MakalaSiasa

JAMVI: Hofu kubwa uyatima wa kisiasa utalikumba eneo la Mlima Kenya

April 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

KIMYA cha Rais Uhuru Kenyatta kuhusu malumbano ya siasa za urithi wake zinazoendelea katika eneo la Mlima Kenya kimebuni dhana ya uyatima wa kisiasa katika ukanda huo, licha yake kuwa uongozini.

Licha ya viongozi mbalimbali wa kisiasa kugawanyika katika makundi matatu yanayong’ang’ania urithi wake, Rais amebaki kimya, akishikilia kuwa hatajiingiza katika siasa za kikanda.

Baadhi ya wachanganuzi wanaonya kuwa wakazi wengi wameanza kuhofia hali ya uyatima wa kisiasa, ikiwa Bw Kenyatta ataendelea kubaki kimya, hasa wanasiasa wa mirengo ya ‘Team Tanga Tanga’ na ‘Kieleweke’ yanapoendelea kulumbana kuhusu urithi wake.

Wachanganuzi wanaeleza kuwa kimya hicho kimebuni dhana kuwa ameshindwa kuzima siasa hizo, hali ambayo huenda ikampotezea umaarufu miongoni mwa wakazi.

“Rais Kenyatta anaonekana kushindwa kukabili mawimbi na mikwaruzano ya kisiasa inayoendelezwa kuhusu urithi wake. Agizo lake kwa viongozi hao kukomesha siasa za urithi limekaidiwa kabisa, hali ambayo imeibua hofu kuwa ameshindwa kudhihirisha mamlaka yake,” asema Waweru Gatonye, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Kulingana na Bw Gatonye, hali hiyo ni hatari kwa Rais Kenyatta, kwani licha ya kuwa anahudumu katika muhula wa pili, usemi wake kuhusu mustakabali wa siasa za eneo hilo bado ni muhimu.

“Ni muhimu Rais Kenyatta kuonekana kudhibiti mkondo wa kisiasa ili kudumisha ushawiashi wake, hasa ielekeapo 2022. Licha ya kuwa rais, anahitajika kuzua taswira ya kuwa kiongozi anayetumia mamlaka yake,” asema Bw Gatonye.

Kando na malumbano ya viongozi wa ‘Tanga Tanga’ na ‘Kieleweke’, ziara nyingi za Naibu Rais William Ruto katika ukanda huo pia zimelaumiwa kwa kupunguza umaarufu wa Bw Kenyatta.

Wachanganuzi wanaeleza kuwa, ingawa Dkt Ruto amekuwa akitumia jukwaa la kuwa “msaidizi wa Bw Kenyatta” katika ziara zake, kutokuwepo kwake ndiko kumewafanya baadhi ya viongozi kutangaza watamuunga mkono kwenye nia ya kuwania urais mnamo 2022.

Wanaeleza kuwa ni vyema kwa Rais Kenyatta angaa kuonekana mara kwa mara, ili kudumisha uthabiti wa kisiasa katika ukanda huo, kinyume na ilivyo sasa.

“Malumbano ya ‘Kieleweke’ na ‘Tanga Tanga’ yameifanya Mlima Kenya kuonekana kama nyumba isiyo na baba mzazi. Vilevile, yamelifanya kupoteza dira yake ya kisiasa. Ni wakati Rais Kenyatta aingilie kati ili kuzima mkanganyiko huo,” asema Prof Macharia Munene, ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha USIU.

Kulingana na Prof Munene, Dkt Ruto ameibukia kuwa maarufu kwani viongozi na wakazi wengi wanamwona kama “mshirika wao ambaye yu karibu nao kila wakati.”

Asema kuwa kuwa licha ya majukumu mengi aliyo nayo, kuna haja ya Rais Kenyatta kufanya ziara za mara kwa mara katika eneo hilo, na ili kudhihirisha kuwa bado angali anadhibiti nafasi yake kama kiongozi wa kisiasa wa jamii za Agikuyu, Aembu na Ameru (GEMA).

Mara ya mwisho ambapo Rais Kenyatta alizuru eneo la Kati ilikuwa mnamo Desemba, katika Kaunti ya Kiambu, ziara ambayo ililaumiwa pakubwa kwa kutopangwa vizuri.

Viongozi wa kaunti hiyo walilaumiwa kwa kutowasilisha maslahi ya wakazi, licha ya Rais kuwatengea muda wa kutosha kuwa naye.

Viongozi hao, ambao waliongozwa na Gavana Ferdinard Waititu, Mwakilishi wa Wanawake Gathoni wa Muchomba katu ya wengine walilaumiwa kwa kumpeleka Rais katika kituo cha kuwarekebishia tabia waraibu wa ulevi badala ya kumwelekza mahitaji ya wakazi.

Hata hivyo, Bw Waititu alijitetea vikali, akisema kuwa walimweleza Rais mahitaji yote ya kaunti hiyo.

“Kuna watu wanaotulaumu kwa tuhuma za kutomwasilishia Rais mahitaji ya wakazi wa Kiambu. Hata hivyo, hawafahamu tuliyojadili. Rais mwenyewe ana ufahamu mkubwa wa maslahi yetu kwani binafsi anatoka katika kaunti hii,” akasema Bw Waititu.

Viongozi wa Mlima Kenya pia wamekuwa wakilalamika kuwa ni vigumu kumpata Rais Kenyatta, hali ambayo imewafanya wengi wao kuegemea upande wa Dkt Ruto.

Kulingana na mbunge mmoja ambaye hakukata kutajwa, ugumu wa kumpata Bw Kenyatta ndio umezua migawanyiko ya kisiasa na ukaidi wa maagizo ambayo anatoa kwa viongozi kukomesha kampeni.

“Dkt Ruto yuko hupatikana kwa urahisi ikilinganishwa na Rais Kenyatta. Kuna taratibu nyingi sana ambazo mtu huhitajika kufuata ili kumfikia. Mara nyingi huwa hapatikani,” akasema mbunge huyo.

Kutokana na hayo, wachanganuzi wanaonya kuwa mkondo huo ni hatari kwa Rais Kenyatta, kwani huenda ukazidisha uasi dhidi yake, kiasi kwamba itakuwa vigumu kwake kutoa maamuzi muhimu mnamo 2022.

“Rais lazima afahamu kuwa bado anatazamwa kuhusu maamuzi ya kisiasa ambayo Mlima Kenya itazingatia mnamo 2022. Hivyo, lazima ajaze pengo la kisiasa lililopo ili kuzima uasi unaoendelea dhidi yake,” asema Oscar Plato, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.