AIPCA: Ni kanisa la Kiafrika lililoshirikiana na Mau Mau
Kanisa la Independent Pentecostal Church of Africa (AIPCA) huenda lilikuwa kanisa la pekee lililohusishwa moja kwa moja na harakati za ukombozi wa kitaifa, na kwa msingi huo lilitarajiwa kupata uungwaji mkono kutoka kwa serikali ya Kenyatta.
Hata hivyo, kama ilivyokuwa kwa shughuli za Mau Mau, AIPCA haikupata msaada mkubwa wa moja kwa moja. Kanisa hili lilianzishwa wakati wa kipindi kigumu ambapo kazi za kulazimishwa zilianzishwa eneo la Kati mwa Kenya, jambo lililosababisha kuundwa kwa chama cha Kikuyu Association mwaka wa 1920 na Young Kikuyu Association mwaka wa 1921.
Katika chama cha pili, ambacho baadaye kilibadilishwa jina kuwa Kikuyu Central Association (KCA) mwaka wa 1925, taasisi nyingi za kidini zilichipuka na kuaminika kuwa sura mpya ya ajenda za kisiasa za jamii hiyo.
Ingawa Bw David Kiragu Maina wa Fort Hall (Murang’a) alikuwa ameanzisha kanisa huru mwaka wa 1921, ni kuanzishwa kwa AIPCA mwaka wa 1925 kulikotoa changamoto kubwa kwa makanisa ya wamishonari wa Ulaya miongoni mwa Wakikuyu.
AIPCA iliwatumia wanasiasa maarufu kama James Beauttah kuwezesha kutoa mafunzo kwa makasisi wao. Ndani ya kanisa hili ndipo wazo la kuanzisha shule huru lilizaliwa, kwa nia ya kujibu mahitaji ya kisiasa na elimu ya jamii ya Wakikuyu.
Hili lilitokana na hofu kuwa wamishonari walishirikiana na serikali ya kikoloni kuwanyima Wakenya ujuzi na maarifa.Kutokana na hali hiyo, makundi mawili yaliibuka: Kikuyu Independent Schools Association (KISA) na Kikuyu Karing’a Education Association kwa wafuasi wa mtazamo wa kitamaduni wa Kikuyu.
Kwa hivyo, tangu mwanzo wake, AIPCA ilikuwa na uhusiano wa karibu na siasa, ikiwa ni kanisa lililokuwa na mwamko wa kisiasa na lililoongozwa na falsafa ya kihooto (haki).Waasisi wake walikuwa wanasiasa waliokuwa ndani ya KCA, akiwemo Peter Gatabaki Mundati, Johanna Kunyiha na Willy Jimmy Wambugu.
Wengine walikuwa Waira Kamau (baadaye Mbunge wa Juja), Taddeo Mwaura (Mbunge wa Kandara) na Wanyoike Thungu (baadaye mlinzi wa Kenyatta).Hata hivyo, kutokuwepo kwa ushawishi mkubwa wa kisiasa kwa AIPCA kulitokana na migogoro ya mara kwa mara ya uongozi.
Hali hii ilisababisha kuibuka kwa makundi mawili: African Independent Pentecostal Church of Kenya (AIPCK) chini ya Askofu Mkuu John Mugecha, na AIPCA iliyobaki chini ya Askofu Mkuu Benjamin Kahihia, mmoja wa makasisi wanne wa kwanza waliowekwa wakfu mwaka wa 1937.
Kuibuka kwa AIPCK kama tawi lililojitenga kulionekana kuwa tishio kubwa kwa makanisa ya kimishonari na pia kwa serikali ya kikoloni. Kwa kuwa haikuwa na viongozi waliowekwa wakfu, kanisa liliongozwa na watu wa kawaida na wanasiasa waliokuwa na uhusiano na KAU.
Kwa sababu hiyo, wanasiasa kama James Beauttah walimwendea Askofu Daniel Alexander William, Mmarekani mwenye asili ya Mauritius, ili kusaidia mafunzo ya makasisi wa kwanza wa kanisa.
