Jamvi La Siasa

Gachagua roho mkononi mashtaka dhidi yake yakiiva, wandani wakiwindwa na polisi

Na BENSON MATHEKA September 27th, 2024 3 min read

DHORUBA ya kisiasa inayotishia kumsomba Naibu Rais Rigathi Gachagua ilidhihirika wazi Alhamisi baada ya Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kupendekeza washirika wake wa karibu washtakiwe kwa kupanga maandamano ya vijana yaliyotikisa nchi.

Huku akionekana kumwelekezea kidole cha lawama Rais William Ruto, Bw Gachagua alilaani matumizi mabaya ya mfumo wa haki kulenga wandani wake kwa sababu ya misimamo ya kisiasa.

Alimkumbusha Rais Ruto kwamba, aliahidi Wakenya kuwa chini ya utawala wake, maafisa wa usalama hawatatumiwa kudhulumu watu kisiasa.

“Rais William Ruto na mimi, tulipoingia mamlakani, tulitoa ahadi kwa watu wa Kenya kwamba, kamwe mfumo wa haki hautatumiwa tena kushughulikia tofauti za kisiasa. Naona aibu tumerudi pale tulipokuwa. Unyanyasaji wa watumishi wa ofisi yangu na Wabunge wanaoonekana kuwa karibu nami umekuwa ukiendelea kwa muda wa miezi miwili iliyopita,” alisema.

Bw Gachagua alisema hayo baada ya DCI kupendekeza mashtaka dhidi ya watu watano wakiwemo Wabunge wawili kwa madai ya kuhusika katika maandamano ya kupinga serikali yaliyoongozwa na vijana mnamo Juni.

Alisema hatua hiyo ni kurudisha mbinu za kisiasa zilizopitwa na wakati, akieleza kuwa, Wakenya ni werevu sana kushindwa kuelewa kinachoendelea.

Katika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, DCI inapendekeza mashtaka dhidi ya wabunge Benjamin Gathiru Mwangi (Embakasi ya Kati) na James Mwangi Gakuya (Embakasi Kaskazini). Wengine ni George Theuri, Martin Deric, na Ngunjiri Wambugu ambao Bw Gachagua alisema ni wafanyakazi wa afisi yake.

“Hili ni jaribio la kuchafua jina langu na kutoa sababu za kuniondoa mamlakani,” alisema Bw Gachagua.

Wakati huo huo, joto la kisiasa linalomzunguka Gachagua limepanda kwa kiasi kikubwa huku mipango ya kuwasilisha hoja ya kumtimua ikisemekana kukamilika.

Zaidi ya wabunge 116 tayari wameripotiwa kuidhinisha hoja ya kumtimua kwa madai ya ukiukaji wa mara kadhaa wa Katiba.

Waandalizi walidokezea Taifa Leo kwamba, mashtaka hayo yanahusu ukiukaji wa Katiba na sheria zinazohusiana, utovu wa nidhamu uliokithiri na matumizi mabaya ya ofisi, hasa yakikitwa katika matamshi yake kama vile ‘serikali ya hisa’, ambayo ni sawa na kuwatenga Wakenya wengine.

Kulingana na baadhi ya wabunge wanaofahamu mchakato huo ulivyosukwa, rasimu ya mashtaka dhidi ya Geoffrey Rigathi Gachagua kama Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya imekitwa katika vifungu vya 73, 75, 79, 129 na 131 vya Katiba.

Baadhi ya makosa ya Gachagua ambayo yamemramba ni pamoja na kauli yake maarufu katika Kaunti ya Kericho Februari mwaka jana kuhusu umiliki wa hisa katika serikali ya Kenya Kwanza, madai ya siasa za migawanyiko, akisisitiza kuwa anazungumzia mlima pekee na kubagua maeneo mengine, ukiukaji wa usiri serikalini kuhusu shughuli za Baraza la Mawaziri.

Washirika wa Rais Ruto walikasirishwa na kauli ya Gachagua dhidi ya Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji, katika kilele cha maandamano ya Gen Z ambayo yalishuhudia uvamizi bungeni. Wanadai kuwa kauli yake ilihatarisha usalama wa Kenya.

Pia, anashutumiwa kwa kukosa kuheshimu afisi yake kwa kujitenga hadharani na uamuzi wa baraza la mawaziri kuhusu Mswada tata wa Fedha wa 2024, ambao uliondolewa. Badala yake, alisema alikuwa akisikiliza mashinani na kukiuka uwajibikaji wa pamoja wa Baraza la Mawaziri.

Mahojiano yake ya hivi majuzi na Citizen TV pia yamemtumbukiza motoni. Analaumiwa kwa kujaribu kunyakua mamlaka ya bunge kwa kuonya kuwa kumshtaki kungesababisha kukosekana kwa utulivu nchini.

Naibu Rais pia amekosolewa kwa shinikizo zake za kutaka raslimali zaidi, na kutetea mfumo wa ugavi wa mapato kwa kutegemea ‘mtu mmoja, kura moja, shilingi moja’, na hata kuwaita wanaompinga milimani ‘tukunia’.

Haya yanajiri huku ikibainika kuwa, washirika wa Rais Ruto walifanya mkutano katika hoteli moja ya Nairobi Jumanne usiku kujadili mkakati wa kumtimua Gachagua mamlakani.

Taifa Leo ilibaini kuwa, angalau wabunge 30 walihudhuria mkutano huo ulioongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot ambapo suala la kumvua Gachagua mamlaka lilijadiliwa.

“Ilikubaliwa kuwa ukusanyaji wa saini uanze, lakini kuwasilishwa kwa hoja na tarehe bado,” duru ziliambia Taifa Leo.

Mbunge wa Kimilili Didmus Baraza alithibitisha kuwa pia atatia saini kuunga mkono hoja hiyo.

Naibu Spika wa Bunge la Kitaifa, Gladys Shollei, ni miongoni mwa wanaotaka Bw Gachagua aonyeshwe mlango.

“Ninakuonya Rigathi Gachagua, utaondolewa mamlakani, ninaweza kukuthibitishia hili na nitasimamia hoja ya kukutimua,” alisema wikendi.

Kufikia sasa, baadhi ya wabunge ambao wamesimama waziwazi na Gachagua ni pamoja na Benjamin Gathiru MejjaDonk (Embakasi ya Kati), James Gakuya (Embakasi Kaskazini), Mary Wamaua (Maragua), Gathoni Wamuchomba (Githunguri), Amos Mwago (Starehe), Shadrack Mwiti ( Imenti Kusini), Susan Ngugi (Mbunge wa Kaunti ya Tharaka/Nithi), Joseph Munyoro (Kigumo) na Edward Muriu (Gatanga).

Wengine ni Treza Wanjiru (Maalumu), George Koimburi (Juja), Njeri Maina (Mbunge wa Kaunti ya Kirinyaga), Peter Kihungi (Kangema), Onesmus Ngogoyo (Kajiado Kaskazini).

Seneta John Methu (Nyandarua), Joe Nyutu (Muranga), James Murango (Kirinyaga), Lenku Seki (Kajiado) na John Kinyua (Laikipia).