JAMVI: Kura za Kibra ni mwanzo wa safari ya farasi wawili kuelekea 2022
Na CECIL ODONGO
Uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kibra uliofanyika Alhamisi wiki jana umebainisha kwamba farasi wawili katika siasa za 2022 ni Kinara wa ODM Raila Odinga na Naibu Rais Dkt William Ruto.
Bw Odinga bado hajatangaza iwapo atakuwa debeni 2022 lakini inakisiwa kwamba atajaribu bahati yake kwa mara ya tano baada ya kuwania Urais 1997, 2007, 2013 na 2017.Dkt Ruto naye tayari ametangaza kwamba atakuwa kiny’ang’anyironi 2022.
Kutokana na matukio mengi ya kisiasa yaliyozingira kuandaliwa kwa uchaguzi huo mdogo wa Kibra ambapo Bernard Imran Okoth wa ODM alishinda kwa kura 24,636 dhidi ya mwanasoka wa kimataifa MacDonald Mariga wa chama cha Jubilee ambaye alijizolea kura 11,230, ni wazi kwamba moja kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto ana nafasi nzuri ya kuingia Ikulu baada ya Rais Uhuru Kenyatta kustaafu siasa.
Kinara wa ANC Musalia Mudavadi, mwenzake wa Wiper Kalonzo Musyoka na nyapara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula bado wanaonekana walegevu kutokana na jinsi wawaniaji wao walivyofifia kwenye kura za Kibra.Licha ya Bw Mudavadi kufanya kampeni kabambe, mwaniaji wa chama chake Eliud Owalo alipata kura 5, 275 na akatangaza kukubali kushindwa baada ya matokeo rasmi kutangazwa.
Bw Musyoka naye ameshutumiwa kwa kimya chake kuhusu uchaguzi huo japo chama chake kilikuwa kimetangaza kuunga mkono mwaniaji wa Ford Kenya Khamisi Butichi aliyejizolea kura 260 pekee.
Kulingana na wachanganuzi wa kisiasa, viongozi hawa watatu bado wana kibarua kudhihirisha kwamba wanaungwaji mkono katika ngome zao na maeneo mengine ya nchi.
“Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula bado wana kibarua kigumu kujionyesha kama viongozi ambao wanaweza kupata kura katika maeneo mengine bali na ngome zao. Siasa ni idadi ya kura kiongozi anaweza kuvutia na siyo kukosa kuchukua msimamo,’ akasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati.
Rais Uhuru Kenyatta pia hakushiriki kwenye kampeni za Kibra huku baadhi ya wabunge wa Jubilee waliokuwa wakimuunga mkono Bw Imran wakisema mwaniaji huyo alikuwa na baraka za kiongozi wa nchi kugombea kiti hicho cha ubunge kilichokuwa kikishikiliwa na marehemu nduguye Ken Okoth.
Kuonyesha kwamba 2022 ni kivumbi cha farasi wawili pekee, punde tu uchaguzi mdogo wa Kibra ulipotangazwa baada ya kifo cha Ken Okoth miezi mitatu iliyopita na IEBC, wachanganuzi wa masuala ya kisiasa na viongozi walisema kwamba ungetumika kama jukwaa la kupima ubabe kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto.
Hayo yalidhihirika wakati viongozi hao wawili walipokita kambi Kibra na kufanya kampeni kali hasa dakika za lala salama.
Kuonyesha jinsi uchaguzi huo ulivyokuwa umejaa hisia kali, kuliripotiwa matukio mbalimbali ya ghasia kabla ya kura hiyo na baada ya harakati hizo.
Kwa mfano, katika baadhi ya vituo vya kupigia kura kama uwanja wa DC, Mashimoni, Kibra Old School kati ya vingine, ghasia zilishuhudiwa baadhi ya maajenti au watu wakipigwa kura vibaya kwa madai ya uwepo wa ununuzi wa kura.
