MakalaSiasa

JAMVI: Chebukati hatarini kusombwa na mawimbi ya mageuzi

December 1st, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na LEONARD ONYANGO

MAPENDEKEZO ya jopo la BBI ya kutaka makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) waondoke huenda yakatatiza shughuli ya kutathmini mipaka ya maeneobunge iliyofaa kungóa nanga mwaka ujao.

Ripoti ya BBI iliyozinduliwa rasmi na Rais Uhuru Kenyatta na kinara wa ODM Raila Odinga katika ukumbi wa Bomas, Nairobi, Jumatano, inasema kuwa Wakenya hawana imani na tume ya IEBC hivyo kuna haja ya kuteua makamishna wapya watakaosimamia Uchaguzi Mkuu wa 2022.

“Kulingana na maoni tuliyopokea, ni bayana kwamba Wakenya hawana imani na tume ya IEBC. Ili kuhakikisha kwamba Wakenya wanakuwa na imani na taasisi hiyo, kuna haja ya kuwa na makamishna wapya watakaoendesha uchaguzi ujao,” inasema ripoti hiyo.

Ikiwa ripoti hiyo itatekelezwa kikamilifu, vyama vya kisiasa vitakuwa na usemi katika uteuzi wa makamishna wa IEBC.

“Katika uteuzi wa makamishna, viongozi wa vyama vya kisiasa vilivyo na wabunge wawe na jukumu la kuteua watu wasioegemea chama chochote,” inasema ripoti.

Tume ya IEBC sasa ina makamishna watatu; Wafula Chebukati (mwenyekiti) na makamishna Abdi Guliye na Boaya Molu.

Hii ilikuwa baada ya makamishna wengine wanne kujiuzulu.Roselyn Akombe alijiuzulu mnamo Oktoba 2017 akidai kuwa alitishiwa maisha.

Mnamo Aprili, mwaka jana, makamishna wengine watatu; Paul Kurgat, Margaret Mwachanya na aliyekuwa naibu mwenyekiti Consolata Nkatha walijiuzulu kutokana na madai kwamba Bw Chebukati alishindwa kuongoza.

Kufikia sasa nafasi za wanne hao hazijajazwa na Rais Kenyatta hajawahi kuthibitisha ikiwa alipokea barua za kujiuzulu kutoka kwa makamishna hao au la.

Ripoti ya BBI inapendekeza kuwa mwenyekiti wa IEBC si lazima awe wakili kama ilivyo sasa.“Mtu yeyote aliyewahi kushikilia wadhifa wa juu katika masuala ya usimamizi anafaa kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa IEBC.

Wadhifa huo usiachiwe mawakili pekee,” inasema ripoti.Wafanyakazi wote wa IEBC wataajiriwa kwa kandarasi ya miaka mitatu na wanaweza kuhudumu kwa miaka mingine mitatu na kisha kuondoka afisini.

Bw Chebukati hata hivyo, amejitokeza na kusema kuwa atangátuka afisini baada ya kukamilisha muhula wake 2023.

Hiyo inamaanisha kwamba Bw Chebukati atasimamia Uchaguzi Mkuu ujao wa 2022.Bw Chebukati, aliyekuwa akizungumza Alhamisi jijini Nairobi, alipuuzilia mbali mapendekezo ya jopo la BBI ya kutaka tume ya IEBC ivunjiliwe mbali.

‘Tuliingia afisini mnamo 2017 na muhula wetu utakamilika Januari 2023 hivyo sina wasiwasi wowote,” akasema Bw Chebukati.

Kauli hiyo ya Bw Chebukati huenda ikazua uhasama baina yake na wanasiasa wanaounga mkono muafaka wa kisiasa, almaarufu handisheki, baina ya Rais Kenyatta na Bw Odinga ambao wamekumbatia ripoti ya BBI.

Tume ya IEBC ilikuwa ikingojea matokeo ya sensa yaliyotolewa mwezi uliopita, kuanza shughuli ya kurekebisha mpaka 2020.

Shughuli ya kutathmini mipaka inafaa kukamilika kabla ya Agosti 2021.Katiba inataka shughuli ya kutathmini mipaka itamatike mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu.

Kulingana na Katiba, ni sharti kuwe na maeneobunge 290 lakini mipaka ya maeneobunge hayo inafaa kurekebisha kwa kuzingatia idadi ya watu.

Wadadisi wanasema kuwa Bw Chebukati pamoja na wenzake, wanafaa kujiandaa kukabiliana na mawimbi makali ya kisiasa haswa ikizingatiwa kwamba hakuna mwenyekiti wa IEBC ambaye amewahi kukamilisha muhula wake tangu 2007.

Mvutano wa kisiasa kati ya Bw Chebukati na wanasiasa huenda ukalemaza shughuli ya kutathmini mipaka.

Mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 uliozua ghasia zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,000, bunge lilivunja Tume ya Uchaguzi (ECK) iliyoongozwa na marehemu Samuel Kivuitu.

Juhudi za Kivuitu kwenda mahakamani kutaka kusimamisha hatua hiyo ya mahakama ziliambulia patupu.

Kivuitu aliyejizolea sifa tele kwa kuongoza uchaguzi mkuu wa 2002 na kura ya maamuzi ya 2005 kwa njia huru na haki, alidai kuwa bunge lilivunjilia mbali ECK bila kufuata sheria.

Masaibu sawa na hayo yalimkumba Isaack Hassan aliyengólewa afisini 2016 kabla ya kukamilisha muhula wale.

Bw Hassan pamoja na makamishna wake; Simiyu Wasike, Winnie Guchu, Yusuf Nzibo, Davis Chirchir, Douglas Mwashigadi, Hamara Ibrahim Adan, Ken Nyaundi na Tiyah Galgalo wakiingia afisini mnamo Novemba 2011 na kuondoka miaka mitano baadaye kufuatia maandamano makali yaliyoongozwa na Bw Odinga.

Bw Chebukati pia huenda akafuata mkondo wa watangulizi wake kwa kuondoka afisini kabla ya uchaguzi wa 2022.