JAMVI: Hatari ya mwafaka wa Uhuru na Raila kuvunjika
Na BENSON MATHEKA
RAIS Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, wanafaa kudumisha mwafaka wao ili nchi isitumbukie kwenye ghasia ukivunjika.
Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Herman Manyora ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Nairobi anasema kwamba kuvunjika kwa mwafaka huo kunaweza kurejesha ghasia nchini.
“Iwapo mwafaka huo utavunjika, ninabashiri ghasia. Kinyume na wengi wanavyofikiri, hasira ya wafuasi wa NASA inaweza kuchipuka upya na kwa haraka,” alisema Bw Manyora kwenye maoni yaliyochapishwa katika tovuti ya gazeti moja nchini.
Kulingana na Bw Manyora, wafuasi wengi wa upinzani hawana imani mwafaka kati ya Rais Kenyatta na Bw Raila. “Kwa hivyo, kiwango cha ghasia na hasira zizoweza kuthibitiwa kinaweza kurudi moja kwa moja,” alisema.
Mchanganuzi huyo anasema ni hatua ya Bw Odinga, kusalimiana na Rais Uhuru iliyofanya nchi kurejea katika utulivu. “ Iwapo Uhuru anaweza kusaliti kusalimiana kwao, kwa sababu ndiye aliye na nguvu za kufanya hivyo, Raila atapungukiwa na nguvu kisiasa,” anasema Bw Manyora.
Hata hivyo, anaeleza kuwa ni rahisi kwa Raila kubuni mikakati mipya na kurejea kwa nguvu katika uga wa siasa. “ Tatizo ni akiamua kuachana na siasa, kutakuwa na shida,” anasema.
“Bila kinara wa kuongoza upinzani, hasa vijana, kinara wa kuelekeza na kutuliza hasira, ghasia haziepukiki,” anaeleza.
Kwa hivyo, anaeleza, ni lazima tujitolee kwa kila hali kufanikisha mwafaka huu kwa sababu usipokuwepo, ni hatari. Kuna dhoruba za hasira katika nchi hii, dhidi ya utawala wa Jubilee, dhidi ya (Rais) Uhuru Kenyatta.
Tunahitaji kiongozi anayeweza kutuliza hasira hizo, hasira zikikosa kuthibitiwa, nchi hii inaweza kubadilika kuwa kitu tofauti,” anasema.
Anatoa mfano wa Jamhuri ya Afrika ya Kati ambayo imevurugika kwa sababu ya vita vya ndani kwa ndani vilivyosababishwa na tofauti za kisiasa. Nchi hiyo ni moja ya zile masikini ulimwenguni.
Bw Manyora anakumbusha Wakenya kwamba kusalimiana kwa Rais Kenyatta na Bw Raila kulirejesha amani mara moja nchini.
“Mara tu waliposalimiana, amani ilirejea, biashara zikanawiri na upinzani ukamtambua Uhuru Kenyatta kama rais wa Kenya. Haya yote yanaweza kuwa hatarini mwafaka huo ukivunjika,” alionya.
Anaeleza kwamba kuvunjika kwa mwafaka huo kunaweza kuathiri pande zote mbili. “ Baadhi wanasema sifa na maisha ya kisiasa ya Bw Raila yataharibika kiasi cha kutorekebika.
Wanasema alivunja uhusiano wake na wenzake katika upinzani alipowatenga. Lakini pia Jubilee itakuwa na wakati mgumu kurejesha imani yake kwa wafuasi iwapo mwafaka utafeli,” anaeleza