Jamvi La Siasa

DCP ya Gachagua yateua kundi lake la kwanza la wawaniaji chaguzi ndogo

Na DANIEL OGETTA July 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

CHAMA cha Democracy for the Citizens Party (DCP) Alhamisi kilizindua rasmi kundi lake la kwanza la wawaniaji kama maandalizi ya chaguzi ndogo zijazo, katika juhudi za kumenyana na muungano wa Rais William Ruto na  kiongozi wa ODM Raila Odinga.

Chama hicho kipya, kinachoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua aliyeondolewa madarakani miezi minane iliyopita kimetangaza nia ya kushiriki kikamilifu kwenye siasa za kitaifa kupitia chaguzi hizi.

Wataalamu wa siasa wanasema chaguzi  mdogo zitaonyesha mwelekeo wa hali itakavyokuwa katika uchaguzi mkuu wa 2027.

Naibu kiongozi wa chama hicho, Cleophas Malala, aliwasilisha wawaniaji wawili: Aden Mohamed kwa kiti cha ubunge cha Banisa na Edgar Busiega wa kiti cha ubunge cha Malava.

Nafasi hizi zilibaki wazi baada ya vifo vya wabunge Kulow Maalim Hassan (Banisa) na Moses Injendi (Malava).

“Hawa ni vijana. DCP ni chama kinachoamini kulea viongozi chipukizi. NEC na kiongozi wa chama wameahidi kutenga rasilmali kuhakikisha tunashinda zaidi ya asilimia 50 ya viti vitakavyogombewa,” alisema Bw Malala.

Alimtaja Aden Mohamed kama “nembo ya mabadiliko” katika uchaguzi wa Banisa na kuwataka wakazi wa eneo hilo “kumwamini kijana huyo.”

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeunda kikamilifu kikatiba na inajiandaa kusimamia chaguzi ndogo 22 zilizokuwa zimechelewa kutokana na ukosefu wa idadi kamili ya makamishna.

Nafasi hizi ni pamoja na viti 6 vya Bunge la Taifa, 1 cha Seneti, na 15 vya MCA.

“Kama DCP, tumeamua kuwasimamisha wagombea katika kila uchaguzi mdogo nchini,” alisema Bw Malala.

“Tunaitaka IEBC kuharakisha mchakato wa kupanga chaguzi hizo.”

Miongoni mwa maeneo wanayopania ni Kasipul (ambako aliyekuwa Mbunge Ong’ondo Were aliuawa) na Ugunja, ambayo imeachwa wazi baada ya Opiyo Wandayi kuteuliwa kuwa Waziri wa Kawi.

Bw Malala alionya dhidi ya vitisho vya wizi wa kura na kuisihi IEBC isimamie kwa nguvu kanuni za uchaguzi.

“Tumewaona baadhi ya washirika wa Rais wakidokeza kuwa wataiba kura 2027. Tutawasilisha malalamishi rasmi  kwa IEBC dhidi yao. Hatuwezi kuruhusu matakwa ya wananchi kuchezewa,” alisema.

Bw Busiega alisema: “Mimi ni kijana wa kijijini, nimelelewa kwa maadili ya kifamilia. Nimejiunga na chama hiki kwa sababu kinawasikiliza wananchi. Nitajitosa mashinani kutafuta kura.”

Kwa upande wake, Bw Mohamed (aliyehama kutoka ODM), alisema uamuzi wake ulitokana na ushauri wa wafuasi wake: “Nilishauriwa na waliokuwa wananisaidia 2022 kuwa nihamie DCP. Nawaahidi DCP kuwa Banisa itakuwa ngome ya kwanza ya ushindi wa chama hiki kipya.”

Bw Malala alidai kuwa chama hicho kimepata umaarufu mkubwa ndani ya miezi miwili iliyopita, kikisajili wanachama zaidi ya 1.8 milioni.