• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
ITIKADI NA MITAZAMO: Ushawahi kusikia eti mume anaweza kupitia uchungu wa kuzaa?

ITIKADI NA MITAZAMO: Ushawahi kusikia eti mume anaweza kupitia uchungu wa kuzaa?

Na MISHI GONGO

AGHALABU jamii zote ulimwenguni huwa na itikadi mbalimbali ambazo huwatofautisha watu wake na wa jamii zingine.

Miongoni mwa jamii za wapwani nchini Kenya kuna itikadi nyingi ambazo wengi wanaamini bila kuzifuata mwanajamii huenda akakumbwa na masaibu au hata maafa.

Kwa mfano, kwa jamii ya Wadigo mwanamwali hafai kuketi katikati ya kizingiti cha mlango. Inaaminika kufanya hivyo msichana huyo hujivunjia bahati ya kupata mume wa kumuoa.

Pia mwanamwali au mvulana aliyebalehe hawaruhusiwi kula chakula kikiwa ndani ya sufuria. Inasemekana kuwa kula ndani ya sufuria husababisha mvua kubwa siku ya harusi zao.

Itikadi au mtazomo mwingine ni kuwa mwanamke aliye na ujauzito hapaswi kumruka mumewe wanapokuwa wamelala kitandani. Wamijikenda huamini kuwa kufanya hivyo huhamisha au huhaliwisha matatizo ya ujauzito kutoka kwa mke hadi kwa mumewe. Kulingana na watu wa jamii hizo mume hupata kichefuchefu na hata kupitia uchungu wa kuzaa.

Kulingana na Mzee wa Wadigo Juma Mango, mtu aliyetenda kinyume na itikadi hizo na mitazamo hiyo hutakiwa kutoa kafara.

“Kafara huamuliwa na wazee wa jamii hiyo,” akasema Mzee Mango.

Aidha msichana ambaye hajazaa pia hafai kuketi kwa jiwe. Kuketi jiwe kwa msichana huyo kunaaminika kuwa kutamfanya kukosa kuzaa au kuzaa jiwe. Hivyo, kabla ya kuketi jiwe anapaswa kulitemea mate au kuepuka kulikalia.

Kuvaa kiatu kimoja kwa jamii ya Wamijikenda pia hakuruhusiwi. Inaaminika kuwa kufanya hivi kutasababisha – kutapelekea – mzazi wa kike wa aliyevaa kiatu hicho kukatika titi moja.

Itikadi nyingine ni binti aliye kwenye hedhi haruhusiwi kusuka nywele za watu wengine ikiaminika kuwa kufanya hivyo kutasababisha aliyesongwa kukatika nywele au kutokwa na wabisi.

Hizo ni baadhi tu ya itikadi, dhana na mitazamo katika jamii ya Wamijikenda. Japo kwa jamii nyingine itikadi hizo zinaweza kuonekana kama vichekesho, lakini kwa jamii husika zinatambulika na kuaminika.

You can share this post!

Umeme warudishwa visiwani Pate na Faza baada ya majuma...

Njaa yatisha Wakenya kuliko corona – Ripoti

adminleo