Makundi ya vijana waliodaiwa kutoka chama cha ODM waliwavamia wabunge wa Jubilee Ben Washiali wa Mumias Mashariki, Oscar Sudi wa Kapseret and Didmus Barasa wa Kiminini na aliyekuwa Seneta wa Kakamega Bonny Khalwale ambao walilazimika kukimbilia usalama wao.
Kuonyesha kwamba siasa za Kibra zilikuwa kati ya Bw Odinga na Dkt Ruto na matayarisho ya jinsi mambo yatakavyokuwa 2022, wabunge wa ODM walijigawa katika makundi mbalimbali yaliyosimamia vituo vya upigajikura kisha kuwaagiza maajenti wao watume matokeo yao kupitia simu hadi wakfu wa Jaramogi Oginga Odinga ambako walikuwa wakijumuisha kura zao.
Wenzao wa Jubilee nao walikuwa ange licha ya uhasama dhidi yao na makundi ya vijana kwa kutuma matokeo yao hadi kwa maafisa wao waliokuwa wakijumuisha kura zao katika hoteli moja jijini Nairobi.
Kulingana na Mbunge wa Suba Kusini John Mbadi ambaye pia ni Mwenyekiti wa ODM, ushindi wa Bw Imran Kibra ni mwanzo wa makabiliano makali ya kisiasa kati ya wanaomuunga Bw Odinga na Dkt Ruto.’
“engi walikuwa wakisema kwamba Bw Ruto amemzidi Kinara wetu kisiasa hadi sasa ameingia kwenye ‘chumba chake cha kulala’ lakini sasa wamefahamu kwamba hawana ufuasi wowote wa kupimana ubabe na kiongozi wetu,” akasema Bw Mbadi kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Kiranja huyo wa wachache kwenye Bunge la Kitaifa pia alisema watamakinika 2022 kuhakikisha kura zao zinalindwa jinsi walivyofanya Kibra huku wakimtaka Dkt Ruto kujitayarisha kwa kivumbi kikali.
Aidha Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed ambaye pia ni kiranja wa wachache bungeni alisema matokeo ya Kibra yatatumika kuvumisha ripoti ya Jopokazi la Mariadhiano (BBI) ambayo inatarajiwa kutoa mwelekeo wa siasa za 2022.
Huku Bw Odinga akiunga ripoti ya jopo hilo walilobuni pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, Naibu Rais na wandani wake wa kisiasa wamekuwa wakiipinga, baadhi wakidai kwamba ni njama ya kumzima kuingia Ikulu 2022.
“Ushindi wa Bw Imran ambaye sasa ni Mbunge wa ‘handisheki’ ndiyo mwanzo wa kuvumisha BBI ambayo Dkt Ruto amekuwa akipinga. Tutamwonyesha kivumbi kwa BBI jinsi Bw Mariga alivyoshindwa kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra,” akasema Mohamed wakati wa kutangazwa rasmi kwa matokeo katika Chuo cha Mafunzo cha Inspectorate, Dagorretti.
Hata hivyo, Bw Washiali ameonya ODM kwamba wasifikirie kwamba kura hushindwa kupitia ghasia au kuwatishia viongozi wengine.’
“Kile walichofanya Kibra ni kutumia ghasia lakini Kenya yote haitakuwa Kibra. Tupo tayari kupambana kwa debe kwa sababu tumewaonyesha kwamba hata kwa chumba chao cha kulala tunaweza kupata kura za maana ikilinganishwa na zile tulipata 2017,” akasema Bw Washiali.
Japo ni mapema kutabiri miungano wa kisiasa itakayochipuka 2022, ni wazi kwamba makali ya viongozi wengine kisiasa nchini hayafikii yale ya Bw Odinga na Dkt Ruto.
Hii ndiyo maana magavana, maseneta, wabunge na viongozi kutoka maeneo mbalimbali wamekuwa wakionyesha uaminifu wao kwa moja kati ya viongozi hawa.