Makala

Huyu hapa anachakata, kupakia na kuuza asali kwa kampuni

Na PETER CHANGTOEK November 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BAADA ya kufuzu na shahada ya Usimamizi wa Hoteli katika Chuo Kikuu cha Moi, 2014, Easter Kojwang alitafuta kazi lakini hakuridhishwa na zile alizopata.

Alipata moja ambapo alihudumu kama msimamizi wa wafanyakazi katika hoteli moja na nyingine kama afisa katika idara ya mapokezi.

Hata hivyo, zote hazikumridhisha, na akaziacha.

Baada ya kuacha kazi, alitoka Nairobi na kuenda kitongojini alikozaliwa katika eneo la Lambwe Valley, Kaunti ya Homa Bay.

Akiwa kitongojini, nyanyake akawa anamtuma shambani kuvuna njugu.

Alipokuwa akivuna njugu, alikuwa akijipiga picha akiwa nazo, na kuweka katika mitandao, na wenzake waliokuwa Nairobi, wakawa wanamwambia awaletea njugu.

Kojwang akaanza kukaanga njugu hizo na kutengeneza siagi akizileta kuuza jijini Nairobi.

Asali iliyopakiwa na Eastnat Foods Limited PICHA|PETER CHANGTOEK

Biashara iliponoga mno, akaanzisha kampuni ya kuchakata njugu na kuuza asali.

Mtaji alioutumia ulikuwa wa Sh9,000.

Kampuni hiyo, iliyoanzishwa rasmi 2016, sasa imekuwa kubwa na ina wafanyakazi 10 na huuza bidhaa mbalimbali.

“Nilianza kuongeza thamani njugu na kuleta Nairobi, na hivyo ndivyo biashara yangu ilivyoanza 2015, lakini niliifanya kuwa kampuni 2016,” asema Kojwang, ambaye aliiasisi kampuni ya ya Eastnat Foods Limited 2016.

Anaongeza kuwa, wao huuza bidhaa aina mbalimbali, lakini bidhaa zao kuu ni asali inayochakatwa na kupakiwa.

“Husambaza asali kwa mikahawa na hoteli. Mikahawa mingi hapa Nairobi hutumia asali ya Eastnat. Pia nasambazqa asali kwa kampuni zinazotengeneza bidhaa, kwa watu wanaouza, na hata kwa wafanyabiashara wadogowadogo na kwa vioski,” asema Kojwang.

“Mbali na asali, nauza bidhaa nyinginezo kama vile mbegu za chia, maboga, simsim, sea mossashwagandhamukombero, habiskasi na chamomile,” afichua.

Kojwang anasema kwamba wao hununua asali kutoka kwa wakulima 3,000 na kuchakata na kuuza tani zaidi ya 6,000 kwa mwezi.

Anadokeza kwamba, hununua asali kutoka kwa wakulima walioko katika kaunti za Nandi na Baringo, na kwa wakati mwingine hununua kutoka eneo la Oloitoktok.

Easter Kojwang (kushoto) na Sarah Vivian, wakionyesha asali iliyopakiwa katika kiwanda chao kilichoko Yogi Corp, Factory Street, Industrial Area, Nairobi. PICHA|PETER CHANGTOEK

Hata hivyo, anaeleza kuwa, mabadiliko ya tabianchi huathiri uzalishaji wa asali.

Kunapokuwa na uhaba wa asali nchini, wao hununua asali kutoka nchini Uganda.

Ili kuhakikisha kuwa wananunua asali bora kutoka kwa wakulima, yeye hutumia kifaa kinachojulikana kama refractometer kupima ubora wa asali.

Kifaa hicho huonyesha kiwango cha maji kwenye asali.

Pia, wanahakikisha kwamba asali ina ladha kwa walaji.

Rangi ya asali pia hukaguliwa kwa sababu wateja mbalimbali hupenda asali yenye aina fulani ya rangi.

Mbali na kutumia refractometer na grader ya asali, wao pia hupeleka asali kwa maabara ili kukaguliwa iwapo imeafiki viwango vinavyotakiwa na Kebs.

Easter Kojwang akionyesha asali iliyopakiwa katika kiwanda chao kilichoko eneo la Industrial Area, Nairobi. PICHA|PETER CHANGTOEK

“Tuna duka katika HH Towers, ghorofa ya nane, na mahali pa wateja kuchukua bidhaa zao kule Kisumu,” anasema Kojwang.

Wao hupakia asali kwa ndoo za lita 25, ambazo huuzwa kwa Sh22,500, na aina hiyo, mara nyingi, hununuliwa na watengenezaji wa bidhaa mbalimbali.

“Tunauza kilo moja kwa Sh9,000. Lakini pia tunauza kwa bei ya jumla kwa wale wananunua kwa wingi,” asema mjasiriamali huyo.

Pia, kampuni ya Eastnat Foods Limited ina asali iliyopakiwa kwa mikebe ya kilo saba, inayouzwa kwa Sh6,300, kilo nne inayouzwa kwa Sh3,600 na kilo moja inayouzwa kwa Sh900.

Aidha, hupakia kwa nusu kilo, inayouzwa kwa Sh500.

Miongoni mwa changamoto anazosema amepitia katika biashara hiyo ni kuwa, huhitaji mtaji mwingi ili kuiendesha.

Kojwang anapania kuanza kuziuza bidhaa zake katika maduka kuu nchini na pia kuisafirisha barani Uropa na Amerika.