Jamvi La Siasa

Ishara handisheki ya Uhuru na Gachagua inanukia

Na BENSON MATHEKA September 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA tukio linaloashiria mabadiliko makubwa ya kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua wameanza kuonyesha ishara za wazi za kushirikiana tena kisiasa.

Hii ni baada ya vyama vyao, Jubilee Party na Democratic Citizens Party (DCP), kumuunga mkono mgombea mmoja wa upinzani katika uchaguzi mdogo wa ubunge wa Mbeere Kaskazini, unaotarajiwa kufanyika Novemba 27 2025.

Hii ni mara ya kwanza kwa wawili hao kuonekana wakielekea upande mmoja wa kisiasa tangu tofauti zao kali kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Wakati huo, Uhuru Kenyatta aliunga mgombea urais wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga huku Rigathi Gachagua akiwa miongoni mwa viongozi wakuu waliomuunga mkono Dkt William Ruto, ambaye hatimaye aliibuka mshindi na kuwa Rais wa sasa wa Jamhuri ya Kenya.

Hatua ya sasa ya Jubilee na DCP kumuunga mkono mgombea wa pamoja wa upinzani, Newton Karish wa chama cha Democratic Party (DP) imezua hisia katika duru za kisiasa, hasa ikizingatiwa kuwa Mbeere Kaskazini ni mojawapo ya maeneo yaliyo ndani ya ngome ya kisiasa ya wawili hao ya Mlima Kenya.

DP inaongozwa na aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi aliyetimuliwa na Rais William Ruto akihudumu kama Waziri wa Utumishi wa Umma.

Sawa na Bw Gachagua, Muturi alikuwa mwandani wa Bw Uhuru kabla ya kutofautiana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Tangazo lilitolewa na Pauline Njoroge, Naibu Katibu Mratibu wa Jubilee Party, ambaye alisisitiza kuwa chama hicho hakitatoa mgombea wake bali kitaunga mkono jitihada za upinzani kuwasilisha mgombeaji wa pamoja ili kuimarisha mshikamano, limechukuliwa kama hatua ya kwanza ya Uhuru kuzika tofauti zake za kisiasa, sio tu na Bw Gachagua bali pia na Bw Muturi.

“Chama cha Jubilee hakitatoa mgombea katika uchaguzi wa Mbeere Kaskazini. Tutaunga mkono mgombea mmoja wa upinzani kwa nia ya kuimarisha mshikamano na kuonyesha umoja wetu mpya wa kisiasa,” alisema Njoroge.

Kwa upande wake, Rigathi Gachagua kupitia kikao cha NEC cha chama cha DCP alitangaza kuwa chama chake kitaunga mkono wagombea wa vyama rafiki katika chaguzi ndogo tatu: Mbeere Kaskazini, Muumbuni (Machakos), na Kabuchai/Chwele (Bungoma).

Katika Mbeere, DCP itaunga mkono mgombea wa DP, Muumbuni itaunga mkono mgombea wa chama cha Wiper, na katika Kabuchai/Chwele, itaunga mkono DAP-K.

Uamuzi huu ulizua malalamishi ndani ya DCP, ambapo mwaniaji aliyetarajia tiketi ya chama hicho, Duncan Mbui, alijiuzulu na kuhamia Chama cha Kazi kinachoongozwa na Moses Kuria.

Kiti cha Mbeere Kaskazini kilibaki wazi baada ya aliyekuwa mbunge, Geoffrey Ruku, kuteuliwa na Rais Ruto kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma.

Kwa hivyo, kinyang’anyiro hicho sasa kinatarajiwa kuwa na wagombea watatu wakuu ambao ni Newton Karish (DP),anayeungwa mkono na Jubilee na DCP, Leonard Muriuki (UDA) na Duncan Mbui (Chama cha Kazi).

Ushirikiano wa Jubilee na DCP katika eneo la Mlima Kenya, ambalo limekuwa uwanja wa mapambano ya kisiasa tangu uchaguzi wa 2022, unatazamwa kama hatua muhimu ya kisiasa.

Wachambuzi wa siasa wanaona hatua hii kama mwanzo wa upatanisho kati ya kambi za Uhuru na Gachagua ambazo zilikuwa mahasimu wakubwa miaka mitatu iliyopita.

“Pia, kuna hisia kuwa huu huenda ni mwanzo wa mazungumzo mapana ya kisiasa kati ya Uhuru na Gachagua kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027, ambapo vyama vyao na upinzani kwa jumla vitaungana ili kutoa ushindani thabiti kwa serikali ya Kenya Kwanza,” asema mdadisi wa siasa Dkt Isaac Gichuki.

Anasema hii ni hali ambayo haikutarajiwa na wengi, ikizingatiwa hakukuwa na mazungumzo yaliyoripotiwa kati ya Uhuru na Gachagua waliotofautiana vikali kisiasa.

“Inaweza kuchukuliwa kuwa sasa wanatengeneza njia ya kurudi katika meza moja ya kisiasa, kwa lengo la kuimarisha ushawishi wao ndani ya Mlima Kenya, na hata kitaifa,” asema.