Jinsi ‘Tawe Movement’ inavyofanya iwe vigumu kwa Ruto kuchota kura za Mulembe kwa urahisi
HUENDA ikawa mlima kwa Rais William Ruto kuimarisha ushawishi wake eneo la Magharibi baada ya kupoteza Mlima Kenya kutokana na hatua yake ya kutengana na aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua.
Licha ya kumweka makwapani kinara wa chama cha ODM Raila Odinga ambaye amekuwa akipata kura nyingi eneo hilo, juhudi za viongozi vijana kutoka jamii ya Mulembe zinaweza kuwa kikwazo kwa Rais Ruto kuongeza umaarufu wake Magharibi mwa Kenya.
Viongozi hao vijana wanaonekana kuungana chini ya mwavuli wa vuguvugu la Tawe Movement linalohusishwa na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya wakiwalaumu vigogo wa kisiasa kutoka magharibi kwa kutosaidia jamii ya Mulembe.
Baadhi ya wabunge wa chama cha ODM kutoka Magharibi tayari wameanza kuonya kuwa itakuwa vigumu kwa jamii ya Mulembe ‘kuuzwa’ kwa Rais Ruto.
“Ni wazi kuwa Rais Ruto anaelekeza juhudi zake eneo la Magharibi kwa kuwa kutofautiana kwake na Bw Gachagua kunaweza kumnyima kura za Mlima Kenya. Hata hivyo, kuna ishara kwamba ili kuzoa kura za eneo hilo kwa wingi, atahitaji kufanya mengi zaidi kwa kuwa kuna upinzani mkubwa mashinani ambao ulianzishwa na vuguvugu la Tawe,” asema mdadisi wa siasa za Magharibi Peter Wafula.
Bw Natembeya amewahi kukutana na viongozi vijana kutoka jamii ya Mulembe kutoka vyama tofauti na kueleza kuwa vuguvugu lake litapigania maslahi ya eneo la Magharibi.
“Kwa wakati huu, sitafanya mikutano ya kisiasa na badala yake nitazungumza na viongozi wa mashinani kusikia kauli zao kuhusu masuala ambayo Tawe inasimamia. Masuala haya ni pamoja na umaskini, ukosefu wa usawa katika utawala na kunyimwa haki za kimsingi kama elimu na afya,” Bw Natembeya alinukuliwa akisema katika mahojiano.
Bw Wafula anasema akiwa mwanachama wa DAP K kinachoongozwa na kinara mwenza wa Azimio Eugene Wamalwa, pamoja na umaarufu wa Tawe mashinani eneo la Magharibi, na jina lake kutajwa kitaifa, huenda mpango wake ukatatiza juhudi za Dkt Ruto eneo la Magharibi.
Mbunge wa Saboti (Mbunge) Caleb Amisi amemuonya Rais Ruto kujiandaa kwa wakati mgumu eneo la Magharibi kuelekea uchaguzi wa mwaka wa 2027.
Kupitia akaunti yake rasmi ya X mnamo Jumatatu wiki hii, Bw Amisi alisema Rais Ruto anapanga mikakati ya kupata kura za jamii ya Mulembe lakini haitakuwa rahisi.Kulingana na mbunge huyo Rais Ruto anajaribu kuwavutia wapigakura Magharibi mwa Kenya kupitia madalali wa kisiasa.
Hii, Amisi anasema, ni kwa sababu si rahisi kushawishi wapigakura wa maeneo mingine tofauti na eneo la Magharibi mwa Kenya.Hata hivyo, mbunge huyo anaonya kuwa mpango huo hautakuwa rahisi jinsi Rais alivyofikiria, akisema kuwa eneo la Magharibi mwa Kenya halitapigwa mnada kisiasa.
‘Ruto anataka kura za Magharibi katika uchaguzi ujao kwa bei ya kutupa kupitia mabroka wa kisiasa, kwa sababu kura za Wakikuyu zina bei. Naam, fikiria mara mbili. Vindu vichenjanga (mambo yanabadilika). Magharibi haitakuwa mteremko’ Amisi alisema.Rais Ruto amedumisha washirika wakuu wa kisiasa kutoka eneo la Magharibi katika serikali yake.
Wao ni Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula ambaye chama chake cha Ford Kenya ni mwanachama wa muungano wa Kenya Kwanza na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni na Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani. Kwa wakati huu, wawili hao ndio viongozi wakuu serikalini kutoka jamii ya Mulembe.
Waziri wa Ushirika Wycliffe Oparanya ni kiongozi wa hivi punde kutoka jamii ya Mulembe kujiunga na serikali katika juhudi za Rais Ruto kuimarisha ushawishi wake eneo hilo.
Dkt Ruto pia ameimarisha ziara zake eneo hilo ya hivi punde ikiwa Novemba 10, 2024, ambapo alihudhuria ibada katika Kaunti Ndogo ya Khwisero, Kaunti ya Kakamega.