Ishara Arsenal itafinya Bournemouth licha ya mastaa kujeruhiwa
MABINGWA mara 13 wa Ligi Kuu ya Uingereza, Arsenal wana fursa nzuri ya kufinya wenyeji Bournemouth na kufikisha ushindi 2,000 kwenye ligi hiyo watakapovaana ugani Vitality Jumamosi, Oktoba 19, 2024 saa moja unusu.
Vijana wa kocha Mikel Arteta wanaokamata nafasi ya tatu kwa alama 17, nyuma ya viongozi Liverpool (18) na mabingwa watetezi Manchester City (17), hawajapoteza mechi katika mashindano yote 10 msimu huu.
Pia, Arsenal wameshinda nambari 13 Bournemouth mara sita mfululizo katika mashindano yote kwa jumla ya mabao 15-3.
Mara ya mwisho pande hizo zilikutana ni katika mechi ya kujiandaa kwa msimu 2024-2025 mwezi Julai wakati Arsenal walitamba 2-1 kwa njia ya penalti baada ya muda wa kawaida kutamatika 1-1 mjini Carson, California.
Msimu 2023-2024, wanabunduki wa Arsenal walimiminia Bournemouth jumla ya mabao 7-0 baada ya kuwalemea 4-0 ugani Vitality kupitia mabao ya Bukayo Saka, Ben White na penalti kutoka kwa Martin Odegaard na Kai Havertz. Vijana wa Arteta walichapa Bournemouth 3-0 ugani Emirates kupitia mabao ya Saka (penalti), Leandro Trossard na Declan Rice.
Mtihani wa Jumamosi unatarajiwa kuwa mgumu kwa Arsenal kutokana na kuwa wana wachezaji karibu 10 nyota mkekani wakiwemo Saka, Gabriel Martinelli, Thomas Partey na Odegaard.
Ni mechi ya kwanza ya Arsenal katika mfululizo wa mechi saba ndani ya siku 22.
Arsenal, ambao mara ya mwisho walishinda ligi msimu wa 2003-2004, watalimana na Shakhtar Donetsk (Oktoba 10) na Inter Milan (Novemba 6) kwenye Klabu Bingwa Ulaya na Liverpool (Oktoba 27) na Newcastle (Novemba 2) ligini na Preston North End (Oktoba 30) katika Kombe la Carabao baada ya mtihani wa Bournemouth.
Saka (Uingereza), Partey (Ghana), Martinelli (Brazil), Havertz (Ujerumani) na Jurrien Timber (Uholanzi) walikosa majukumu ya timu ya taifa majuzi kutokana na majeraha, ingawa baadhi yao huenda wakawa fiti dhidi ya Bournemouth.
Odegaard (jeraha la kifundo), Oleksandr Zinchenko (mguu), Takehiro Tomiyasu (goti) na Kieran Tierney (mguu) wako nje kabisa.
Sajili mpya Mikel Merino yumo mbioni kuanza mechi ya Arsenal kwa mara ya kwanza baada ya kutumiwa kama nguvu-mpya katika michuano miwili iliyopita.
Gabriel Jesus na Raheem Sterling huenda wakaongoza mashambulizi ya Arsenal kutokana na kuwa hawakujiunga na mataifa yao wakati wa mechi za timu za taifa.
Kocha wa Bournemouth, Andoni Iraola naye hana majeraha mengi kama Arsenal. Anatarajiwa kumkaribisha kikosini Tyler Adams, ingawa atategemea sana mchezaji matata Antoine Semenyo kutafuta magoli.
Ratiba ya EPL (Uingereza):
Oktoba 19 – Tottenham vs West Ham (2.30pm), Ipswich Town vs Everton (5.00pm), Manchester United vs Brentford (5.00pm), Fulham vs Aston Villa (5.00pm), Newcastle vs Brighton (5.00pm),
Southampton vs Leicester (5.00pm), Bournemouth vs Arsenal (7.30pm);
Oktoba 20 – Wolves vs Manchester City (4.00pm), Liverpool vs Chelsea (6.30pm); Oktoba 21 – Nottingham Forest vs Crystal Palace (10.00pm)