JIFUNZE LUGHA: Mazingira ambapo {ni} hutumiwa kutoa amri
KATIKA sehemu ya pili ya msururu wa makala haya, tuliondolea mbali dhana kwamba {ni} inaweza kutumiwa kama kiambishi maalumu cha kutoa amri.
Nilieleza kuwa suala la amri au rai sharti liwe mtambuko au likate kuwili.
Yaani, haiwezekani amri kutolewa katika hali ya wingi tu. Rafiki yangu na ashiki mkubwa wa safu hii, Bw Kanyai, alitaja neno ‘tokeni!’ akitaka kufahamu iwapo ni kweli kuwa kiambishi {ni} kinatekeleza dhima ambayo tumekwisha kuitaja.
Nilitamatisha sehemu ya pili ya makala kwa kueleza kuwa yamkini dhana ya amri katika neno hilo inadhihirishwa kwa kiimbo ambapo alama ya hisi inashadidia suala hilo.
Katika mazingira mengine ya kisarufi, rai, himizo au amri huibuliwa na kiambishi {e} kinachojiri mwishoni mwa baadhi ya vitenzi vya Kibantu kwa mfano ‘utoke’, ‘uondoke’, ‘umwambie’, ‘aelezwe’ na kadhalika.
Ifahamike kuwa maneno hayo yawapo katika hali ya kutenda ambayo ndiyo hali ya kawaida ya vitenzi vyote, huishia kwa kiambishi {a} ambacho si sehemu ya mzizi wa kitenzi kwa kuwa ni kawaida vitenzi vingi vya Kibantu kuishia kwa kiambishi hicho.
Kosa moja ambalo wazungumzaji wengi wa lugha ya Kiswahili hulifanya ni kukitumia kiambishi {ni} hata katika mazingira ya umoja.
Hebu tazama mfano ufuatao: *“Bwana Ondiek, asanteni sana kwa kuja,” baba alimshukuru mgeni wake. Waama, iwapo kauli hii inamlenga Ondiek pekee basi ni kosa kutumia {ni} mwishoni mwa neno ‘asante’.
Kwa maoni yangu, hakuna kiambishi {ni} cha kutoa amri wanavyodai baadhi ya waandishi!