JAMVI: Gavana Mutua amnyemelea Raila kujenga umaarufu akilenga Urais
Na BENSON MATHEKA
Gavana wa Machakos na kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap, Dkt Alfred Mutua, ameamua kumnyemelea kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga katika juhudi zake za kujijenga kisiasa kipindi chake cha pili kikielekea ukingoni.
Dkt Mutua ni mmoja wa magavana wanaohudumu kipindi cha pili na cha mwisho ambao wametangaza kuwania urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 na hivi majuzi alikutana na Bw Odinga katika kile ambacho wachanganuzi wanasema ni kujenga umaarufu wake.
Baada ya mkutano huo, Dkt Mutua, mtaalamu wa mawasiliano na mnenaji shupavu, alisema walijadili uchaguzi mkuu wa 2022 miongoni mwa masuala mengine ya umuhimu wa kitaifa.
Bw Odinga hakuzungumza baada ya mkutano wao au kuandika chochote katika jukwaa zake za mitandao ya kijamii japo Bw Mutua alipakia zaidi ya picha 14 kwenye anwani yake ya Twitter pekee.
Wadadisi wanasema kuwa kukutana na Bw Odinga, Dkt Mutua alitaka kutoa ishara kwamba yuko tayari kwa siasa za kitaifa baada ya kuhudumu kama gavana kwa vipindi viwili na kwamba anakumbatia muafaka kati ya waziri mkuu huyo wa zamani na Rais Kenyatta.
Dkt Mutua amekuwa kwenye vita vya ubabe wa kisiasa eneo la Ukambani na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka, ambaye alikuwa mgombeamwenza wa Bw Odinga kwenye uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017.
Ameungana na magavana wengine kutoka eneo la Ukambani kumpiga vita Bw Musyoka ambaye amekumbatia handisheki.
Gavana huyo ambaye aliongoza chama chake cha Maendeleo Chap Chap kumuunga Rais Uhuru Kenyatta alipata pigo baada ya Bw Musyoka kukumbatia handisheki na kutangaza kuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta.
“Kwa kukutana na Bw Odinga, Dkt Mutua analenga kubadilisha mbinu zake za kisiasa baada ya kugundua kuwa hangembandua Bw Musyoka kama msemaji wa jamii ya Wakamba. Aidha, alitaka kuzika tofauti zake na kiongozi huyo wa chama cha ODM ili amsaidie kumpiku Bw Musyoka kwa umaarufu Ukambani,” alisema mdadisi wa siasa, Joseph Kiilu.
Anasema kwamba uhusiano wao uliingia doa tangu enzi za serikali ya muungano wa kitaifa Odinga alipokuwa waziri mkuu naye Dkt Mutua akiwa msemaji wa serikali.
“Wakati huo, Bw Odinga alikuwa akimlaumu Dkt Mutua kwa kutumiwa na mrengo wa mshirika wake serikalini Rais Uhuru Kenyatta kumhujumu,” alisema.
Kwenye uchaguzi wa 2013, Dkt Mutua alichaguliwa kwa tiketi ya chama cha Wiper kilichokuwa kwenye muungano wa Cord ulioshirikisha ODM cha Bw Odinga. Hata hivyo, alitofautiana na muungano huo na kuunda chama chake cha Maendeleo Chap Chap ambacho alitumia kwenye uchaguzi wa 2017.
Kulingana na Bw Kiilu, kwa kukutana na Bw Odinga, Dkt Mutua alilenga kujitafutia umaarufu. “ Anaelewa kwamba mazingira ya kisiasa yamebadilika baada ya handisheki. Anajua kwamba yataendelea kubadilika na miungano mipya ya kisiasa kuibuka na hataki kuachwa nyuma,” asema.
Anasema moja ya mbinu ambayo gavana huyo anatumia ni kumualika Bw Odinga kufanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo kaunti ya Machakos.
“Dkt Mutua anataka kutumia ziara hiyo kujijenga kisiasa. Analenga sifa kwa kumkumbatia Bw Odinga akiidhinisha miradi ya maendeleo ambayo serikali yake imeanzisha. Kwa kufanya hivi analenga kumpiga kumbo Bw Musyoka ambaye amekuwa akimlaumu kwa kutoanzisha miradi ya maendeleo eneo la Ukambani,” asema.
Baada ya mkutano huo, Bw Odinga hakutoa kauli yoyote lakini msemaji wake Dennis Onyango alisema viongozi hao walibadilishana maoni kuhusu masuala kadhaa muhimu ya kitaifa hasa handisheki na vita dhidi ya ufisadi.
Kulingana na Bw Onyango, Bw Odinga pia alikubali mwaliko wa Dkt Mutua kufanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo kaunti ya Machakos hivi karibuni.
Wadadisi wanasema Dkt Mutua anataka kutumia ziara hiyo kujipiga jeki katika juhudi zake za kutaka kuwa msemaji wa jamii ya Wakamba na katika azima yake ya kugombea urais.
Kulingana na Dkt Mutua, amekuwa akimtambua na kumheshimu Bw Odinga licha ya kuwa na misimamo tofauti ya kisiasa.
Wadadisi wanasema kwamba kukosa kuhutubia kikao cha pamoja baada ya mkutano wao, kuliacha wengi na maswali.
“Ni kawaida ya Bw Odinga kutoa taarifa rasmi au kuhutubia kikao cha pamoja na viongozi wanaomtembelea au kupakia picha kwenye anwani zake rasmi za mitandao ya kijamii na ya chama chake cha ODM. Hata hivyo, hakufanya hivyo alipokutana na Dkt Mutua. Hii inafaa kumuacha Dkt Mutua na maswali,” asema Newton Syanda, mdadisi wa siasa.
Kulingana na mchanganuzi huyo, huenda Raila hakutaka watu kusawiri ziara hiyo kama ya kumtema mshirika wake wa kisiasa Kalonzo Musyoka ambaye ni hasimu wa kisiasa wa Dkt Mutua.