• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Ifahamu ala ya muziki isiyopigwa na watu goigoi

Ifahamu ala ya muziki isiyopigwa na watu goigoi

NA KALUME KAZUNGU

MJA anaposikiliza au kupokea tumbuizo mbalimbali mara nyingi hujihisi ameburudika na kuliwazika.

Tumbuizo au muziki mara nyingi huambatanishwa au kusindikizwa na sauti za ala aina aina, ikiwemo nzumari au zumari, ngoma, marimba, filimbi, njuga, kinubi, tarumbeta, kayamba na nyinginezo nyingi.

Wanaoburudishwa hudhania kuwa ni jukumu rahisi kwa mtumbuizaji kuvipiga au kuvipuliza vifaa husika hadi kufikia kiwango cha kutoa sauti za kutumia katika muziki husika.

Ila wasichokijua ni kwamba kuna vifaa vya muziki au ala ambazo yeyote anayezipiga, kuzipuliza au kuzichanganya burudanini lazima ajikaze la sivyo zitamlemea.

Bw Omar Ali, mmoja wa wapiga nzumari maarufu kisiwani Lamu. Ala hii ya muziki huwa haipulizwi na watu goigoi bali wenye kutumia nguvu na kujituma maishani. Picha|Kalume Kazungu

Miongoni mwa ala hizo za muziki ni nzumari, pia ikifahamika kama zumari.

Zumari ni ala ya muziki ambayo huwa nyembamba mdomoni na pana upande unakotokea sauti.

Kifaa hiki cha muziki huwa na matundu kadhaa yanayoguswaguswa au kuzibwazibwa kwa awamu, hivyo kutoa au kubadilisha sauti mbalimbali.

Sifa wazi za nzumari au zumari ni kwamba watu wanaozitumia huwa ni wenye kujituma na shujaa.

Kwa mintarafu, watu goigoi au wanyonge, wavivu na wenye hulka ya utepetevu wa aina yoyote ile katu hawawezi kukitumia kifaa hiki katika kutekeleza jukumu husika la kuburudisha au kutumbuiza.

Wazee wataalamu wa muziki waliohojiwa na Taifa Leo, hasa kwenye visiwa mbalimbali vya Lamu ambapo nzumari au zumari hutumika kwa wingi walikiri kuwa watu wavivu mara nyingi wamekuwa wakikwepa kukaribia ala hiyo ya muziki wakijua fika kuwa jukumu la kuitumia kutoa sauti za tumbuizo ni zito.

Ili kuitumia nzumari, utahitajika kuzuia hewa nyingi kwanza pafuni, kujitutumua kifua na kisha kuhifadhi hewa nyingine mdomoni au mashavuni.

Mpiga nzumari au zumari tofautitofauti wa Lamu. Picha|Kalume Kazungu

Ni hewa hiyo ambayo hupulizwa kupitia kwenye kona kali kama kwa filimbi au kwa kipande cha tete inayotetema katika mwendo wa hewa.

Mashujaa wa kupuliza nzumari au zumari pia hutumia midomo kama asili ya mitetemo mfano wa vile inavyofanyika kwenye tarumbeta.

Bw Hussein Miji, mkazi wa kijiji cha Shanga kilichoko kisiwa cha Pate, Lamu Mashariki, anasema mbali na ujuzi mja anastahili kujihami nao kumwezesha kuipuliza zumari, pia kunahitajika nguvu nyingi, umahiri na mwili wenye afya.

“Kuitumia zumari au nzumari ipasavyo, ni uwe mwenye afya njema ya kimwili kwani utahitajika kutumia kiwango kikubwa cha nguvu. Pumzi ndio uhai wa mwanadamu, hivyo mwenye kuipuliza zumari mpaka awe imara. Mtu mvivu, mnyonge au goigoi hawezi kuitumia ala hii,” akasema Bw Miji.

Ikumbukwe kuwa visiwa vya Siyu, Tchundwa, Shanga na Kiunga, vyote vikipatikana Lamu Mashariki, tangu jadi vimesifika sana kwa matumizi ya zumari au nzumari kwenye miziki yao.

Ali Madi, mkazi wa Matondoni, anaitaja nzumari kuwa ala au kiungo muhimu kwa tumbuizo mbalimbali zipatikanazo Lamu.

Anaitaja nzumari kuwa miongoni mwa turathi muhimu zinazoenziwa eneo hilo.

“Twatumia nzumari kwa karibu kila ngoma au densi ya asili ya Lamu. Tupo na karibu ngoma au densi 20 tofautitofauti hapa kwetu. Utapata nzumari ikitumiwa na wacheza ngoma ya chama, Uta, Goma la Barani, Vugo, Kirumbizi nakadhalika. Ni turathi muhimu hapa Lamu,” akasema Bw Madi.

Licha ya ugumu uliopo katika kuitumia nzumari, wenye ujuzi, ushujaa na bidii ya kupuliza ala hiyo imewapatia umaarufu mkubwa na pia ajira ya ndani na nje ya Lamu.

Bw Bakari Salim, mkazi wa Siyu na shujaa katika kuitumia nzumari, anasema mara nyingi amealikwa kujumuika na wacheza densi mbalimbali za asili ya Lamu kwenye mji wa kale wa Lamu, hasa wakati wa Tamasha za Utamaduni wa Lamu, hivyo kujipatia mtaji.

“Mimi kandarasi zangu za kupuliza zumari huja msimu wa sherehe au tamasha kama vile Hafla ya Utamaduni wa Lamu, Maulidi na mengineyo. Nikitoka huku Siyu na kupiga kambi kisiwani Lamu kuhudumia kwa kupuliza hii zumari hupata kati ya Sh4000 na Sh10,000 kwa siku. Hizo ni fedha nzuri,” akasema Bw Salim.

Anasema yeye mara nyingine pia hujipata amealikwa nje ya nchi ili kutekeleza jukumu lake la kupuliza zumari.

“Iwapo nitaalikwa nje ya nchi, kama vile Tanzania, Uganda, Rwanda nakadhalika, malipo au kandarasi huwa ni tofauti. Hapa hupata malipo makubwa zaidi ikilinganishwa na utoaji huduma za papa hapa nyumbani,” akasema Bw Salim.

  • Tags

You can share this post!

DCI walivyorudi zero baada ya kukosa kuhusisha Wanigeria...

Gachagua alivyomshushia Nyoro makombora siku ya mwisho...

T L