Handisheki za vinara wa kisiasa ni sumu kwa wananchi
UKURUBA wa kisiasa kati ya Rais William Ruto na waliokuwa mahasimu wake katika uchaguzi mkuu wa 2022 kiongozi wa ODM Raila Odinga na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta hauna manufaa yoyote kwa raia inavyosawiriwa na washirika wa viongozi hao, wadadisi wa siasa na utawala wanasema.
Wanasema ushirikiano wa viongozi hao watatu ni sumu kwa demokrasia na haki za raia kwa kuwa watakuwa wakiunga sera za serikali ambazo zinawakandamiza raia wa kawaida.
Rais Ruto alianza kwa kuzika tofauti zake na Bw Odinga na kupitia ushirikiano wao washirika wa waziri mkuu huyo wa zamani wakajumuishwa katika serikali na wakaacha kuikosoa.Hali ilikuwa sawa mwaka wa 2018, Uhuru aliposalimiana na Bw Odinga aliyekuwa mpinzani wake katika uchaguzi mkuu wa 2017.
sumu kwa raia
“Handisheki za Dkt Ruto na Bw Odinga na ya hivi punde na Bw Kenyatta ni sumu kwa raia wa kawaida. Kwanza, zinaua upinzani na kuacha serikali bila sauti ya kuikosoa jambo ambalo ni hatari,” asema mchambuzi wa siasa
Dkt Isaac Gichuki.Anatoa mfano wa washirika wa Bw Odinga ambao wamejumuishwa serikali na bungeni ambao wameacha kukosoa sera za serikali ambazo walikosoa kabla ya handisheki ya kiongozi wao na Dkt Ruto.
“Ukisikiza kauli za viongozi wa ODM ambao kwa sasa ni mawaziri kama Hassan Joho (waziri wa madini) Opiyo Wandayi (Kawi), John Mbadi (Fedha) Wycliffe Oparanya (Ushirika) na Junet Mohamed (Kiongozi wa Wachache bunge la kitaifa) utaona jinsi handisheki hizi zilivyo hatari kwa demokrasia ya vyama vingi,” asema.
Wachambuzi wanasema lengo la wanasiasa hao sio kujali maslahi ya raia wanavyodai mbali ni kulinda maslahi yao na kuwaacha Wakenya wa kawaida peke yao.
“ Mradi Raila anaungwa mkono kwa wadhifa wa AUC na serikali, yeye na familia yake wako sawa na salama, hajali kwamba raia wanaumia kwa kubebeshwa mzigo wa gharama ya maisha. Umemsikia akitetea serikali hata kwa kwa kashfa kama sakata za Adani ambazo zilifutwa baada ya Amerika kuanika kampuni hiyo ya India,” asema mchanganuzi wa siasa James Warukira.
Akitaja handisheki hizi kama sumu kwa demokrasia kwa demokrasia ya vyama vingi Kenya, Warukira anasema zinaua upinzani huku “ wanasiasa wakiungana kulinda tabaka lao.”
Mwelekeo mbaya
“Ni mwelekeo mbaya unaohusisha tabaka la wanasiasa. Kwanza, handisheki hizi ni sumu ya kuua upinzani. Bila upinzani wenye nguvu, serikali inaweza kufanya chochote ikiwemo kukiuka haki za raia.
Hii ndiyo sababu hakuna mwanasiasa anayegeemea vinara wa handisheki anayekosoa serikali kwa kubebesha raia ushuru na kutoleshwa raia. Hakuna anayejali raia wanapokosa matibabu kwa sababu ya kuvurugika kwa mfumo wa bima ya afya na hakuna anayejali kwamba matatizo ya akili yamelemea raia kutokana na mapato kupungua,” asema Warukira.
Dkt Simon Odhiambo, mtaalamu wa utawala anasema japo handisheki za wanasiasa zinasemekana kutuliza nchi wakati wa joto la kisiasa, zinakuza ukabila huku vinara wakisawiri jamii zao kama zinazopatana.
“ Salamu hizi za wanasiasa zinapalilia ukabila. Wanajenga taswira ya kupotosha kwamba wanaposalimiana ni jamii zao zinazosalimiana na kutenga zile ambazo viongozi wao wanakataa kujiunga nao,” asema Odhiambo.Anasema mbali na kukuza ukabila zinagawanya nchi kimaeneo.
“Umesikia kila kiongozi anayeegemea vinara wanaosalimiana akiambia wakazi wa eneo analotoka kwamba ukuruba wa Raila na Ruto au Uhuru utafanya maeneo yao kupata maendeleo. Kwamba kuwa serikalini ndio hakikisho la kupata maendeleo kumaanisha wale wanaobaki katika upinzani wanatengwa kana kwamba maeneo yao yako nje ya mipaka ya Kenya,” asema.
Dkt Gichuki anasisitiza kuwa ukuraba wa viongozi hao wakuu ni wa kulinda maslahi yao na sio ya kusaidia raia wa kawaida.