Jamvi La Siasa

Gema wajumuisha rasmi Wakamba kwenye kundi lao, Ruto akipendezwa na umati Nyanza

Na MERCY SIMIYU, MOSES NYAMORI November 28th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

BARAZA la Wazee wa jamii za Mlima Kenya limejumuisha Wakamba katika muungano mkubwa wa Gikuyu, Embu, Meru (GEMA) katika mpango mpana wa kisiasa kufuatia miezi kadhaa ya kampeni kutoka kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Tangazo la kujumuisha rasmi jamii hiyo lilitolewa Jumatano katika hafla iliyofanyika katika All Saints Cathedral jijini Nairobi. Bw Musyoka na Bw Gachagua hawakuhudhuria mkutano huo, lakini washirika wao walisema walikuwa na baraka zao.

Mkutano huo ambao ulikuwa na mihemko ya kisiasa kufuatia kuondolewa ofisini kwa Bw Gachagua, ulijiri siku moja tu baada ya Rais William Ruto akiwa Kisumu kuwaonya viongozi dhidi ya ubaguzi wa kikabila. Bw Gachagua na Bw Musyoka walikuwa wameashiria nia yao ya kuwa na muungano imara zaidi kwa kuleta jamii zao pamoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Umepita muda mrefu sana tangu tulipoungana na ndugu zetu Wakamba. Hakuna kitu cha thamani zaidi kuliko kuungana tena na familia baada ya muda mrefu kama huo. Nyumba yetu husimamiwa na wazee, na ni wajibu wetu kuilinda. Kutunza nyumba yetu ni muhimu, na kunahakikisha nguvu na uendelevu wake,” akasema Bw Wachira Kiago, mwenyekiti Baraza la Wazee la Agikuyu.

Aliendelea, “Lazima tubaki kuwa chonjo na umoja, tusiruhusu kamwe wapinzani wetu wapande mifarakano au kudhoofisha msingi wa nyumba yetu.”

Rais William Ruto alipopokewa na umati mkubwa Kisumu Jumanne. Picha|PCS

Kwa miaka mingi, Gema imesalia kuwa muungano tata, huku wakosoaji wakichukulia kama ulioundwa hasa kuibua hisia za kikabila kulenga uchaguzi.

Wakati Rais Daniel Moi alipoingia madarakani mwaka wa 1978, mojawapo ya hatua zake kuu za kwanza za kukita mamlaka ilikuwa ni kuiondoa Gema iliyokuwa na nguvu wakati huo.

Alipiga marufuku mashirika yote ya kikabila na kusimamisha shughuli za kisiasa za muungano huo mkubwa wa jamii za eneo Mlima Kenya ulioongozwa na aliyekuwa mfanyabiashara tajiri na mwanasiasa Njenga Karume.

Akiwa Kisumu Jumanne, Dkt Ruto alionekana kushambulia viongozi ambao bado wanatumia jamii zao kama msingi wa kuwania nyadhifa za kisiasa. Alisema viongozi wanapaswa kukumbatia siasa za masuala kwa kuwaambia watu ni suluhu gani wanazotoa, badala ya kueneza mihemko ya kikabila.

“Wale ambao wana nia ya kuwagawanya Wakenya tu kwa misingi ya kikabila na kueneza chuki wataenda nyumbani. Serikali yangu haitaki wale wanaoabudu ukabila, chuki na migawanyiko. Ninawahakikishia, chini ya upendo wa Mungu, tutaunganisha nchi hii kuwa moja,” akasema Dkt Ruto.

Lakini wale wanaounga mkono muungano huo mpya walisema uamuzi wao ulitokana na hitaji la jamii jirani kusalia na umoja. Baadhi pia walisema kuwa Kenya imesalia kuwa ya kikabila, kwa hivyo watu hawafai kulalamika baadhi ya jamii zinapokutana kwa ajenda ya umoja.

Msemaji wa Baraza la Uongozi la Koo za Wakamba Davis Kithuka alisema msukumo wa kuwaunganisha Kamba ulianza tangu mwaka wa 2016.

“Hivi majuzi tulikutana na kufanya azimio la kusimama pamoja katika kila changamoto. Kuanzia wakati huo, tuliahidi kushikilia kila mmoja, bila kujali hali mbaya. Leo, tunafanya upya uhusiano huo—wenye nguvu zaidi, wenye umoja, na kujitolea kutembea njia hii pamoja hadi mwisho. Tutapitia kila kitu na ninamaanisha kila kitu,” alisema Bw Githuka.

Wakili Ndegwa Njiru katika ujumbe wa X kufuatia mkutano huo alisema, “Sisi ni taifa la makabila, na tutatumia ukabila wetu, tutatumia nguvu zetu za ukabila kujijenga, makabila yote yanapaswa kukutana na kuazimia kufanya kazi kwa pamoja ili kuondoa Zakayo kutoka Ikulu.”

Alikuwa akijibu ukosoaji kwamba miungano kama hiyo ina uwezo wa kugawanya nchi kwa misingi ya kikabila.

Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni pia alikaribisha uamuzi wa kutaka jamii ya Wakamba kujiunga na GEMA akisema kuwa itaimarisha muungano huo kuelekea uchaguzi ujao.

“Hiyo inamaanisha tunakua na tunafurahi ikiwa wameweza kufanya uamuzi huo na wanapaswa kuwasiliana na wengine,” Bw Kioni aliambia Taifa Leo.

Aliendelea: “Wanapaswa kuupanua hadi Kisii, kwenda kwa Waluhya, Mijikenda, Taita na kila mtu.”

Kuunganishwa kwa jamii ya Wakamba ni kichocheo kikuu kwa Bw Musyoka, ambaye amekuwa akifanya mikutano mikubwa ya kisiasa katika eneo hilo la Mlima lililo na kura nyingi.

Naibu Gavana wa Machakos, Francis Mwangangi, ambaye ni mshirika wa karibu wa Bw Musyoka, alisema ingawa aliyekuwa Makamu wa Rais hakuwepo, mkutano huo ulikuwa na baraka zake kamili.

“Tunaunga hatua hii. Ninaweza kukuambia kuwa yeye (Kalonzo) anahusika sana. Tunahitaji jamii imara ili kuhakikisha nchi ina mshikamano,” akasema Bw Mwangangi.

Wakati wa hafla hiyo, Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Ameru Josephat Murigira alisema uamuzi huo ni kuhakikisha jamii zinafanya maamuzi kama kambi pamoja na kuwa na nguvu ambazo ni muhimu katika uchaguzi.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA