Gachagua akomboe ushawishi wake mlimani baada ya ziara ya Ruto
BAADA ya Rais William Ruto kukamilisha ziara yake ya wiki moja katika eneo la Mlima Kenya, macho yote sasa yanaelekezwa kwa aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua kuona iwapo atakomboa ushawishi wake ambao kiongozi wa nchi alilenga kubomoa.
Katika ziara hiyo, Rais na washirika wake walionyesha ubabe kwa kuhudhuria mikutano mikubwa huku wakimshambulia Bw Gachagua na kumsawiri kama asiye na ushawishi.Rais mwenyewe alisisitisa kuwa angali simba wa eneo hilo kisiasa akisema hahitaji kuomba ruhusa kutoka kwa yeyote kulitembelea.
|Akizungumza mjini Maua, Kaunti ya Meru mnamo Jumatano, Rais alieleza kuwa urafiki wake na eneo hilo umejengwa kwa zaidi ya miaka ishirini na hauwezi kuvunjwa na mtu binafsi.’
Urafiki wangu na watu wa Mlima Kenya umejengwa kwa zaidi ya miaka 20. Hakuna mtu anayeweza kuja kati yangu na watu wa Mlima Kenya,’ alisema Ruto.
Alisisitiza kuwa ataendelea kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni.
“Kwa sababu mlinipigia kura, nitaendelea kufanya kazi hadi mshangae,”aliongeza.
Bw Gachagua amekuwa akilaumu Rais Ruto na serikali yake kwa kutenga eneo hilo kimaendeleo na kulenga kutimua washirika wake serikalini.Kabla ya ziara ya Ruto katika eneo la Mlima Kenya, Gachagua alimwambia Rais aache kujivunia miradi akisema ilianzishwa na Rais wa zamani Uhuru Kenyatta.
“Unapokuja hapa, sema ukweli. Miradi yote hii ya Mlima Kenya, ni Rais Uhuru Kenyatta aliyeanzisha. Wewe umekataa kuikamilisha. Hakuna hata mmoja ambao ni wako. Usithubutu kudanganya watu,” alisema Gachagua akiwa Wangige, Kaunti ya Kiambu mnamo Machi 31, 2025.
Ziara
Ziara hiyo ya wiki moja ilikuwa ya kwanza rais kutembelea eneo hilo baada ya takriban miezi sita tangu atofautiane na Gachagua na kuidhinisha kuondolewa kwake ofisini. Alifika Laikipia, Nyeri, Nyandarua, Kirinyaga, Murang’a, Embu, Tharaka Nithi, Meru na Kiambu.
Akiwa Tharaka Nithi, Rais Ruto alimsifu naibu wake Kithure Kindiki akionekana kufichua kuwa tangu mwanzo alipanga ashikilie wadhifa huo licha ya kumteua Gachagua kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu wa 2022.
“Mimi nilikuja hapa wakati wa uchaguzi mkitaka kuchagua huyu bwana awe gavana wenu. Nikawaambia mnipe huyu Profesa nitembee naye. Baadaye akawa Waziri wa Usalama na sasa yeye ndiye Naibu Rais,” Ruto alisema.
Rais alimpongeza Kindiki kwa kuwa kiongozi mpole mwenye nia ya kuunganisha taifa na kukuza maendeleo.“Nashukuru kwa sababu mlimkubali Profesa Kindiki ajiunge nami kuwatumikia Wakenya. Ni mtu wa heshima, mwenye bidii na mwenye nidhamu,” Ruto aliongeza.
Katika kauli iliyomlenga Gachagua, Ruto alimlaumu kwa kuchochea siasa za mgawanyiko kabla ya kuondolewa kwake madarakani, na kumkumbusha kuwa Kindiki sasa ni Naibu wa Rais wa nchi nzima.
“Naibu Rais si wa Tharaka Nithi, wala Mlima Kenya, wala Chuka pekee. Yeye ni Naibu Rais wa nchi nzima,” aliongeza.
Wachambuzi wa siasa wanasema baada ya Ruto kukamilisha ziara yake itabidi Gachagua asuke mikakati ya kujikomboa na kuonyesha kwamba ushawishi wake hakuathiriwa kwa vyovyote. \
“Gachagua hana budi kujikomboa hata kama umati uliohudhuria mikutano ya rais ulilipwa au wakazi walitishwa kufanya hivyo baadhi ya walivyodai,” asema mchanganuzi wa siasa Benard Kibara.