Jamvi La Siasa

Hasira za Mlima zilivyozima ziara ya Ruto Embu Jumapili

Na CHARLES WASONGA October 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa Mlima Kenya sasa wameonekana kumkataa Rais William Ruto kwa kukosa kumnusuru naibu wake Rigathi Gachagua anayekabiliwa na hatari ya kutimuliwa afisini na maseneta wiki hii.

Aidha, wamekuwa wakiwazomea hadharani wabunge waliopitisha hoja ya kumtimua Gachagua afisini katika Bunge la Kitaifa Jumanne wiki iliyopita.

Ili kujiepusha na hasira za wakazi hao, Rais Ruto Jumamosi jioni alifutilia mbali ziara yake katika kaunti ya Embu ambako Jumapili aliratibiwa kuhudhuria maadhimisho ya miaka 34 tangu kuanzishwa kwa dayosisi ya Embu ya Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK).

Awali, Mbunge wa Manyatta Gitanga Mukunji alikuwa amethibitisha kuwa Dkt Ruto alipaswa kuwa mgeni wa heshima katika sherehe hiyo katika Chuo cha Mafunzo ya Walimu cha Kigari, kilichoko eneo bunge lake.

“Hii sherehe inafanyika katika eneo bunge langu. Rais ndiye mgeni mheshimiwa. Endapo hatafika, bila shaka atawakilishwa na naibu wake,” Bw Mukunji akaambia Taifa Leo.

Jana, Rais Ruto alifichua mbele ya waumini wa Kanisa la AIC Milimani, Nairobi, kwamba hakuwa amepanga kuungana nao kwa ibada ya Jumapili bali aliratibiwa kuhudhuria kwingineko.

“Nilikuwa nimeratibu kwenda kwingine. Ilinilazimu kujadiliana na watu maeneo mengine kwa sababu sikutaka kukosa sherehe hii,” Rais Ruto akasema.

Ibada hiyo iliandaliwa mahsusi kuadhaminisha miaka 30 tangu kujengwa kwa kanisa hilo la AIC Milimani.

Sherehe ya ACK, Embu, hata hivyo, ilihudhuriwa na Bw Gachagua na mkewe Pasta Dorcas huku maswali mengi yakiibuliwa kuhusu kudorora kwa uhusiana kati ya Rais na naibu wake.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba ziara ya Rais Ruto Embu ilifutiliwa dakika za mwisho kwa sababu hakutaka kushiriki jukwaa moja na naibu wake.

Rais, ambaye amechelea kuzungumzia suala ka kutimuliwa kwa Bw Gachagua tangu Oktoba 3, 2024, angeonekana hadharani na naibu wake endapo angehudhuria hafla ya ACK Embu.

Huku akionekana kung’amua kuwa wakazi wa eneo hilo wamekasirishwa na mchakato wa kubanduliwa kwake, Bw Gachagua aliwashauri kudumisha utulivu na kukoma kuzuia fujo pasina kuzingatia uamuzi wa Seneti kuhusu suala hilo.

Aliwaomba Wakenya wamuombee na taifa wakati huu ambapo joto la kisiasa limepanda nchini baada ya wabunge kupitisha hoja ya kumtimua wiki jana.

“Licha ya yale yanayofanyika nchini, ombi langu ni kwamba tudumishe amani. Mungu ndiye yuko mamlakani. Tuhubiri amani bila kuzingatia matokeo ya hoja hii. Kenya ni nchi yetu,” akasema.

Bw Gachagua alielezea imani kuwa Mahakama itaamua suala hilo kwa njia ya haki endapo litafikishwa huko.

Wabunge wandani wa Rais Ruto wanapitia wakati mgumu katika maeneo ambako Bw Gachagua anaungwa mkono kwa wingi.

Mnamo Ijumaa wakazi wa eneo bunge la Bahati, Kaunti ya Nakuru walimzomea Gavana Susan Kihika alipojaribu kusoma risala za rambirambi za kutoka kwa Rais Ruto wakati wa mazishi ya kakake mbunge wa eneo hilo Irene Njoki, Henry Gachie.

Wabunge George Kariuki (Ndia), Anne Wamuratha (Kiambu), Oscar Sudi (Kapseret), James Githua (Kabete) na Betty Maina (Mbunge Mwakilishi wa Murang’a) walizimwa kuwahutubia waombolezaji waliowazomea vikali.

Hawa ni miongoni mwa wabunge 281 waliopiga kura ya NDIO kuunga mkono hoja ya kutimuliwa kwa Gachagua inayodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

Endapo hoja hiyo itaungwa mkono na angalau maseneta 45 kati ya 67 (thuluthi mbili), Bw Gachagua atakuwa ameondolewa rasmi kutoka wadhifa wa Naibu Rais wa Jamhuri ya Kenya.