Makala

Ipoa yafichua inachunguza visa 60 vya mauaji ya waandamanaji

Na NYABOGA KIAGE April 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

TAKRIBAN mwaka mmoja baada ya waandamanaji wasiopungua 60 kuuawa na maafisa wa usalama wakati wa maandamano ya kulalamikia ushuru, taasisi inayosimamia malalamishi dhidi ya polisi wanaokiuka sheria bado inaendelea na uchunguzi, huku kesi mbili pekee zikiwa mahakamani.

Miongoni mwa visa ambavyo bado vinaendelea kuchunguzwa ni mauaji ya watu tisa yaliyotokea katika majengo ya Bunge jijini Nairobi mnamo Juni 25, 2024, wakati wa maandamano dhidi ya Mswada wa Fedha.

Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) imefafanua kuwa vifo sita vilitokana na risasi na vitatu kutokana na kupigwa kwa nguvu  na kusema uchunguzi unaendelea.

Vifo vingi kati ya hivyo 60 vilitokana na risasi polisi walipokuwa wakikabiliana na waandamanaji waliokuwa wakishinikiza wabunge kukataa mswada  wa fedha 2024 uliolenga kuanzisha ushuru mkubwa.

Hata hivyo, licha ya hasira ya umma, wabunge walipitisha mswada huo siku ambayo vijana waliandamana na kuvamia Bunge, lakini baadaye Rais William Ruto alikataa kuutia saini kuwa sheria.

Kulingana na IPOA, waliouawa ndani ya Bunge mnamo Juni 25, 2024 ni: Erickson Kyalo, David Chege, Beasley Kogi, Wilson Sitati, Kelvin Odhiambo Maina, Kenneth Njiru Mwangi, Ibrahim Kamau Wanjiru, Erick Kayoni Shieni na Ernest Kanyi.

Mnamo Jumatatu usiku, IPOA ilisema kuwa: “Hadi sasa, kati ya visa 60 vya vifo vilivyosajiliwa,  imekamilisha uchunguzi wa visa 22, inaendelea kuchunguza 36, na kesi 2 ziko mahakamani.”

Taarifa hiyo ilitolewa  Shirika la Habari la BBC lilipokuwa linatarajiwa kupeperusha hewani ripoti inayowafichua maafisa wa usalama waliowapiga risasi waandamanaji katika majengo ya Bunge lakini serikali ya Kenya ililazimisha BBC kutoonyesha makala hayo.

IPOA, mamlaka ambayo ina jukumu la kuchunguza malalamishi dhidi ya polisi, kukagua vituo vya polisi na kufuatilia shughuli zao ili kuhakikisha zinazingatia sheria na katiba, ilisema kati ya uchunguzi uliokamilika, nane bado unakaguliwa.

Ilisema iko katika hatua za mwisho za kuandika ripoti kuhusu visa vinne kabla ya kupelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP), mbili vimefungwa ndani ya taasisi hiyo, nne tayari zimepelekwa kwa ODPP, na tatu zimefungwa kufuatia maagizo ya ODPP.

Kesi mbili zilizoko mahakamani kwa sasa ni za kupigwa risasi hadi kufa kwa Rex Masai na Evans Kiratu. Zote zinaendelea katika Mahakama ya Milimani.

Masai alikuwa mtu wa kwanza kuuawa kwa risasi wakati wa maandamano hayo. Alipigwa risasi katika  Moi Avenue, Nairobi. Uchunguzi kuhusu kifo chake bado unaendelea.

Afisa wa polisi Isaiah Muraguri, anayehusishwa na mauaji hayo, tayari ametoa ushahidi wake. Kamanda wa zamani wa Polisi wa Nairobi, Adamson Bungei, ambaye sasa ni Mkurugenzi wa Operesheni za Polisi, pia ametoa ushahidi.

Idadi ya visa vinavyochunguzwa ni kubwa zaidi ikilinganishwa na vile vilivyokamilika.
Wengine waliouawa na kesi zao bado zinachunguzwa ni: Brian Kimathi, Ryan Mwenda, Abdikadir Saadia, Sammy Mutisya, Brian Mwinzi, Christopher Gitonga, Timothy Karenyua na Patrick Muthoni.

Wengine ni Patrick Irungu, Juma Boidaras, Rashid Wagura, Joash Ombati, Dennis Otieno, Dennis Juma, Patrick Ameyo, Daniel Wanje, Titus Miheso, Caroline Shiramba na Reagan Ouko.

Vifo vya Austine Onyisa, Michael Kihunga, Kevin Madanga, John Nyabuto, Josephat Kingi na Benson Ouma pia bado vinaendelea kuchunguzwa.

Visa ambavyo uchunguzi wake umekamilika lakini bado unapitiwa kabla ya kuwasilishwa kwa ODPP ni za: Francis Sawe, Credo Oyaro, Kevin Ochieng, Brian Odhiambo, Brian Mike Kasaine, Daniel Kakai, Kennedy Onyango, Anthony Kimeu, Charles Owino, Shaquille Obienge, Alex Muteti na Denis Lubanga.
Faili ambazo ziko kwa ODPP baada ya kukabidhiwa na IPOA ni za mauaji ya  Tillen Odhiambo, Andrew Mwawasi, Emmanuel Tata na Anthony Mwangi.

Kesi zilizofungwa ndani ya IPOA ni pamoja na ile ya Joseph Gitau, ambaye ilielezwa kuwa majeraha aliyopata yalilingana na kuanguka kutoka kwenye gari la polisi.
Kesi zingine zilizofungwa kufuatia maagizo ya ODPP ni za: Sammy Maina, Frankline Ondwari na Lewis Msoro.

IPOA pia ilisema kuwa imesajili visa 233 vya majeraha wakati wa maandamano, ambapo 191 kati ya hivyo bado vinachunguzwa kikamilifu.

“Katika kesi zilizobaki, 42 zilifungwa ndani ya taasisi, huku 2 zikipelekwa kwa ODPP. Mamlaka pia ilibaini kuwepo kwa kutoshirikiana kwa maafisa wa polisi na mashahidi, jambo ambalo limechelewesha baadhi ya uchunguzi,” ilisema IPOA.