JAMVI: Kura ya maamuzi haitawezekana mwaka huu
Na LEONARD ONYANGO
HALI ya sintofahamu inayofumbata nchi hii kwa sasa kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona imeweka Mpango wa Maridhiano (BBI) katika njiapanda na kuzima kampeni za mapema za wanasiasa wanaomezea mate viti katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Sasa ni bayana kwamba kura ya maamuzi ili kubadili katiba haitafanyika mwaka huu kinyume na mapendekezo ambayo yamekuwa yakitolewa na kinara wa ODM Raila Odinga.
Japo wanasiasa wa ODM wanashikilia kuwa ni sharti kura ya maamuzi ifanyike mwaka huu, wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa huenda ikafanyika mwaka ujao au ikose kabisa kufanyika kutoka na ukosefu wa fedha na muda wa kutosha.
Jopokazi la BBI linaloongozwa na Seneta wa Garissa Yusuf Haji lilikamilisha mkondo wa pili wa vikao vya kusikiza mawasilisho kutoka kwa wananchi na makundi mbalimbali mnamo Machi 10, mwaka huu. Lakini liliendelea kupokea maoni kwa njia ya maandishi hadi Machi 31.
Jopokazi hilo linafaa kuwasilisha ripoti yake ya mwisho kwa Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga mwishoni mwa Juni.
Chama cha ODM sasa kinataka jopokazi hilo kuwasilisha ripoti yake pamoja mswada wa kubadili katiba ili kuwezesha mchakato wa kutaka kubadili katiba kuanza mara moja.
Viongozi wa ODM pia wanapanga kaunzisha shughuli ya kukusanya saini milioni 1 kutoka kwa wananchi mara tu baada ya kuwasilishwa kwa ripoti ya mwisho.
Lakini mdadisi wa masuala ya kisiasa Javas Bigambo anasema itakuwa vigumu kukusanya saini iwapo janga la virusi vya corona litaendelea hadi mwishoni mwa Mei.
Huku viwanda vikiwa vimefungwa na shughuli za kiuchumi zimekwama, Bw Bigambo anasema kuwa itakuwa vigumu kupata fedha za kufanyia kura ya maamuzi.
Hii ni kwa sababu Tume ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haikujumuisha fedha za kura ya maamuzi katika bajeti yake ya mwaka ujao wa fedha wa 2020/2021 utakaoanza Julai, mwaka huu.
Seneta wa Siaya James Orengo anasema kuwa kura ya maamuzi inahitaji Sh2 bilioni kwa sababu wapigakura watahitaji kuandika ‘Ndiyo’ au ‘Hapana’ tofauti na uchaguzi mkuu ambapo wanapigia kura wawaniaji wa viti sita.
Bw Orengo anasema kuwa serikali pia inaweza kukopa fedha za kufanyia kura ya maamuzi.
“Hata wakati wa uchaguzi mkuu wa 2013, serikali ya Kenya ililazimika kukopa,” anasema wakili Orengo.
Lakini wadadisi wanasema kuwa ulimwengu sasa unakabiliana na virusi vya corona na itakuwa vigumu kwa Kenya kupata mkopo wa Sh10 bilioni kufanyia kura ya maamuzi.
Kadhalika, Kiongozi wa Wengi Bungeni Aden Duale anasema kuwa itahitaji maandalizi ya takribani muda wa miezi 12 kabla ya kufanyika kwa kura ya maamuzi.
“Utaratibu wa kisheria ni mrefu mno. Kutakuwa na haja ya kukusanya saini kutoka kwa wananchi na shughuli hiyo itachukua miezi kama miwili, baadaye mswada utajadiliwa katika mabunge yote ya kaunti 47 kwa miezi mitatu. Baada ya kupitishwa mswada huo utaletwa katika bunge la kitaifa ambapo utashughulikiwa na kisha kupelekwa katika seneti,” anasema Bw Duale.
Lakini Bw Orengo anasema shughuli ya kukusanya saini inaweza kuchukua mwezi mmoja na mabunge ya kaunti yatalazimika kufupisha muda.
Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka anaonya kuwa ikiwa kura ya maamuzi itakosa kufanyika mwaka huu basi itakuwa vigumu kuiandaa mwaka ujao kwani tume ya IEBC itakuwa imeanza maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2022.
Iwapo kura ya maamuzi itakosa kufanyika, itakuwa habari njema kwa kundi la wandani wa Naibu wa Rais William Ruto ambao wamekuwa wakishinikiza kura ya maamuzi ifanyike pamoja na uchaguzi mkuu wa 2022.
Kamati ya Bunge Inayosimamia Utekelezaji wa Katiba inayoongozwa na mbunge wa Ndaragwe Jeremiah Kioni, pia inapendekeza kuwa kura ya maamuzi ifanyike pamoja na uchaguzi mkuu ujao.
Mbunge wa Marakwet Mashariki Bowen Kangogo na Mwakilishi wa Kike wa Kaunti ya Nakuru Liza Chelule ambao ni wandani wa Dkt Ruto, wanataka jopokazi la BBI kusitisha shughuli zake na fedha zilizotengwa kwa ajili ya shughuli hiyo zielekezwe katika vita dhidi ya virusi vya corona.
“Kwa sasa suala muhimu ni virusi vya corona. Mpango wa BBI unafaa kutupiliwa mbali. Ripoti iliyozinduliwa mwaka jana iwasilishwe Bungeni ifanyiwe kazi,”anasema Bw Kangogo.
Mbunge wa Soy Caleb Kositany anasema kuwa jopokazi la BBI linafaa kusitisha shughuli zake hadi baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.
Wanasiasa wa Tangatanga pia wanahisi kuwa Dkt Ruto ametengwa katika vita dhidi ya maradhi ya corona.
Wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen na naibu gavana wa Kisii Joash Maangi wamekuwa wakisisitiza kuwa vita dhidi ya virusi vya corona vinafaa kujumuisha kila kiongozi na wala visiingizwe siasa.
Viongozi wa Tangatanga wanahofia kuwa hatua ya naibu wa rais kutoshirikishwa katika kamati ya kukabiliana na maradhi ya corona huenda ikamuumiza kisiasa katika uchaguzi ujao.
Dkt Ruto ambaye tayari alikuwa ameanza kampeni zake za mapema kwa ajili ya kinyangányiro cha urais 2022, hajajumuishwa katika kamati ya kukabiliana na virusi vya corona na sasa amekuwa akitumia mitandao ya kijamii kuhimiza Wakenya kuketi nyumbani.