Makala

INDINDI: Walezi, wanataaluma wajipange kuwasilisha mawazo yao kwa BBI

February 25th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

NA HENRY INDINDI 

MCHAKATO unaoendelea wa kuchangia mabadiliko katika katiba ya taifa hili umeshika kasi tena baada ya wiki mbili za kumwomboleza aliyekuwa Rais wa awamu ya pili, hayati Mzee Daniel Toroitich arap Moi.

Wananchi na viongozi mbalimbali wanawasilisha mawazo na matamanio yao kwenye jopokazi linalosimamia mchakato huu maarufu kama BBI.

Huu ndio wakati mwafaka wa kujitokeza kwa walezi na wanataaluma wa Kiswahili kuwasilisha mawazo na mapendekezo yao kuhusu nafasi wanayoitarajia ya Kiswahili kama wanavyofanya wanasiasa na viongozi wa sehemu mbalimbali za nchi hii.

Walezi wa Kiswahili wakinyamaza sasa hakuna atakayejua ikiwa kuna uhitaji wa kukitwa kisawasawa kwa Kiswahili katika katiba yetu.

Haitoshi tu kuitaja lugha kama ya taifa bila kuiwajibisha kitaifa wala kuitaja kama rasmi bila kuiwajibisha katika urasmi huo.

Hatuwezi kuendelea kuhakiki na kutathmini mustakabali wa Kiswahili katika makongamano, tukaibuka na makala katika majarida ambayo sawa na tasnifu zilizo katika rafu za maktaba vyuoni, husomwa na wachache tena kwa nadra sana.

Tutafute nafasi ya kuwasilisha mawazo, maoni na mapendekezo yetu sasa. Wanasiasa wakipitisha mambo ya maslahi kwao, sisi na uzalendo wetu tuwe na nafasi imara ya Kiswahili kama lugha ya taifa na rasmi.

Naibu Gavana wa Nyeri Bi Caroline Karugu aliposimulia kuhusu mkutano wake wa kwanza na hayati Mzee Moi na ombi lake la utotoni la kutaka Kiswahili kiondolewe katika masomo wanayosoma, wakati wa mazishi ya Mzee, niliisikitikia hali ya Kiswahili katika taifa hili.

Alieleza kuwa alimwomba hayati Mzee Moi ombi hilo kutokana na ukweli na hali halisi kwamba hawakukutana na Kiswahili pengine isipokuwa darasani wakisoma somo la Kiswahili.

Niliwaona wazazi wake katika ombi lake ambao wanawakilisha wazazi wengi tu katika taifa hili na nikawaona walimu wengi katika ombi hilo.

Nyumbani walihimizwa kujua ama Kiingereza au Kikikuyu na shuleni vilevile kulisisitizwa Kiingereza. Hii ndiyo kadhia ambayo Kiswahili kimepitia na kinaendelea kupitia hata katika ulimwengu wa sasa.

Hii ni moja katika sababu za kuuchochea moto wa malezi ya Kiswahili. Walezi wa Kiswahili wasiyafumbie macho mambo yanayoendelea haya ya BBI. Wasipojitokeza sasa Kiswahili kitaendelea kuzikwa.

Tayari kuna atiati kuhusu nafasi hasa ya Kiswahili katika mtaala mpya wa elimu hasa katika ngazi ya juu au awamu ya pili ya shule za upili.

Si dhahiri ikiwa Kiswahili kitakuwa somo la lazima au hiari na kwa kweli yeyote anayewazia kulifanya kuwa somo la hiari sharti walezi wa Kiswahili wawe ange kumkabili.

Hatuwezi kuliruhusu hilo wakati tunapowania kuhakikisha kwamba taifa hili lina uhuru wa kisawasawa.

Walezi, wanataaluma, wataalamu na wakereketwa wa Kiswahili, muwe tayari wakati wowote maanake hivi karibuni tutatoa mwelekeo wa kuwasilisha mawazo na mapendekezo yetu kuhusu mustakabali wa Kiswahili kama lugha ya taifa na rasmi.

Mabadiliko na marekebisho yasiachiwe vipengele vya kisiasa pekee.

Nasi tusipojitokeza kuhakikisha kwamba Kiswahili kinakuwa na nafasi imara katika katiba na nyenzo nyingine za kisera, tutaamkia taifa lililouzika uzalendo wake siku moja. Tujitokeze.