Jamvi La Siasa

Gachagua alivyojitoa pumzi kususia mazishi ya Raila

Na BENSON MATHEKA October 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

Uamuzi wa aliyekuwa Naibu Rais, Rigathi Gachagua wa kutojitokeza katika ibada ya wafu ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga jijini Nairobi, Bondo, na hata kutoonekana kwake katika hafla ya umma ya kutazama mwili wa marehemu bungeni, umeendelea kuibua mjadala kuhusu athari zake kisiasa, kijamii na kimaadili katika kipindi cha maombolezo ya kitaifa.

Kifo cha Raila, ambaye alikuwa nembo ya mapambano ya demokrasia, kiliunganisha Wakenya kutoka pembe zote za nchi. Hata hivyo, hatua ya Gachagua kukosa kushiriki moja kwa moja katika matukio hayo imezua maswali kuhusu nafasi yake katika siasa za kitaifa na mustakabali wake wa kisiasa.

Katika mazishi yaliyohudhuriwa na viongozi wakuu akiwemo Rais William Ruto, aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta, viongozi wa upinzani, wanadiplomasia na wananchi wa kawaida, kutoonekana kwa Gachagua kulichukuliwa kama kujitenga na masuala muhimu ya kitaifa.

Kwa mujibu wa Seneta wa Kiambu, Karungo wa Thang’wa, Gachagua aliamua kuepuka hafla hizo kwa makusudi ili kuzuia mazishi hayo yasigeuke uwanja wa kisiasa. “Siku hiyo haikuhusu siasa, ilihusu Kenya kuungana kumuaga shujaa wa historia yetu,” aliongeza.

Hata hivyo, maelezo hayo hayakuwaridhisha wakosoaji wake. Naibu Gavana wa Kakamega, Ayub Savula, alimshutumu Gachagua kwa kile alichoita “uchungu wa kisiasa” uliomfanya ashindwe kutekeleza wajibu wa kimaadili.

“Hata kama una uchungu, Raila hawezi kufa halafu ushindwe hata kwenda kusaini kitabu cha rambirambi. Hasira ya aina gani hiyo?”

Maneno haya yalielezea hisia za sehemu kubwa ya wananchi na viongozi waliotafsiri kutokuwepo kwa Gachagua kama kukosa utu kisiasa na kutoheshimu utamaduni wa taifa wa kushiriki katika maombolezo ya viongozi wakuu.

Aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Kipruto arap Kirwa, pia alimtetea Gachagua, akisema alifanya uamuzi wa busara.

“Nadhani alifanya uamuzi sahihi. Kama angeenda uwanjani, kungeweza kuzuka lawama kutokana na historia ya kisiasa  kati yake na Raila,Kirwa alisema kwenye mahojiano ya runinga.

Kirwa alifafanua kuwa uhusiano wa kisiasa kati ya Gachagua na Raila ulikuwa wa mivutano, na uwepo wake ungezua mada tofauti na ya hafla hiyo.

Kwa mujibu wake, kutohudhuria kwa Gachagua hakukuwa ishara ya chuki, bali ya busara ya kisiasa na jaribio la kudumisha heshima ya tukio hilo la kihistoria.

Hata hivyo, wachambuzi wa siasa wanasema kwamba uamuzi huo, japo unaonekana wa kuepuka mivutano, umeacha doa la kisiasa kwa Gachagua ambaye alikuwa ameanza kupata ushawishi mkubwa baada ya kutimuliwa serikalini mwaka jana, tarehe ambayo mwili wa Raila ulikuwa unatazamwa Bungeni. Huku wengine wakisema kwa mtu wa hadhi ya Gachagua, kukosa kujitokeza katika tukio la kitaifa ni sawa na kujitenga na hisia za umma, kuna wanaohisi kuwa kufika kwake kungeibua kumbukumbu hasi kwake kwa kukutana ana kwa ana na waliomshtaki na kuunga kutimuliwa wake.

Wachambuzi wanasema kuwa uamuzi wa Gachagua kutohudhuria hafla hizo unaweza kuwa na athari kubwa kwake katika siasa za taifa.
Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya utawala, Prof Peter Kagwanja, Gachagua anaweza kupoteza uungwaji mkono wake kitaifa kwa kuonekana kukosa umoja na huruma.
“Huu ulikuwa wakati wa kuonyesha utu na umoja. Viongozi wanapokosa kuonekana katika nyakati kama hizi, ujumbe wanaotuma ni kwamba siasa ziko juu ya utu wa kibinadamu,” alisema Kagwanja.

Hali ilidorora zaidi kufuatia kauli za Gavana wa Kaunti ya Nyeri, anayotoka Gachagua, Mutahi Kahiga aliyoonekana kufurahia kifo cha Raila siku ambayo naibu rais huyo wa zamani alisemekana kupanga kuandamana na wazee wa Mlima Kenya kufariji familia ya Raila na kuzuru kaburi lake. Ingawa upinzani ulioungana unaojumuisha Gachagua ulijitenga na kauli za gavana huyo, Kahiga anachukuliwa kuwa mshirika wa kiongozi huyo wa chama cha Democratic Citizens Party (DCP).

Baadhi ya wachanganuzi wanasema kwamba hatua hiyo inaweza kuwa sehemu ya mkakati wa kisiasa wa kujitenga na hali ya kisiasa iliyojaa hisia, na hivyo kujipanga upya kwa mustakabali wake.

Kwa maneno ya Karungo wa Thang’wa “Kenya haisimami Gachagua akichagua kunyamaza; bali husikiliza kwa makini zaidi.”

Seneta huyo alisisitiza kuwa ukimya wa Gachagua haukuwa ishara ya udhaifu au kiburi, bali ulionyesha “hekima ya kisiasa, ustaarabu wa kihisia na heshima  wakati wa huzuni  taifa.”

Kwa mujibu wa Karungo, Gachagua alichagua kimya kwa makusudi ili kuhakikisha maombolezo ya Raila hayageuki kuwa jukwaa la siasa. Aliongeza kuwa hatua hiyo ilikuwa njia ya “kumheshimu shujaa wa taifa” bila kugeuza hafla hiyo kuwa tamasha la kisiasa,” alisema.

Lakini kwa wengine kama mchanganuzi wa siasa Tony Gachoka, hatua ya Gachagua si ishara ya hekima bali udhaifu wa uongozi.

“Ilikuwa kosa kutomtembelea Mama Ida, kutohudhuria hafla ya kitaifa—ilikuwa kushindwa kwa uongozi.”alisema Gachoka aliambia wanahabari wa Standard kwenye mahojiano wiki hii.