Husubiri hatua ya uanguaji kuhakikisha thamani ya mayai iko juu
Na SAMMY WAWERU
MARGARET Njeri Maina amekuwa kwenye ufugaji wa kuku wa kienyeji wa kisasa maarufu kama ‘kuroilers’ kwa muda wa miaka miwili sasa.
Alianza shughuli hii 2016, baada ya kufunga duka la biashara aliyokuwa ameweka jijini Nairobi.
“Kabla ya kuanza biashara nilikuwa nimeajiriwa kama msimamizi katika shule moja Nairobi. Niliacha kazi hiyo 2010, ili kuwekeza katika biashara,” adokeza Bi Njeri.
Ilimgharimu mtaji wa Sh30,000 kufungua duka la kupiga karatasi na stakabadhi chapa.
Pia alikuwa akiandalia mashirika na kampuni muundo wa barua, mabango na stika.
“Baba alikuwa mfugaji mashuhuri wa kuku nyumbani kwetu Nyeri. Nimelelewa katika mazingira ya kuku, na ni kwa sababu hiyo nikaanza kuwafuga,” anaelezea.
Isitoshe, anasimulia kwamba hakuna kinachomtuliza moyo kama boma lake kuhinikiza kelele za kuku pamoja na kutazama wakipiga maraundi katika mazingira.
Safari ya kuafikia azma yake iligharimu Sh15, 000 pekee, alizokuwa ameweka kama akiba kupitia biashara aliyofunga. Aliunda kizimba kidogo. “Nilinunua vifaranga 100 wenye umri wa siku moja, kila mmoja nikiuziwa Sh100,” asema mfugaji huyu. Fedha zilizosalia, alizitumia kugharamia lishe, matibabu na mahitahi ibuka.
Miezi minne baadaye, kuku hao walikomaa na kuanza kutaga mayai. Kwa siku alikuwa akikusanya kreti mbili. Aidha, kreti moja ina jumla ya mayai 30.
Anasema alikuwa mtalii wa mara kwa mara kwa wafugaji waliofanikisha ufugaji wa kuku na hata kufanya utafiti katika mitandao ili kuimarisha jitihada zake.
Ili kupanua mradi wake aliousajili na kuupa jina Gratia Poultry, alinunua kiangulio cha idadi ya mayai 264, kwa Sh65,000.
Kufikia mwishoni mwa 2016, alikuwa na karibu kuku 500 wanaotaga.
Bi Njeri, mama wa watoto wawili, anasema hilo lilikuwa jaribio kuona iwapo anaweza kuongeza thamani (value addition) katika mazao ya kuku. Ndege hawa wa nyumbani wanafugwa kwa minajili ya mayai na nyama.
Katika siku za hivi karibuni wafugaji wa kuku wa mayai hapa nchini wamekuwa wakilalamikia biashara yao kuzorota kwa sababu ya kuwepo kwa mayai kutoka nchi za kigeni.
Wanadai bei ya mayai hayo ni ya chini mno, suala linalowasababishia hasara ikizingatiwa wamegharamika kulisha, kutibu na kutunza kuku.
Serikali imefungua mipaka kati ya Kenya na mataifa ya Afrika Mashariki ili kuruhusu biashara huru ya bidhaa.
Ni kutokana na hilo, kreti moja ya mayai sasa inauzwa hata chini ya Sh250 kutoka Sh350 miaka ya awali.
“Ili kuepuka kero ya kutafuta soko la mayai, niliamua kuyaongeza thamani kwa kusubiri uanguaji kupata vifaranga. Yai kwa bei ya rejareja ni Sh10, kifaranga wa siku moja ninamuuza Sh100,” afafanua.
Ili kufanikisha jitihada zake, mbali na kiangulio cha mayai 264, Njeri ameongeza vingine; cha mayai 2112, 1056 na 500.
Mfugaji huyu wa Kiambu ana zaidi ya kuku 200 wanaotaga.
Mayai huanguliwa baada ya siku 21, na anasema huhakikisha kila wiki hakosi kuuza vifaranga. Amepenyeza soko lake katika zaidi ya kaunti 10, zikiwemo Kiambu, Nairobi, Nyeri, Nyandarua na Nakuru.
Wakati wa mahojiano, alisema Machakos ndiyo mnunuzi wake mkuu.
Kaunti zingine ni Mombasa, Kisumu, Uasin-Gishu na Busia.
“Mitandao ya kijamii hasa Facebook hunisaidia kuwafikia wateja,” anasema.
Ufanisi katika ufugaji wa kuku unategemea masuala kadha wa kadha. Ujenzi wa makazi ni jambo linalopaswa kutiliwa maanani, wataalamu wa ufugaji wakishauri kuku mmoja awe na nafasi ya futi 2 kwa 2 mraba.
Usafi uwe wa hadhi ya juu ili kudhibiti usambaaji wa magonjwa na wadudu. “Hufagia makazi ya vifaranga na kuku kila siku. Vifaa vya maji na lishe lazima pia niving’arishe kabla kuwatilia,” aeleza Njeri.
Okuta Ngura, mtaalamu wa masuala ya ufugaji hasa kuku anasema ndege hawa wanapaswa kulishwa chakula chenye madini kamilifu. Kulingana na mdau huyu ni kuwa vifaranga walishwe chickmash, wanapofokisha umri wa mwezi mmoja growers na wanaotaga layers mash.
Hali kadhalika, matibabu yatiliwe mkazo. “Kuna chanjo mbalimbali za kuku, kuanzia vifaranga. Wa umri wa siku moja huchanjwa Marek. Chanjo zingine wanapoendelea kukua ni dhidi ya ugonjwa wa Newcastle, na chanjo ya Gumboro,” aeleza Bw Okuta Ngura, akihimiza umuhimu wa mfugaji kutafuta ushauri wa mtaalamu kuku wanapoonesha udhaifu.
Bi Njeri 36, anasema katika utangulizi wake kufuga kuku alipitia changamoto za kuelewa matibabu na chanjo. Hata hivyo, alihusisha wataalamu na madaktari wa mifugo waliompevusha.
Ili kudhibiti usambaaji wa magonjwa haswa kupitia makanyigio ya viatu, yeyote anayezuru Gratia Poultry sharti akanyage maji yaliyotibiwa langoni.
Anasema hajutii ufugaji anaofanya, hasa wa kuangua vifaranga, akihoji umemuinua kimaisha. “Sina presha ya kuamkia kazi, kama nilivyokuwa nimeajiriwa hususan msimu wa mvua. Nimelea watoto wangu kupitia ufugaji wa kuku,” asema.
Anahimiza wanaopania kuwekeza katika biashara hii kutoiendeshea wakiwa mbali nayo. Anasema kinachofilisha biashara nyingi ni kuzianzisha na kuachia wafanyakazi, waasisi wakisimamia kwa njia ya simu.