Hatuachi Raila hata mkinuna, viongozi wa Mulembe waambia Gen Z
CHAMA cha ODM kinaonekana kuanzisha juhudi za kufungia vyama vingine nje ya Magharibi mwa Kenya baada ya viongozi wa chama hicho kuahidi kutokiacha kwa kuendelea kumuunga Raila Odinga.
Haya yanajiri huku kukiwa na shinikizo kutoka kwa sehemu ya vijana mitandaoni maarufu Gen Z wanaotaka Raila kutoungwa mkono kwa wadhifa wa AUC wakimwita msaliti kwa kukubali minofu serikalini ili kuzima maandamano ya kulalamikia uongozi mbaya.
Badala yake, wanataka mwaniaji wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf ashinde kiti hicho ‘ili iwe funzo kwa Raila’.
Lakini viongozi kutoka ukanda wa Magharibi wameahidi ‘kusimama’ na Bw Odinga wakimwombea dua afaulu kwenye azma yake ya kuwania hicho cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Na iwapo Bw Odinga atalambishwa sakafu kwenye kinyang’anyiro hicho cha Februari mwakani, wabunge hao wamesisitiza kuwa eneo hilo ‘litasimama’ naye kisiasa hadi uchaguzi mkuu wa 2027.
‘Hakuna kinachobadilika’
“Hapa Vihiga na Magharibi nzima ni ngome ya Raila na hakuna kile ambacho kitabadilika akienda AUC ama asipoenda. Chama chetu cha ODM kitasalia kipenzi chetu hapa na lazima tuendelee kukijenga,” akasema Gavana wa Vihiga Wilber Otichillo.
Alikuwa akizungumza mnamo Jumapili kwenye hafla ya kumkaribisha Seneta wa Vihiga Geodfrey Osotsi nyumbani baada ya kuteuliwa naibu kiongozi wa ODM.
Mbali na Bw Osotsi, manaibu viongozi wengine ni Gavana wa Kisii Simba Arati na mwenzake wa Mombasa Abdulswamad Nassir. Viongozi waliohutubu katika hafla hiyo walisema kuwa Magharibi haina nafasi katika vyama vingine na ODM itaendelea kupanua mawanda yake katika kaunti za Bungoma, Busia, Kakamega na Vihiga ikilenga kunyakua viti vyote.
“Hapa Magharibi ni ODM. Kila mara taabu ikitokea Kenya ni Raila anatafutwa na hapa Magharibi tunajivunia kuwa amekuwa kiongozi wetu,” akasema waziri wa zamani Fred Gumo ambaye pia alihudumu kama mbunge wa Westlands, Nairobi kwa miaka mingi.
Bw Gumo aliwaambia wakazi wa Magharibi kuwa hakuna haja ya kuendelea kung’ang’ania vyama vidogo ilhali kwa miaka yote hii wamejenga ODM na kuunga azma ya Bw Raila.
ODM ikitawala siasa za Magharibi
ODM imekuwa ikitawala siasa za Magharibi tangu ibuniwe mnamo 2005 huku wakazi wa ukanda huo wakimpigia Bw Raila kura hata wakati ambapo Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi aliwania urais kupitia ANC mnamo 2013.
Bw Mudavadi amekubali kuvunja ANC ili ijiunge na UDA huku Ford Kenya ambayo anaongaza Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ikiwa na ufuasi mkubwa katika Kaunti ya Bungoma.
“Raila ana wafuasi ambao wako tayari kufa kwa ajili yake na ninakuhakikishia kuwa hapa Magharibi huwa umeungwa mkono kwa asilimia 90 kwa miaka mingi na itapanda zaidi.
“Hatutakubali kugawanywa na vyama vidogo vidogo na atakayejaribu hilo sisi wazee tutawaonyesha njia. Kama jamii ya Mulembe tuko pamoja nyuma ya Raila na wengine wote ni punda,” akasema Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi (COTU), Francis Atwoli.
Katibu huyo alikuwa mwandani wa Bw Odinga kuelekea uchaguzi wa 2022 lakini baada ya waziri huyo mkuu wa zamani kukosa urais, alirukia mrengo wa serikali ukiongozwa na Rais William Ruto.
Wawili hao walijibizana vikali mnamo Septemba 2, 2023 katika mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa Cotu Rajab Mwondi, Vihiga.
Atwoli kutelekeza wafanyakazi
Kwenye mazishi hayo, Raila alimshutumu vikali Bw Atwoli kwa kutelekeza wafanyakazi na kushirikiana na Rais Ruto.
Wakati huo alisema Bw Atwoli alistahili kuendeleza maasi dhidi ya serikali kwa sababu wafanyakazi walikuwa wanaumia kiuchumi.
Bw Atwoli naye alimjibu akisema kuwa Bw Odinga anastahili kukubali kuwa alibwagwa na Rais Ruto na kuendelea na kazi yake ya upinzani.
Hafla ya kusherekea uteuzi wa Bw Osotsi pia ilihudhuriwa na Gavana wa Bungoma Kenneth Lusaka, mbunge wa Hamisi Charles Gimose, na mbunge wa Kiminini Didmus Barasa ambao wote ni wandani wa Bw Wetang’ula.
Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Kakamega Elsie Muhanda alisema hakuna chama chochote ambacho kitafunika ODM katika ukanda wa Magharibi kwa sababu Raila ameweka msingi imara na kuna viongozi chipukizi watakaoivumisha.
“Raila amesimama na watu wa Magharibi na hata saa hii amemteua Wycliffe Oparanya serikalini. Sisi tunasonga mbele na Raila na hatuelekei popote ashinde AUC au asishinde,” akasema Bi Muhanda.
ODM ‘inatwaa viti vingi 2027’
Wabunge Caleb Amisi (Saboti), Tim Wanyonyi (Westland), Wilberforce Oundo (Funyula), Emmanuel Wangwe (Navakholo), George Aladwa (Makadara), Raphael Wanjala (Budalang’i), Oku Kaunya (Teso Kaskazini) Beatrice Elachi (Dagoretti Kaskazini) Peter Nabulindo (Matungu) miongoni mwa wabunge wengine, waliahidi kuhakikisha kuwa ODM inatwaa viti vingi 2027 Magharibi iwe Raila bado atakuwa AUC au kwenye siasa za nchi.
“Hapa Magharibi ni ODM na hatubanduki hata sisi kule Nairobi tumeshikilia chama. Hapa Mulembe tuna hisa kubwa hapa ODM na Raila ajue ODM itakuwa imara hata akienda AUC,” akasema Bw Wanyonyi.
“Sisi Busia ndiyo tuko wengi ODM na tunasubiri hatima ya Raila AUC. Hakuna pengo katika chama na Magharibi bado tutakuwa nyuma ya Raila,” akasema Bw Oundo.