Kanda ya siri iliyovunja kabisa uhusiano kati ya Ruto na Gachagua
MWENDO wa usiku Agosti 30, Naibu Rais aliyeondolewa afisini Rigathi Gachagua aliwasili katika mkahawa wa Acacia Premier mjini Kisumu.
Hii ni baada ya kushinda mchana kutwa akiandamana na bosi wake, Rais William Ruto, katika ziara ya eneo la Luo Nyanza.
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwa viongozi hao wawili kupata mapokezi mazuri mjini Kisumu tangu uchaguzi mkuu wa 2022.
Hii ni kutokana na kuimarika kwa uhusiana kati yao na mpinzani wao mkuu, Raila Odinga ambaye ni kigogo wa siasa katika eneo hilo.
Hii haikuwa mara ya kwanza kwa Bw Gachagua kutembelea mkahawa huo wa kifahari wenye vyumba mahsusi vilivyotengewa wageni wa hadhi ya rais (Presidential Suites).
Kwa mfano, mnamo Januari mwaka huu, katika akaunti yake ya mtandao wa X, Acacia Premier Hotel iliweka picha ya Bw Gachagua akiwa humo pamoja na Meneja wake Mkuu Shanawaz Basheer.
Na jioni mnamo Agosti 30, Mbunge mmoja kutoka Rift Valley aliungana na Naibu Rais katika mkahawa huo. Mbunge huyo anachukuliwa kuwa mwandani wa Gachagua kwani alimtetea Julai mwaka huu mjadala wa kumtimu ulipochipuza kwa mara ya kwanza.
Awali, mbunge huyo amewahi kuendesha kampeni za kumpinga Dkt Ruto na akapata bahati ya kuibuka mshindi baada ya kumshinda mwaniaji aliyeungwa mkono na Rais.
Mbunge huyo aliketi na Bw Gachagua katika chumba chake kwa saa kadha wakipiga gumzo walilodhani lilikuwa la siri.
Lakini iliibuka kuwa mtu fulani alikuwa akisikiza mazungumzo hayo akiwa chumba kingine kwenye mkahawa huo huo.
Siku moja kabla ya Gachagua kuwasili katika mkahawa huo, maafisa wa usalama na itifaki walitangulia na kukodi chumba hicho.
Maafisa hao walifanya mipango yote ikiwemo ya kukagua hali ya usalama katika mkahawa huo ambapo mgeni huyo mashuhuri angelala.
Wageni wengine mashuhuria walipewa vyumba vya juu ya orofa ya chumba cha Bw Gachagua.
Saa chache kabla ya Gachagua kuwasili, mlinda usalama wake mmoja alifanya ukaguzi kuhakikisha chumba hicho ni salama.
Duru zilisema kuwa usiku huo, mbunge huyo alifanya mazungumzo na Gachagua kwa saa kadhaa kabla ya kuelekea katika chumba chake.
Usiku huo sasa umegeuka kuwa wa usaliti wa Gachagua na watu aliowaamini.
Hakujua kuwa watu fulani ambao hawakuwa katika chumba chake walikuwa wakirekodi mazungumzo yake na mbunge huyo kutoka Bonde la Ufa.
Imeibuka kuwa rekodi ya mazungumzo hayo sasa ndio chimbuka la uhasama kati ya Bw Gachagua na Rais Ruto.
Jumapili, Oktoba 20, 2024 Bw Gachagua alipoondoka Hospitali ya Karen, alifichua kuwa maajenti wa shirika la kitaifa la ujasusi (NIS) waliingia katika chumba chache katika mkahawa wa Acacia Premier Hotel, mjini Kisumu Agosti 30.
Anaamini kuwa hilo lilikuwa jaribio la kumuua.
“Maafisa wa ujasusi waliingia chumbani mwangu Kisumu, Agosti 30 lakini tukagundua. Tena mnamo Septemba nikiwa Nyeri kulikuwa na njama ya kuwekea sumu kwenye chakula,” Bw Gachagua akawaambia wanahabari katika Hospitali ya Karen.
Taifa Digitali ilimfikia mbunge huyo kwa kumtumia ujumbe mfupi na ule wa WhatsApp lakini hakuwa amejibu.
Afisa mmoja wa cheo cha juu serikalio ambaye ni mfuasi sugu wa Gachagua aliambia Taifa Dijitali kwamba maelezo kuhusu kanda hiyo ya siri yaliwekwa wazi kwa mara ya kwanza katika mkutano kati ya viongozi fulani wa kidini waliokutana na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi wakijaribu kuleta upatanisho kabla ya mswada wa kumtimua Gachagua kuwasilishwa katika Bunge la Kitaifa.
Afisa huyo alisema Rais Ruto aliwaeleza kwamba ako na ushahidi kwamba naibu wake anavuta upande tofauti.
Japo Rais hakutoa ufafanuzi kuhusu kanda hizo za siri, wale waliohudhuria mkutano huo wanakisia kuwa kanda hizo za siri zinasheheni mazungumzo kati ya Bw Gachagua na watu wengine.
Wiki jana, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga aliambia Taifa Dijitali kwamba viongozi fulani wa kidini walikutana na Rais Ruto katika Ikulu ya Nairobi kwa lengo la kumpatanisha na Bw Gachagua.
Bw Kahiga alichelea kutoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo japo akaongeza kuwa yeye pia aliongea na wabunge kadha kutoka Mlima Kenya katika juhudi za kumnusuru Gachagua.
Imetafsiriwa na CHARLES WASONGA