Akili MaliMakala

Idara ya Magereza Kenya inavyojituma kusaidia kuboresha kilimo

Na SAMMY WAWERU January 14th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA miaka ya hivi karibuni, Idara ya Magereza Kenya imekuwa ikionyesha jitihada zake kusaidia serikali kuangazia kero ya njaa na uhaba wa chakula.

Kuanzia mashamba ya mboga hadi uzalishaji wa mifugo, magereza mbalimbali nchini yamejitokeza kama washirika muhimu wa usalama wa chakula.

Taasisi hiyo, kando na kujukumika kurekebisha tabia ya wafungwa wanaohukumiwa inawasaidia kupata mafunzo kujiendeleza kimaisha, ambayo watakapokamilisha kuhudumu vifungo watayakumbatia. Kilimo, ni mojawapo ya mafunzo hayo.

Jitihada hizo, aidha, zimeashiria kuzaa matunda baada ya idara hiyo kutwaa taji la kwanza – kwenye orodha ya asasi za kiusalama, Maonyesho ya Kimataifa ya Kilimo na Kibiashara Nairobi 2025, yanayoandaliwa na Baraza la Kilimo Nchini (ASK).

 

Idara ya Magereza Kenya inajikakamua kusaida kuboresha kilimo. Pichani, Sajenti Cosmas Ayako kutoka Gereza la Lang’ata ambalo lifanya bora kwenye kilimo kwa kushirikisha mahabusu. Picha|Sammy Waweru

Kwenye hafla hiyo iliyofanyika kati ya Septemba 29 na Oktoba 5, Jamhuri Grounds, Nairobi, Idara ya Magereza iliwashangaza wengi baada ya kuibuka mshindi kwa mara ya pili mfululizo.

Ushindi huo uliashiria ukuaji wa mchango wa taasisi hiyo katika mfumo wa chakula nchini.

Kwa muda mrefu, Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) ndilo limekuwa likitawala ushindi huo kwenye maonyesho ya ASK, idara hiyo ikijulikana kwa nidhamu, na ukakamavu wake kukumbatia teknoloJia za kisasa na kibunifu kuboresha huduma za kilimo.

Hata hivyo, mwelekeo huo unaonekana kubadilika polepole, Idara ya Magereza ikijipanga kimyakimya hasa kwenye vumbuzi za kilimo na teknolojia kuhamasisha uzalishaji wa chakula nchini.

Mboga maridadi zilizokuzwa na Gereza la Wanawake la Lang’ata, Nairobi kwa kutumia mfumo wa kisasa. Picha|Sammy Waweru

Kwenye maonyesho ya ASK Nairobi mwaka huu, kivutio kikubwa hakikuwa teknolojia ya kisasa au mashine na mitambo, bali kilikuwa aina ya viazi asilia – nduma.

Idara hiyo inakuza aina mpya ya nduma inayojulikana kama Maranta, inayolimwa katika Gereza la Wanawake la Lang’ata, Nairobi.

Kiazi hicho kilitwaa nafasi bora kwenye kitengo cha mazao ya mizizi na pia kushinda tuzo ya kibanda bora, mpangilio uliomvutia Rais William Ruto alipohudhuria.

Nduma ni chakula kinachopendwa sana, hasa wakati wa kifungua kinywa.

Kiazi kikuu aina ya ndumaa kinacholimwa na Gereza la Wanawake la Lang’ata, Nairobi. Picha|Sammy Waweru

Kwa kawaida, hukua maeneo yenye maji mengi na udongo wenye unyevuunyevu, na huzalishwa sana maeneo ya Kati, Nyanza na Magharibi.

Kwa muda mrefu limeonekana kama zao lenye mipaka ya uzalishaji, lakini ujio wa Maranta umebadilisha mtazamo huo.

“Aina hii mpya ya nduma hustahimili ukame na inaweza kustawi hata katika maeneo kame na nusu-kame (ASAL),” alieleza Sajenti Cosmas Ayako, Meneja wa Shamba la Gereza la Wanawake la Lang’ata.

Aidha, gereza hilo lilianza kuikuza 2024 baada ya kufanyiwa majaribio na taasisi za utafiti nchini.

 

Sajenti Cosmas Ayako wakati wa Maonyesho ya ASK Nairobi 2025 akielezea mkulima kuhusu ndumaa mpya aina ya Maranta. Picha|Sammy Waweru

Maranta ina uwezo kuzalisha hadi kilo 30 kwa tawi moja, zao hilo likiwa mara mbili ya nduma za kawaida.

“Mbegu zake zilitolewa Afrika Kusini, na Lang’ata kuteuliwa kuwa kituo cha kuzalisha kwa ajili ya usambazaji maeneo tofauti nchini,” Ayako akaambia Akilimali.

Afisa huyo anafananisha uzalishaji wa Maranta na kuku anayetaga mayai mfululizo, akisema kila tawi linatoa matawi mengine 20.

Anafichua kuwa Gereza la Lang’ata lilianza na mbegu – matawi matano pekee, na sasa limepanua uzalishaji hadi robo ekari.

Sajenti Cosmas Ayako akionyesha nduma aina ya Maranta. Picha|Sammy Waweru

Kwenye kilimo, Ayako anadokeza kwamba kituo hicho cha urekebishaji tabia cha wanawake kimejumuisha wafungwa 250.

Tofauti na nduma ya kawaida inayochukua zaidi ya miezi sita kuanza kuzalisha, Maranta hukomaa ndani ya miezi mitatu pekee.

Kwa sasa, gereza hilo limeanza kusambaza mbegu kwa maeneo mbalimbali nchini na linahimiza wakulima kulitembelea ili kupata mbegu.

Maranta, Sajenti Ayako anaitaja kama mojawapo ya teknolojia kusaidia kuangazia kero ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ndumaa mpya aina ya Maranta inatoa mazao mengi ajabu. Picha|Sammy Waweru