JAMVI: Kalonzo alijikwaa kisiasa kukubali kuwa ‘mtu wa mkono’ wa Uhuru
Na BENSON MATHEKA
Huenda kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka alijikwaa katika azima yake ya kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu ujao kwa kukubali kuwa mtu wa mkono wa Rais Uhuru Kenyatta.
Japo wadadisi wanasema alichukua hatua hiyo kuendeleza muafaka ambao umefanya Kenya kuwa thabiti, Rais Kenyatta aliposalimiana na kiongozi wa upinzani Raila Odinga, washirika wa karibu wa Bw Musyoka wamemkosoa vikali wakisema amewavunja moyo.
Wadadisi wanasema ikiwa Bw Musyoka atatengwa na washirika wake kutoka eneo la Ukambani ambao wanahisi amekosa mwelekeo kwa kukubali kuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta, itakuwa mlima kwake kushinda urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.
Akihutubu wakati wa mazishi ya babake mbele ya Rais Kenyatta na viongozi wengi wa Ukambani, Bw Musyoka alisema hangetaka mtu yeyote kuingilia ushirika wake na Rais Kenyatta na kwamba hakutaka kuulizwa maswali na yeyote kuhusu uamuzi wake.
Inasemekana kuwa wawili hao walikuwa wamekamilisha mazungumzo yaliyoanza Bw Musyoka alipotembelea Ikulu Oktoba 9 mwaka huu na kisha akaandamana na Rais alipozuru China baadaye mwezi huo.
Baada ya mkutano huo, Bw Musyoka alitangaza kuwa chama chake kitaunga ajenda za serikali na akathibitisha hayo kwa kuunga hatua ya serikali ya kuanzisha ushuru mpya wa mafuta uliopingwa vikali na wabunge.
Baadhi ya washirika wa Bw Musyoka walifichua kuwa viongozi hao wawili walikuwa wameafikiana kuwa makamu huyo wa rais wa zamani akabidhiwe majukumu ambayo hayakuwa yamebainika.
Kwenye mazishi ya Mzee Peter Musyoka Mairu eneo la Tseikuru, Kaunti ya Kitui , Rais Kenyatta aliashiria kuwa angempatia Bw Musyoka wadhifa wa kueneza amani barani Afrika, ambao kiongozi wa Wiper alianza kutekeleza wikendi iliyopita nchini Sudan Kusini alipowasilisha ujumbe wa rais kwa Rais Salvar Kiir.
Hata hivyo, washirika wake kutoka Ukambani ambao wamekuwa wakimuunga mkono kama msemaji wa jamii yao kugombea urais, wanahisi kwamba alijidunisha kwa kukubali kuwa tarishi wa Rais Kenyatta.
Mwenyekiti wa chama chake cha Wiper Kivutha Kibwana, seneta wa Makueni Mutula Kilonzo Junior na aliyekuwa seneta wa Machakos Johnson Muthama walikasirishwa na uamuzi wa Bw Musyoka wakisema utakuwa pigo kwa azma yake ya kugombea urais 2022.
Viongozi hao watatu wana ushawishi mkubwa eneo la Ukambani na ni nguzo katika chama cha Wiper.
“Kiongozi wa watu akikubali kuwa mtu wa mkono, wafuasi wake ambao walimteua kuwakilisha jamii watakuwa nini?” Profesa Kivutha aliuliza.
Naye Muthama alimtaka Bw Musyoka kufafanua matamshi yake akisema inaonyesha ameacha azima yake ya kugombea urais 2022.
Wadadisi wanasema ikiwa Bw Musyoka anatarajia kupata baraka za Rais Kenyatta kuwa mrithi wake 2022, basi huenda nyota yake ya kisiasa ikawa inazima kwa kasi.
“Ilivyo ni kuwa, kwa wakati huu hakuna anayeweza kuamini atapata baraka za Rais Kenyatta kuwa mrithi wake akistaafu siasa 2022 inavyosema katiba ya Kenya. Kumbuka Rais mwenyewe amekuwa akiwaambia watu kwamba sio wakati wa siasa na uchaguzi ukifika kila mtu anafaa kuingia uwanjani kutafuta kura,” alisema Bw Paul Muasya, mdadisi wa masuala ya kisiasa.
Anasema hata kama ana mkataba wa kisiri na Rais Kenyatta, Bw Musyoka hafai kutoa matamshi au kuchukua hatua inayoweza kumtenga na washirika wake eneo la Ukambani au katika chama chake cha Wiper.
“Ni hatari sana kwa mwanasiasa kukosa uungwaji mkono nyumbani. Bw Musyoka hafai kuamini sana watu walio nje ya ngome na nyumba yake ya kisiasa. Wakimuacha itakuwa pigo kubwa kwake,” alisema.
Imeibuka kuwa, huenda kuna makundi mawili katika chama cha Wiper yanayovuta pande tofauti- moja likimtaka Bw Musyoka kushirikiana na Naibu Rais William Ruto ambaye ameanza kampeni za mapema na lingine likimtaka ashirikiane na Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga kuendeleza muafaka.
“Wale ambao wanamtaka ashirikiane na Bw Ruto hawakufurahi alipotangaza kuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta. Kuna mvutano ndani ya chama. Hii ndiyo ilimfanya Bw Musyoka kusema kuwa hataki yeyote kuingilia ushirikiano wake na Rais, na kwamba hafai kuulizwa maswali,” alisema mbunge mmoja wa chama cha Wiper ambaye aliomba tusitaje jina lake. Kulingana na katibu mkuu wa Wiper, Judith Sijeny, chama hicho kilimpatia Bw Musyoka ruhusa ya kukubali wadhifa wa kuwa balozi wa amani. Aliwalaumu viongozi wanaomkosoa Bw Musyoka kwa kutosema ukweli.
Wadadisi wanasema kwamba inaweza kuwa pigo kubwa kwa Bw Musyoka ikiwa atatofautiana Bw Kibwana, Bw Muthama na viongozi wengine wa ngome yake ya kisiasa ya Ukambani ambao wanasema kukubali kuwa mtu wa mkono wa Rais Kenyatta hakutaifaidi jamii na eneo lao.
“Bw Musyoka anafaa kupanga vyema nyumba yake ya kisiasa ikiwa anataka kuwa Rais. Akikosa kuungwa mkono na watu wake, asahau urais,” asema Bw Douglas Ngui, mdadisi wa siasa za Ukambani.
Kulingana na Profesa Kibwana, Bw Musyoka angeeleza jinsi ushirikiano wake na Rais Kenyatta utafaidi wakazi wa eneo la Ukambani.
“Inaonekana hakushauriana vyema na washirika wake wa kisiasa kabla ya kukubali wadhifa wake wa kuwa balozi wa amani au ikiwa alifanya hivyo, hakukuwa na makubaliano na ndio sababu alisema hakutaka kuulizwa maswali,” asema Bw Ngui.