Jamvi La Siasa

Hekima ya Marende kuhusu maamuzi bungeni yamhepa Wetang’ula

Na DAVID MWERE February 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HALI ambayo Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula alijipata alipohitajika kuongoza nchi kuhusu suala la upande wa walio wengi katika Bunge si geni katika historia ya Bunge.

Kwa mfano, mnamo Aprili 28, 2009 aliyekuwa Spika wakati huo, Kenneth Marende alitoa uamuzi kuhusu nani alikuwa kiongozi wa shughuli za serikali Bungeni na hivyo basi mwenyekiti wa Kamati ya Shughuli za Bunge (HBC) katika Serikali ya Muungano.

Spika Marende alikuwa ametakiwa kutoa mwongozo na aliyekuwa Mbunge wa Kisumu Mjini Magharibi Olago Aluoch siku tano zilizotangulia.

Hii ilikuwa baada ya chama cha aliyekuwa rais wakati huo Mwai Kibaki cha PNU na ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kuwasilisha mwanachama kwa wadhifa huo muhimu kwa shughuli na uongozi katika Bunge.

Hatua hii ilimaanisha kwamba Bunge halingeweza kuendesha shughuli bila HBC, ambayo inaweka ajenda na uongozi wa shughuli bungeni. Ingawa ilikuwa ni matarajio ya wengi kwamba Spika Marende angeamua wadhifa ungeendea mmoja wa hao wawili walioteuliwa na vyama vilivyokuwa vikivutana, haikuwa hivyo.

“Kwa masikitiko makubwa, natoa uamuzi kwamba Spika wa Bunge, atakuwa mwenyekiti wa kamati hadi pale Spika atakapopokea, jina la mtu mmoja aliyependekezwa na serikali kwa wadhifa wa mwenyekiti wa Kamati ya Shughuli za Bunge,” Bw Marende alisema.

Spika, chini ya Kanuni za Kudumu za Bunge, ni mwanachama wa kamati hiyo. Kisha Mbunge wa Eldoret Kaskazini ambaye alikuwa pia Waziri wa Kilimo William Ruto, ambaye sasa ni rais, aliunga mkono uamuzi wa Bw Marende.

“Ninaungana na wenzangu kukupongeza kwa msimamo uliochukua alasiri hii wa kutoa mwongozo kwa Bunge hili ambalo limekuwa na mvutano kwa muda wa wiki moja iliyopita,” Bw Ruto alisema wakati huo alipokuwa bungeni.

Pia alimkosoa aliyekuwa mbunge wa Juja George Thuo kwa kusawiri bunge kama serikali na upinzani.

“Amezungumza kuhusu pande mbili za Bunge mara mbili. Tunazungumzia serikali moja! Hakuna pande mbili za bunge. Hakuna upinzani na upande wa serikali. Kwa hivyo, anapaswa kusahihisha hilo kulingana na uamuzi wako,” Bw Ruto alisema.

Mbunge wa Mugirango Kusini Omingo Magara ambaye alikuwa Waziri Msaidizi wa Biashara wakati huo alisifu uamuzi huo. “Mtu fulani alisema kwamba walitafuta mtu mwenye busara ambaye aliokoa maisha ya mtoto. Ninataka kukukumbusha leo, Mheshimiwa Spika, kwamba mtu aliyekuwa akinukuliwa wakati huo alikuwa Suleimani na ninataka kukuambia kwamba umekuwa Suleimani wetu leo katika nchi hii,” akasema Bw Magara.

Siku chache tu baada ya uamuzi wa Bw Marende, Bw Kibaki na Bw Odinga walikutana na kukubaliana kuhusu jina la Kalonzo Musyoka walilowasilisha bungeni kupitia barua kwa Spika na likapitishwa bila mvutano.

Huku Bw Marende akipongezwa kwa kutoa uamuzi wa hekima ambao ulisuluhisha kwa amani mzozo mkali kati ya PNU na ODM, Spika Wetang’ula ametoa maamuzi mawili kuhusu upande wa wengi katika Bunge ambayo yamezua mgawanyiko. Mnamo Oktoba 6, 2022, baada ya uchaguzi mkuu uliofuatiwa na maandamano makubwa ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022, Spika Wetang’ula alitangaza muungano wa Rais William Ruto wa Kenya Kwanza kuwa wa wengi katika Bunge.

Licha ya mahakama kutangaza uamuzi huo ulikuwa kinyume cha katiba, Bw Wetang’ula mnamo Februari 11, 2025 alisisitiza kwamba Kenya Kwanza ni muungano wa wengi hatua ambayo imemfanya asutwe vikali na wabunge wa Azimio la Umoja One Kenya