Jamvi La Siasa

Dalili Ruto sasa hapendwi Mlima Kenya, aonekana kama ‘msaliti’

Na MWANGI MUIRURI  October 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto yuko katika njia panda anapoangalia kura alizopokea kutoka eneo la Mlima Kenya zikionekana kupungua pakubwa kuelekea uchaguzi wa 2027.

Hali hii imejiri baada ya uhusiano wake na Naibu Rais aliyeondolewa Rigathi Gachagua kuharibika huku wakazi na baadhi ya viongozi wakiwa na hasira dhidi ya Rais.

“Tuache kujifanya kuwa hali ni nzuri Mlimani. Hivi maajuzi tulihofia kuwa Dkt Ruto ataonekana adui wa Mlima Kenya…ni kama hayo yamefanyika hatimaye,” alisema Seneta wa Murang’a Joe Nyutu.

Katika chaguzi za vyama vingi, eneo la Kati limekuwa likipiga kura dhidi ya wawaniaji ambao linawaogopa ama kuwachukia, Dkt Ruto anaonekana kuingia kwenye orodha hii kufikia 2027.

Bw Nyutu ameambia Taifa Leo kuwa eneo hilo halikutarajia Bw Gachagua atapitia masaibu baada yake kutimuliwa na Bunge.

“Kinachoonekana kuwa mbaya zaidi  Mlima Kenya sasa ni kuondolewa kwa Gachagua. Tunajua Rais Ruto aliudhi sana utawala wa Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa Naibu Rais lakini haikufika katika kiwango cha kuchukiana,” alisema.

Mwimbaji wa nyimbo za Injili Ben Githae aliyevuma kwa nyimbo za kupigia debe Bw Kenyatta na Dkt Ruto katika chaguzi za 2013 na 2017 ameambia Taifa Leo kuwa sasa ni wakati wa kuimba nyimbo za kuchukizwa na serikali hii.

“Ni wakati wa kuunda pesa kwa kuimba nyimbo za kudhihirisha kuchoshwa na serikali na kuwarejesha mashabiki wangu waliopotea. Sasa ninavuma na kibao changu kwa jina ‘Wasaliti’,” alisema Bw Githae akieleza kuwa Dkt Ruto hauziki tena kimuziki.

Katibu Mkuu wa Chama cha UDA Bw Omar Hassan ameambia Taifa Leo kuwa hawawezi kuacha eneo la Kati nyuma katika juhudi zao za kuunganisha Wakenya.

“Hatuwezi kukubali kuvutwa katika siasa za kuzuiana, kujitenga na kufunga maeneo fulani kuwa hayafai kutembelewa,” alisema.

Bw Hassan alikuwa anarejelea kauli ya Rais Ruto akiwa Uasin Gishu Jumapili alipoonekana kumpiga vijembe Bw Gachagua kuwa mwanasiasa anayeendeleza siasa za ukabila.

“Siwezi kukoma kuunganisha Wakenya wote na kufanya maeneo yote kujihisi kuwa sehemu ya serikali bila kubaguliwa,” alisema Rais.

Akiwa Kiambu mnamo Jumapili, Bw Gachagua alirai wananchi kumuombea Rais Ruto ili awakomboe dhidi ya ushuru wa juu, ukosefu wa kazi, uchumi mbaya na sekta ya afya yenye matatizo.

“Mwombeeni Rais apate njia ya kuokoa nchi ing’atuke kutoka kwa matatizo haya,” akasema.

Siku hiyo hiyo, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alisikitikia masaibu ya Bw Gachagua huku akiashiria eneo la Kati limejitenga na Dkt Ruto.

Kalonzo alisema: “Tunashukuru kuwa watu wa Mlima Kenya hawajaingia katika mtego wa kugawanywa kupitia njia ya kulaghaiwa kuwa mnaunganishwa.”

Lakini Mlezi wa Kitaifa wa Kiama Kia Ma Bw Kung’u Muigai amepinga kauli kuwa Rais anapingwa eneo la Mlima Kenya akisema Kaunti za Meru, Tharaka Nithi na Embu zinamfurahia Dkt Ruto.

“Ni Wakikuyu wa (Nyeri, Murang’a, Kirinyaga na Kiambu) ambao wanajitenga na sehemu nyingine za nchi,” alisema.

Mwenyekiti wa chama cha PNU Bw Peter Munya aliambia Taifa Jumapili kuwa ‘eneo hilo lina shida kubwa sana na Rais Ruto.’

“Rais anageuza wanasiasa wanaomuamini kuwa kama roboti zinazoambiwa cha kufanya. Nchi imefika kiwango cha kupigwa mnada,” Bw Munya alikariri kauli ya Bw Gachagua.

“Inaoneka kuwa wale ambao wanataka kupendwa na wapigakura wanafaa kukaa mbali na Rais Ruto,” aliongeza Bw Munya.

Lakini Mbunge wa Mbeere Kaskazini Bw Geoffrey Ruku anasema wanaompinga Dkt Ruto eneo la Kati ni wachache.

Alisema: “Tunafaa kuungana na Rais Ruto ili kupata maendeleo.”

Naye Seneta wa Kiambu Bw Karungo Thang’wa alimpinga Bw Ruku.

“Hatuwezi kuwavamia wale ambao hawapendwi na Rais ili tupate maendeleo.”