjwa anaugua ugonjwa wa kisukari unaoathiri sehemu hiyo ya macho.
Zaidi ya hayo, Dkt Sokwalla anasema iwapo unalenga kutumia sindano hizi kupunguza uzito wako, hupaswi kutumia sindano pekee bali pia kubadilisha vyakula unavyokula na kufanya mazoezi.
Wagonjwa wenyewe hujidunga sindano hizi mara moja kwa wiki kabla muda wa saa 48 kuisha huku Dkt Sokwalla akisema ni rahisi sana kujidunga kwenye sehemu zenye mafuta kama tumbo, mapaja na hata mikono karibu na makwapa.
“Ukijidunga dawa hii zaidi ya unavyostahili, unaweza ukahisi kichefuchefu, ukatapika, ukaendesha na kupata maumivu ya tumbo haswa ukijidunga dozi ya juu kuliko kawaida,” anafafanua Dkt Sokwalla.
Mwaka jana, Bodi ya Kudhibiti Dawa na Sumu nchini (PPB), ilionya Wakenya dhidi ya matumizi ya sindano hizi za Ozempic zilizokuwa zikienea nchini, kwamba hazikuwa halali.
Kwenye taarifa yao kwa vyombo vya habari, bodi hiyo ilisema kuwa sindano hizo zilikuwa Apidra Solostar pens (glulisine) ambazo hutumika kutibu ugonjwa wa kisukari aina ya 1 na 2.
“Bodi ingependa kufahamisha umma kuwa sindano hizo za Ozempic hazijasajiliwa wala kuidhinishwa na bodi kutumika nchini. Sindano hizo zinazouzwa kama Ozempic si salama na bado haiwezi ikathibitisha usalama, ubora na ufanisi wake,” ikasema taarifa yake.