MakalaSiasa

JAMVI: Ishara Uhuru ameshindwa kudhibiti uasi katika ngome yake

June 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 3

Na WANDERI KAMAU

ONYO kali la Rais Uhuru Kenyatta kwa kundi la ‘Tanga Tanga’ mnamo Jumapili dhidi ya kuendesha kampeni za mapema za 2022, limeibua maswali ya ikiwa ameshindwa kudhibiti kisisasa ngome yake ya Mlima Kenya.

Duru zinasema kuwa Rais Kenyatta hakuwa amealikwa rasmi katika kikao cha wafuasi wa dini ya Akorino katika uwanja wa Kasarani, Nairobi, lakini “alivamia” mkutano huo, ilipoibuka kuwa wabunge wa mrengo wa ‘Tanga Tanga’ walikuwepo.

Ni baada ya hapo, ambapo alionyesha hasira kali, akiwaonya wabunge hao kwa kutumia lugha ya Gikuyu.

“Thaakirai biu, no ngamugiira nginya kuria guothe muri. Nii ndiri kihii kianyu muuthaakagire uria muukwenda,” akafoka rais kwa hasira: (Nichezeeni tu. Nitawatoa hata kule huwa mnaenda. Mimi si mvulana wenu muwe mkinichezea mtakavyo).

Tukio hilo limezua hisia mbalimbali, huku wachanganuzi na viongozi wakisema hasira za Rais ni dalili ya kushindwa kudhibiti uasi ambao umekuwa ukimkabili katika ukanda wa Mlima Kenya, ambapo viongozi wengi wamekuwa wakimlaumu kwa kulitenga kimaendeleo na kisiasa.

Wakili Ndegwa Njiru, ambaye ni mchanganuzi wa siasa, anafananisha hasira ya Rais na “baba aliyeshindwa kuwadhibiti watoto wake” akishikilia kuwa ndiye wa kujilaumu kutokana na migawanyiko ya kisiasa iliyo katika ukanda huo.

“Rais hana yeyote wa kulaumu, mbali yeye mwenyewe. Amesahau nyumbani. Wabunge wengi wamekuwa wakilalamika kuwa hawawezi kumpata, licha ya juhudi zao,” asema Bw Njiru.

Rais alionekana kuelekeza hasira zake kwa wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu), Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Alice Wahome (Kandara), Rigathi Gachagua (Mathira) na wengine ambao wamekuwa wakimfanyia kampeni Naibu Rais William Ruto kuwania urais mnamo 2022.

Tayari, wabunge hao wamejitokeza wazi na kusema kuwa wataendelea na kampeni zao ikiwa Rais hataitisha kikao cha wabunge wote wa Chama cha Jubilee (JP) kujadili hali na mwelekeo wa chama.

“Tuna mambo mengi ambayo tungetaka kumfikishia Rais, na ndipo tumekuwa tukishinikiza kuandaliwa kwa kikao cha viongozi wote wa Jubilee ili kutathmini mwelekeo wa chama. Kama hataitisha kikao hicho, hatuna lingine, ila kuendelea na kampeni zetu,” akasema Bi Wahome.

Mbunge huyo alimkosoa Rais, akisema kuwa haoni vile kujihusisha kwao katika siasa kunaingilia mipango yake ya maendeleo.

Bw Nyoro alisema kuwa “ataendelea kumfanyia kampeni Dkt Ruto, kwani haoni makosa yoyote aliyofanya.”

“Nitaendelea kutetea kile ninachoamini kinawafaa watu wetu [Mlima Kenya]. Ninaheshimu kila mmoja, ila simwogopi mwanadamu yeyote,” akasema Bw Nyoro, kwenye matamshi yanayoonekana kumlenga Rais.

Mbunge wa Gatundu Kusini, Moses Kuria, alisema ataendeleza kampeni yake ya urais, “kwani ni haki yake kikatiba.”

Kando na ukanda wa Mlima Kenya, wabunge wengine ambao wamemwasi Rais kiwazi ni Oscar Sudi (Kapseret), Caleb Kositany (Soy), Anthony Kiai (Mukurwe-ini), Kimani Ngunjiri (Bahati) kati ya wengine.

Kwa kauli hizo, wachanganuzi wanasema kuwa imefika wakati kwa Rais Kenyatta kuzingatia miito ya wabunge hao, kwani huenda ikazima mgawanyiko huo, ambao unazidi kupanuka kila kuchao.

“Imefikia wakati Rais Kenyatta kuitisha kikao cha pamoja cha wabunge na viongozi wote wa Jubilee waliochaguliwa ili kuondoa tofauti zilizopo. Msimamo wake mkali utaendelea kukigawanya chama, hivyo kumzuia kutimiza malengo yake makuu ya maendeleo,” asema Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Baadhi ya masuala ambayo wabunge wanataka Rais kuwafafanulia ni mkataba kati yake na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, maarufu kama “handisheki” wakisema kuwa hawakushauriwa.

Vile vile, wanataka ufafanuzi kuhusu lengo la Kamati ya Maridhiano iliyobuniwa na Rais na Bw Odinga, wakisisitiza kuwa ilibuniwa bila kuzingatia taratibu za kisheria.

Baadhi ya wabunge wamekuwa wakisisitiza kuwa kamati hiyo inaendesha njama za kuandaa mageuzi ya katiba kichinichini, ili kuzima azma ya Dkt Ruto kuwania urais.

Rais Kenyatta pia ameahirisha ziara zake kadhaa katika ukanda huo, duru za kijasusi zikieleza kuwa hilo limechangiwa na hofu ya kukumbwa na upinzani kutoka kwa wakazi, kwani wengi wanahisi kutengwa.

Lakini katika kujitetea kwake, Rais Kenyatta amekuwa akishikilia kuwa juhudi zake zinalenga kuleta umoja nchini, akisema ataendelea kufanya hivyo, hata ikiwa hilo litamaanisha kukosana na baadhi ya viongozi.

“Nitafanya kila juhudi kuhakikisha watu wetu wanaendesha shughuli zao za kibiashara mahali popote nchini bila hofu yoyote. Sitaghairi kauli yangu kuhusu hilo,” akasema.

Hata hivyo, wachanganuzi wanasema kuwa Rais hapaswi kusahau ngome zake, hata anapotafuta amani.

“Rais Kenyatta anapaswa kufahamu kuwa hata ikiwa hatawania urais mnamo 2022, angali mwanasiasa, na umoja wa ngome zake utakuwa muhimu sana, hasa katika maamuzi ya baada ya uchaguzi huo,” asema Bw Muga.

Mwaka uliopita, zaidi ya wabunge 70 wa ukanda wa Mlima Kenya walifanya kikao katika eneo la Naivasha, wakilalamikia eneo hilo kutengwa kimaendeleo na rais.