Makala

IMANI: Si rahisi kwa dini zote kukubaliana kuhusu maadili

May 29th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na MWANGI MUIRURI

MAADILI hutajwa kama injini ambayo husukuma jamii kutenda mema na kususia maovu. Lakini kuna mjadala mkali ambao huzuka mara kwa mara ikiwa kuna ule uwiano wa kutambua yaliyo ya maadili na yasiyo.

Kasisi Mstaafu wa Kanisa Katoliki nchini Kenya, Peter Kairu anasema kuwa kuna maadili ambayo ni ya kufuatwa na wote walioumbwa, lakini kuna mengine ambayo ni ya kujadiliwa.

“Yale ambayo huongoza maisha ya binadamu, mengi huwa ni ya kufuatwa na wote walioumbwa. Kuna maadili ya kimsingi ambayo hupatikana katika amri za Mungu—kwa wale ambao huamini Mungu. Kuna mengine ambayo hufuatwa tu katika usajali wa ni wapi, ni nani na kuhusu nini,” anasema katika mahojiano na Taifa Leo Dijitali.

Anasema kuwa katika maadili ya kijamii, utapata kuwa kuna yale marufuku ya kuua.

“Lakini marufuku hayo hayafuatwi dhidi ya sheria za kuendesha jamii kwa kuwa kuna sheria za mataifa ambazo hutoa mwanya wa washukiwa sugu wa uhalifu kuuawa. Ndio sababu Kanisa Katoliki limekuwa katika mstari wambele kupinga hukumu ya kifo.

“Lakini mtu akiwa anatekeleza mauaji na kuwe na hali ya makabiliano dhidi ya mtekelezaji mauti hayo na mwaathiriwa, mtekelezaji wa mauaji aishie kulemewa na auawe, sasa hapo tutatsema maadili ya kushinikiza watu wasiuane yatakuwa yamekiukwa? Sidhani,” asema.

Anasema kuwa maadili yanaweza tu yakatajwa kuwa maadili iwapo tu kuna ule uhalisia wa mirengo inayobishana kuhusu uhalali au uharamia wa maadili wanaishi katika msimamo mmoja wa kimaisha.

“ Nasema kuwa jamii hatuna ule msimamo mmoja kuhusu lolote. Kuna wale huamini dini hii, na wengine wanafuata dini ile. Katika imani yao, wote wanajihisi kuwa na ule uhalali wa kuchukua hili na kuligeuza kuwa maadili ya kufuatwa.

“Katika ule utengano wa kiimani, utapata kuwa kunao watafuata hili na walitaje kuwa la maadili, wengine walipinge wakisema si la maadili. Kila kitu duniani ni cha kujadiliwa,” asema.

Anasema kuwa kwa Wakiristo, maadili yametolewa mwongozo katika zile Amri Kumi na maandiko ya kufafanua imani yao ndanki ya Bibilia.

‘Lakini usisahahu kuwa sio Wakiristo tu ambao wako katika ibada. Kuna dini nyingi na hata kunao ambao hata hawaamini dini. Na maadili mengine hukataa ubaguzi na utengano.

“Unaona hali kanganya hapa ambapo unatakiwa ushikilie maadili yako ambayo wewe huona ni ya haki lakini walio na maoni mengine kuhusu maadili hayo yako wapewe fursa ya kujihisi wakiwa bado na uhalali wa kimaoni kwa kuwa hawafai kutengwa au kubaguliwa?” ahoji.

Askofu Kairu anasema kuwa “wewe unafaa kufuata yako katika imani yako kwa kuwa kwa ujumla hata hakuna aliye na jibu la uhalali wa maadili na ndiyo sababu katika hukumu ya mwisho, Mungu kwa waaminiao ndiye atatuhukumu. Ndiye atatoa jibu. Na kwa hili pia kuna ugumu wa hali kwa kuwa, jibu hilo litatolewa kwa mtu binafsi wala sio kwa jumuia ya watu. Maadili ndani ya imani ni suala fiche,” asema.

Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Havard, Marc Hauser anasema kuwa unaporejelea maadili, unafaa utenganishe kama unajihusisha na mjadala wa Kisayansi, wa Kiimani au wa kijamii. Anasema kuwa hakuna uwiano utawahi kupatikana katika mjadala wa maadili kuwa na ule uwiano kwa wote.

“Wanasayansi watakupa sababu ya kuavya mimba, walio katika dini watapinga lakini mara kwa mara uwaone wakikubali kwa msingi wa kuokoa maisha nao wale walio katika jamii wakichukulia uavyaji mimba kwa imani ya kibinafsi. Hakuna aliye na ufunguo halisi kuhusu maadili ni nini,” asema.

Bw Julius Kabeu ambaye ni mwalimu katika somo la dini ya Kikiristo anasema kuwa “maadili ni imani. Maadili ni hilo wewe huamini.”

Anasema kuwa ikiwa huoni hili ni la kukufaa maishani, achana nalo.

“Ukiona linakufaa, kumbatia. Lakini hakuna yeyote aliye na uwezo wa kukwambia kuwa hili hufuatwa na wote kama maadili. Ya kwenu ni ya kwenu, ya kwetu ni ya kwetu. Jibu tutapata katika hukumu ya kimaisha.”