JACKY AMADEDE: Lengo ni kumfikia Patience Ozokwor
Na JOHN KIMWERE
‘MGAAGAA na upwa hali wali mkavu,’ ni methali inayohimiza binadamu asiwahi kuvunjika moyo kwenye jitihada za kutaka kutimiza malengo fulani maishani mwake.
Aidha imethibitishwa na wengi wanaozidi kushangamkia shughuli tofauti kwenye harakati za kusaka rikizi.
Kati yao ni mwigizaji wa kike, Jacqueline Amadede Enyakai maarufu Hotlips anayeamini kuwa licha ya kutopiga hatua anacho kipaji cha kufanya makubwa katika sanaa ya maigizo.
”Ingawa kufikia sasa sijafaulu kufika mbali ninapania kutinga upeo wa kimataifa katika masuala ya uigizaji,” anasema na kuongeza kuwa hakuna kisichowezekana mradi kujiamini na kutia bidii.
Anasema alianza kujituma kwenye masuala ya maigizo kama taaluma mwaka 2007 maana alianza kushiriki tangia akiwa mdogo.
Hata hivyo anasema tangia akiwa mtoto alitamani sana kuwa rubani maana shuleni alikuwa mwerevu zaidi katika masuala ya sayansi na hesabu.
Mwana dada huyu anasema angetaka zaidi kufikia kiwango cha kimataifa kama mwigizaji shupavu mzawa wa Marekani aitwaye Sharon Vonne Stone ambaye ameshiriki filamu nyingi ikiwamo kama Total Recall, Basic Instinct, Casino na Sliver kati ya zingine.
”Kusema kweli natamani sana kushiriki filamu kama mhusika mkuu ili nitambuliwe na wengi maana hata wafuasi wangu kamwe hawajawahi kuona sura yangu kwenye runinga,” anasema na kuongeza kuwa nyakati zote hupata nafasi kama mwigizaji wa ziada.
Anasema alipata motisha zaidi kushiriki uigizaji alipotazama filamu ya mzawa wa Marekani, Edward Regan Murphy iitwayo ‘Coming to America.’ Msanii huyu anajivunia kushiriki filamu kama ‘Hulaballoo,’ na ‘Varshita’ (Maisha Magic East).
Pia ameshiriki filamu kama ‘Pendo,’ ‘Tamani one to one,’ ‘The Launch,’ ‘Ulafi,’ ‘Disability Court,’ na ‘Struk in the middle,’ kati ya zingine.
”Ingawa bado sijapiga hatua najivunia kufanya kazi na kampuni kadhaa katika masuala ya uigizaji ikiwamo Zuia Theatre na Loreal Production kati ya zingine,” alisema mwigizaji huyu mwenye umri wa miaka 46 anayefanya kazi na Badilisha Production.
Kwa filamu Nollywood anataka kufanya kazi na waigizaji mahiri kama Mercy Johnson na Patience Ozokwor Maarufu Mama G kati ya wengine.
Kwa wasanii wa hapa Kenya anasema anatamani sana kushirikiana na wenzake kama Sanaipe Tande na Lupita Amondi Nyong’o anayezidi kutesa kwenye filamu za Hollywood.
PANDASHUKA
Dada huyu anasema amepitia changamoto nyingi tu ikiwamo kunyimwa nafasi ya kuigiza kutokana na sababu zisizona msingi.
”Nyakati zingine hukutana na maprodusa wakorofi ambao huwa vigumu kufanya kazi nao,” alisema na kuongeza kuwa suala ya mapendeleo linazidi kubomoa tasnia ya uigizaji ambayo hutawala miongoni mwa waigizaji waliotangulia.
Dada huyu siyo mchoyo wa mawaidha. Anahimiza wenzake kwamba wanastahili kujiepusha na mahusiano ya kimapenzi dhidi ya waigizaji wenzao maana suala hilo huwashusha hadhi wanawake.
Anadokeza kwamba mahusiano sapuli hiyo hatimaye huambulia patupu maana wanaume husepa huku wanawake wakiachwa kwa mataa.
Kadhalika anasema malipo duni ama kutolipwa kabisa hufanya baadhi ya waigizaji chipukizi kuvunjika moyo na kuzipigia chini shughuli za maigizo.
Hata hivyo anashauri wenzake kutovunjika moyo upesi licha ya kukutana na pandashuka nyingi katika tasnia ya uigizaji.