Ndani ya kundi hili, waliowekwa wakfu wa mwanzo walikuwa Kahihia, Harrison Gacokia na Daudi Kiragu.Moja ya migogoro ya awali kati ya AIPCA na makanisa ya kimishonari ilikuwa kuhusu suala la tohara ya wasichana, jambo ambalo lilipingwa vikali na wamishonari.
Wamishonari walianzisha kiapo cha kirore (sahihi au alama ya kidole gumba), ambapo familia zilizoshindwa kulaani tohara ya wasichana zilipigwa marufuku kushiriki meza ya Bwana au kuwapeleka watoto wao shule za kanisa.
Hali hii ilisababisha kuibuka kwa shule za Karing’a (kumaanisha shule za Wakikuyu halisi). Kuzaliwa kwa shule huru mbili kati ya 1928 na 1929 kulithibitisha mwamko huo. Aidha, uongozi wa Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Githunguri chini ya Mbiyu Koinange, ambapo Jomo Kenyatta alikuwa Mkuu, kilipatia kanisa huru hadhi kubwa.
Kadiri harakati za kupigania uhuru zilivyokuwa zikishika kasi, AIPCA ikawa kama tawi la kidini lisilotambulika la harakati hizo. Kwa sababu hiyo, serikali ya kikoloni ilipoamua kukandamiza Mau Mau, AIPCA pia ikawa miongoni mwa walengwa.
Kanisa hilo pamoja na shule zake huru zilipigwa marufuku.Kabla ya Siku ya Kwanza ya Jamhuri, ujumbe wa AIPCA ulitembelea nyumbani kwa Kenyatta Gatundu na kuwasilisha ombi.
Walitaka kanisa lisajiliwe rasmi na kurejeshewa shule lililokuwa likisimamia kabla ya kuchukuliwa na makanisa ya kimishonari baada ya vita vya Mau Mau na hali ya hatari kutangazwa mwaka wa 1952.
Ingawa Kenyatta alikubali usajili wa kanisa hilo, migawanyiko ya uongozi na serikali kuchukua usimamizi wa shule hizo kulisababisha ombi lao la pili kupuuzwa.AIPCA ilifufuliwa mwaka wa 1963 na kusajiliwa rasmi Februari 13, 1964.
Kanisa lililohusiana nalo, National Independent Church of Africa (Eneo la Embu na Meru), liliandikishwa Februari 7, 1964, huku African Orthodox Church of Kenya likisajiliwa mwaka wa 1965.
AIPCA iliendelea kutumia ushawishi wa marafiki wao wa kisiasa kama Wanyoike Thungu na Koinange ili kuendeleza harakati zao. Walipanga safari nyingi za wanafunzi kwenda Gatundu, mojawapo ikiwa mwaka wa 1968 ambapo maelfu ya watoto kutoka Nyeri, Kirinyaga na Laikipia walimtembelea Kenyatta kama sehemu ya kudai kanisa kurejeshewa shule zao.
Mafanikio mojawapo yalikuwa kufunguliwa tena kwa Kenyatta Mahiga High School huko Nyeri mwaka wa 1969 na Koinange baada ya shule hiyo kufungwa mwaka wa 1953. Shule hiyo ya AIPCA ilikuwa imefungwa kwa madai kuwa waanzilishi wake walikuwa na uhusiano wa karibu na Mau Mau.
Kwa sababu ya ukaribu wake na Kenyatta kwa miaka mingi, AIPCA ilichukua msimamo wa kutotilia shaka uongozi wa serikali na haikuwa na ushawishi mkubwa kisiasa.Hata hivyo, ilitumika kama chombo cha kuanzisha shule za Harambee, nyingi zikiwa maeneo ya Nyeri, Kiambu na Murang’a, zilizojengwa katika maeneo ya shule za zamani.
Hili limeendelea kuibua mgogoro kwani kanisa bado linadai usimamizi wa shule hizo.Lakini kutokana na migogoro ya uongozi tangu awali, makanisa haya hayakuweza kusukuma ajenda yao ipasavyo. Ingawa Kenyatta aliepuka kuingilia migogoro hiyo, wanasiasa kama Waira Kamau waliendelea kuwa na ushawishi mkubwa, hali iliyojitokeza zaidi baada ya kifo cha Kenyatta.