JAMVI: Atwoli amepiga jeki azma ya Joho kuingia Ikulu lakini…
KALUME KAZUNGU na CHARLES WASONGA
SAFARI ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho ya kuelekea Ikulu 2022 imeonekana kupigwa jeki na Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli baada ya viongozi hao kushiriki jukwaa moja hivi majuzi.
Ilikuwa ni katika hafla ya kuchanga fedha za kusaidia makundi ya akina mama katika kaunti ya Lamu iliyofanyika katika eneo la Mkunguni ambao pia ulihudhuriwa na wanasiasa kutoka mirengo Jubilee na upinzani.
Kilichojitokeza wazi wakati wa mkutano huo ni imani kubwa ambayo katibu huyo kiongozi huyo wa COTU amejenga kwa Gavana Joho anafahamika maeneo ya pwani kama, ‘Sultan’.
Wakati wa hotuba yake Bw Atwoli alimtangaza hadharani Gavana Joho kuwa mfalme wa siasa za Pwani ambaye anatosha kurithi vigogo wa zamani wa siasa za pwani marehemu Ronald Ngala, Sharif Nassir na Karisa Maitha.
Kiongozi huyo wa wafanyakazi pia aliahidi kwamba yuko tayari kuendeleza kampeni kabambe kote nchini, ikiwemo Magharibi mwa Kenya, kwa lengo la kuhakikisha Joho anakuwa miongoni mwa viongozi watakaounda serikali ijayo.
“Nina imani kuwa kwa sifa za uongozi wa Gavana Joho. Kusema kweli tangu vigogo kisiasa wa eneo hili la pwani, kama vile Ronald Ngala na Sharif Nassir kufariki, Mungu wetu hajalala. Hii ndiyo sababu sasa Mungu amewapa Wapwani huyu kijana. Nawasihi mumuunge mkono kwa sababu najua anatosha,” akasema Bw Atwoli.
Ni katika hafla hiyo ambapo Bw Atwoli alitoa kauli tata kwamba Naibu Rais William Ruto hataingia Ikulu mnamo 2022, tamko ambalo limewakera wafuasi wa mwanasiasa huyo maarufu kama “Team Tanga Tanga”
“Miongoni mwa wale wote mtakaowachagua, nataka kuwaambia kuwa jina la William Samoei Ruto halitakuwepo. Hayo sio maneno yangu lakini ya muumba wa mbingu na ardhi,” akasema.
Dkt Ruto na wanasiasa wandani wake walimshutumu Bw Atwoli kwa matamshi hayo wakidai yeye ni mganga ambaye anapanga kumwangamiza naibu huyo wa rais kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria harambee hiyo ya Lamu ni; wabunge wawakilishi wa kaunti, Ruweidha Obbo (Lamu, Jubilee), Asha Hussein (Mombasa, ODM), Elsie Muhanda (ANC), Cathrine Wambilinga (Bungoma, ANC), na wabunge Mishi Mboko (Likoni), Eva Obara (Kasipul Kabondo) na Godfrey Osotsi (Maalum, ANC). Pia alikuwa Spika wa Bunge la Nairobi aliyesimamishwa kazi Bi Beatrica Elachi.
Kila mmoja aliyehutubu alimpigia debe Bw Joho akimhimiza kutolegeza kamba katika azma yake ya kuwania urais 2022.
“Tunataka uingie Ikulu ili ukomboe si tu pwani bali taifa nzima kutokana na maovu kama vile ufisadi na utawala mbaya,” akasema Bi Mboko.
Akihutubu, Gavana Joho alidhihirisha wazi kwamba urafiki kati yake na Bw Atwoli unalenga kumwezesha kutimiza ndoto yake ya kuingia Ikulu 2022.
“Mzee Atwoli ni mzee mwenye busara, mwadilifu na anayeitakia taifa hili mema. Ni furaha yangu kwamba ameahidi kunishika mkono na kuzunguka nami kote nchini ikiwemo ngome yake ya magharibi mwa Kenya katika safari yangu ya kuikomboa nchi hii mnamo 2022,” akasema Bw Joho.
Wachanganuzi wa siasa waliohojiwa na Taifa Jumapili eneo la Lamu sasa wanaungama kuwa urafiki wa Joho na Atwoli kuwa wenye misingi ya kumkuza Joho na kumtayarisha kwa kinyang’anyiro cha urais ifikapo 2022.
Wanasema hatua ya Bw Atwoli kuahidi kuunga mkono azma Bw Joho ili kutimiza azma ya kuunda serikali ijayo ni kigezo muhimu ambacho kitarahisisha kampeni za urais za gavana ambaye pia ni naibu kiongozi wa ODM.
“Atwoli tayari yuko na wafuasi wengi karibu katika kila kaunti. Ikiwa urafiki kati yake na Joho utadumu basi atachukuliwa kuwa mwiba mkuu kwa Naibu wa Rais William Ruto katika kampeni zijazo za urais,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Alawi Abdalla.
“Ikiwa Joho ataelewana na vigogo wengine wa pwani kama vile mwenzake gavana Amason Kingi basi ukaribu wake na Atwoli pamoja na kiongozi wake Raila Odinga utamweka kifua mbele katika kinyang’anyiro cha urais 2022,” anaongeza.
Kwa upande wake, Bw Mohamed Sheyumbe anasema kuwa ujasiri wa Bw Joho katika kukemea maovu serikalini, likiwemo kero la ufisadi ni sifa ambayo itamwezesha kupata uungwaji mkono miongoni mwa Wakenya kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Lakini Bw Martin Andati ana kauli tofauti na Mbw Alawi Abdalla na Mohamed Sheyumbe.
Kulingana na mchanganuzi huyu bado ni mapema kubaini ikiwa safari ya Bw Joho ya kuingia Ikulu itafanikiwa au la kwani Bw Odinga ambaye ni kiongozi wa chama chake cha ODM hajatangaza wazi ikiwa atawania urais 2022 au la.
“Kupata uungwaji mkono kutoka kwa Bw Atwoli haipasi kuchukuliwa kuwa sababu kuu ya kudai kuwa barabara ya Joho ya kwenye Ikulu imenyooka. Mwelekeo kuhusu azma ya gavana huyu wa Mombasa kuwania urais 2022 utatolewa na Raila,” anasema Bw Andati.
Kufikia sasa Bw Odinga ambaye anashirikiana na Rais Uhuru Kenyatta kupalilia umoja wa kitaifa nchini baada ya kuridhiani kisiasa mwaka jana, hajatangaza waziwazi ikiwa atawania urais 2022 au la.
Hata hivyo, Naibu Rais Dkt Ruto na wandani wake wanaamini kuwa Bw Odinga anatumia muafaka kati yake ni Rais Kenyatta kujisuka kisiasa kwa ajili ya kushiriki kinyang’anyiro cha urais 2022.
Ukuruba kati ya Gavana Joho na Bw Atwoli pia inasemekana kuwa huenda usimfaidi mwanasiasa huyo wa pwani katika juhudi zake za kusaka kura magharibi mwa Kenya ikizingatiwa kuwa vigogo kadhaa wa kisiasa kutoka eneo hilo wametangaza nia ya kuwania urais 2022.
Wao ni kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya na Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.
Mnamo 2017, Bw Atwoli alimtawaza Bw Mudavadi kuwa msemaji wa jamii ya Waluhya ana anayepasa kuungwa mkono na watu wa jamii katika kinyang’anyiro cha urais. Lakini baadaye Bw Mudavadi aliamua kumuunga mkono Bw Odinga chini ya mwavuli wa muungano wa NASA.