Jamvi La Siasa

Gachagua alenga kuponyoka na mahasla wa Ruto

Na JUSTUS OCHIENG’ May 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto na aliyekuwa naibu wake Rigathi Gachagua sasa wamejikuta wakiwa pande tofauti za uwanja wa kisiasa unaobadilika kwa kasi.

Katika mabadiliko ya kushangaza baada ya kutofautiana kwao, Bw Gachagua siku ya Alhamisi alizindua chama kipya cha kisiasa, hatua ya moja kwa moja ya kumpinga Rais Ruto, huku akirejelea ujumbe ule ule maarufu wa “hasla” uliowapa ushindi mnamo Agosti 2022.

Ahadi kuu na kaulimbiu zenye matumaini, zilizowasilishwa na chama kipya ni juhudi za kumvutia mwananchi wa kawaida anayehisi kutengwa na mfumo wa kisiasa unaotawaliwa na tabaka la watawala. Huu ni mwelekeo unaofanana na ule uliotumiwa na Rutomiaka mitatu iliyopita kuomba kura.

Gachagua, aliyekuwa mtu wa pili kwa mamlaka serikalini, anajibadilisha kisiasa na ameanzisha chama cha Democracy for the Citizens Party (DCP) akilenga mahsla, wakati huu kama silaha ya kuhakikisha Ruto anakuwa Rais wa muhula mmoja, mbinu iliyotumiwa 2022 kumshinda Raila Odinga wa Azimio aliyeungwa mkono na Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta.

Baada ya kutofautiana na mkubwa wake na chama tawala cha Jubilee, Dkt Ruto, ambaye alikuwa Naibu Rais, aliwageukia wapiga kura wa Mlima Kenya kuuza chama cha UDA.Sasa Gachagua, baada ya kuondolewa madarakani Oktoba 2024, ameiga hatua hiyo kwa kulenga eneo hilo hilo akiahidi kukomesha ushawishi wa UDA.

Amedai kuwa eneo la Kati mwa Kenya limekatiza rasmi uhusiano wa kisiasa na Rais Ruto na halitamunga mkono katika uchaguzi wa 2027.

“Tumeachana na UDA. Hatutawahi tena kuingia uchaguzi bila chama chetu. Mara ya mwisho tuliingia harusi kwa gari la bwana harusi, lakini tulipofika mtoni, alituagiza tushuke na kuwapakia wengine,” alisema kwenye mahojiano ya runinga hivi majuzi.

DCP sasa imejitokeza kama chama kipya cha kisiasa kinachozungumza lugha ya kawaida inayolenga watu wa mapato ya chini.

“Wakenya wametuambia kwa ujasiri kuwa wana suluhisho la matatizo yanayowakabili. Wametutaka tuanzishe chama kitakachounda serikali ya watu kwa ajili ya watu,” alitangaza Gachagua wakati wa uzinduzi wa chama chake siku ya Alhamisi.

Kama alivyofanya Ruto hapo awali, Gachagua amekipanga chama chake kipya kama kinachosikiliza kilio cha wananchi wa kawaida.Alisema kuwa DCP itatoa kipaumbele kwa sauti za wananchi, kupitia kauli mbiu kama ‘Skiza Wakenya’ au ‘Skiza Ground’ (Sikiliza wananchi).

Aliyekuwa Naibu Rais aliongeza kuwa chama hicho kitazingatia ushirikishaji wa watu wote nchini, wakiwemo Gen Z, kizazi ambacho kimekuwa na ushawishi mkubwa tangu maandamano ya Juni 2024.

Nembo ya chama ni mkono ulioshika sikio, kuonyesha kusikiliza watu wa kawaida, huku rangi rasmi za chama zikiwa kijani, nyekundu, nyeupe na nyeusi.Ili kujipendekeza kwa wananchi zaidi, Gachagua alitangaza kuwa chama hakitafanya uteuzi wa wawaniaji kwa njia ya moja kwa moja.“Hatuna tunaopendelea.

Chama ni cha Wakenya wote. Ni watu wa Kenya watakaowachagua viongozi wanaowataka,” alisema.
 Aliongeza: “Chama hiki hakina nafasi ya uteuzi wa moja kwa moja. Kinaamini kuwa ni wananchi wanaopaswa kuamua. Nina viongozi wengi waliokuwa nami wakati wa dhiki — waliotembea nami kwenye safari ya kisiasa — lakini pamoja na kuwathamini, hakuna mwenye haki ya kuteuliwa moja kwa moja.”

Wachambuzi wa siasa wanasema hatua hiyo kama njia ya Gachagua kuonyesha kuwa Rais Ruto amewasahau watu walisimama naye licha ya dhuluma za kisiasa alizopitia kabla ya uchaguzi wa 2022.

“Anachofanya Gachagua ni ishara ya kisiasa — anajipanga kama mlezi wa ahadi ya mahsla,” alisema mchambuzi wa kisiasa Christopher Omore, ambaye ni wakili.

Aliongeza: “Kwa kuwavutia wale waliomuunga Ruto, anajaribu kwa ujanja kumsawiri Rais kama mtu aliyefaulu kwa msaada wa wananchi wa kawaida, kisha akawasahau mara tu alipopata mamlaka.”

Gachagua pia amejitosa kwenye chama chake kipya akiwa na baadhi ya watu waliokuwa na ushawishi mkubwa ndani ya UDA, akiwemo msemaji wa zamani na Katibu Mkuu Cleophas Malala, aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mithika Linturi na aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake Laikipia Cate Waruguru, ambao wote wametajwa kuwa maafisa wa chama.