Hofu ya walimu kuhusu mishahara yao na wanafunzi Covid-19 ikizidi kuhangaisha dunia
Na GEOFFREY ANENE
HUKU wazazi wakijipata wamegeuka kuwa walimu baada ya shule kufungwa kwa ghafla kutokana na janga la virusi vya corona kisa cha tatu kilipothibitishwanchini Kenya mnamo Machi 15, walimu wanaonekana kujawa na hofu masilahi yao yataathirika vibaya katika kipindi hiki kigumu.
Leo Alhamisi idadi jumla ya visa vya maambukizi imefikia wagonjwa 31 baada ya Waziri Msaidizi wa Afya Mercy Mwangangi kutangaza visa vitatu vipya vya wanawake wa umri wa kati ya miaka 30 na 61.
Katika mahojiano na walimu kadhaa, pia walikiri watalazimika kufanya kazi ya ziada hali ya kawaida itakaporejelewa ili kutimiza malengo waliyoweka kabla ya muhula wa kwanza kuanza.
Mwalimu Meshack Ambaisi wa shule ya msingi ya St Anne Junior School Lubao katika kaunti ya Kakamega anasema alikuwa amekamilisha masomo saba kati ya 11 aliyofaa kufundisha muhula huu. “Kifedha, kipindi hiki kimeathiri vibaya mapato yangu kwa sababu sitapata chochote mwezi huu. Hali itakuwa mbaya hata zaidi tusiporejea darasani hivi karibuni.”
Ambaisi, ambaye ni mwalimu wa hisabati na sayansi, anasema alishauri wanafunzi wake wafuata agizo la serikali la kukaa nyumbani wakati huu wasije wakaambuzikwa virusi hivyo, ambavyo vimetikisa dunia nzima.
Juddy kutoka shule ya msingi ya Smart Kids Angel Academy mtaani Kariobangi South jijini Nairobi ameambia ‘Taifa Leo’ kuwa hawakuwa wamemaliza robo ya masomo ya muhula huu.
“Muhula wa kwanza unajumuisha wiki 14. Tulikuwa katika wiki ya 11 kumaanisha kuwa hatukuwa tumekamilisha robo ya masomo ya muhula huu na pia kuyapitia tena.” “Bila shaka, kipindi ambacho hatujakuwa shuleni kitaathiri pakubwa malipo yetu,” anasema mwalimu huyo wa Kiingereza na Kiswahili.
Julius Otieno kutoka shule ya upili ya Buruburu Girls anasema, “Huwa tunasomesha masomo matatu kila muhula. Tulikuwa tumekamilisha masomo mawili. Ugonjwa wa Covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona utakuwa na madhara makubwa katika kukamilisha silabasi. Itahitaji kazi ya ziada na pia ushirikiano kubwa ili kurejesha mfumo wa elimu unapofaa kuwa,” anasema.
Mwalimu huyo wa Kemia na Biolojia anasema alishauri wanafunzi wake kutumia mitandao kujinufaisha na masomo wakati huu ambapo shule zimefungwa. “Kuna mafunzo mengi kwenye mitandao ambayo itawasaidia. Mafunzo yanayotolewa na Tasisi ya Elimu nchini Kenya (KICD) kwenye redio pia itawasaidia pakubwa. Watumie muda wao vyema kwa sababu muda ni raslimali ambayo haiwezi kuongezwa,” anasema kabla ya kufichua kuwa wanafunzi wa shule hiyo walipewa kazi ya kufanyia nyumbani. “Tunawasiliana nao mara kwa mara kwa njia ya simu kujua wanavyoendea na masomo,” ameongeza.
Mwalimu wa shule za Nairobi Rabbani Group of Schools, Muchenya anasema walikuwa mbali sana katika kufikia malengo yao ya muhula wa kwanza.
“Tulifaa kukamilisha masomo manane, lakini kufikia wakati serikali ilitangaza kufunga shule, tulikuwa tumekamilisha angaa tatu hivi,” anasema Muchenya, ambaye aliongeza kuwa alishauri wanafunzi wake kutia bidii, hasa wanafunzi watakaofanya mtihani wa kitaifa baadaye mwaka 2020.
“Niliambia watahiniwa kuwa wazamie masomo yao wakisubiri mtihani wao wa mwisho.”
Kuhusu mshahara alisema: “Oooh! Mshahara wetu umeathirika na hali hii. Huenda tukapata nusu ya mshahara.”
Kevin Lugalia anayefundisha Kiingereza katika shule ya Upili ya St Anthony Kitale ni mmoja wa walimu wachache waliokuwa wamekamilisha sio tu masomo ya muhula, bali ya mwaka mzima.
“Mimi nafundisha Kiingereza katika kidato cha nne katika shule ya upili ya St Anthony Kitale. Sisi tulikuwa tumemaliza kufundisha masomo ya mwaka huu.”